Kuna wakati utahitaji kutumia akili za ziada zaidi ya kutumia akili za darasani. Ni watu wachache mno ambao wana uwezo huo. Tunaweza kusema watu hawa ni watu “waliojiongeza” kiakili. Watu wa namna hii ni watu wanaofikiri.

“Palipo na mafanikio: Watu hawapimwi kwa urefu au ufupi, shahada za chuo au familia walizotoka, wanapimwa kwa uwezo wao wa kufikiri,” alisema David Schwartz.

Naye Henry Ford aliwahi kusema: “Kufikiri ni kitu kigumu ndiyo maana watu wachache hujihusisha nacho.”

Kumbe kama wewe hautaki kutumia kichwa chako kufikiri ni wazi kwamba utapishana na barabara yako ya mafanikio. Wewe unakwenda mashariki, mafanikio yanakwenda magharibi. Ni wazi kwamba utachukua muda mrefu kufanikiwa. Jifunze kufikiri ili ufanikiwe katika maisha yako.

Watu waliotumia vichwa vyao kufikiri ni watu walioleta mapinduzi makubwa katika dunia. Siku moja kijana akiwa amekaa chini ya mti baada ya kuchoka na safari aliangukiwa embe.

Baadaye alilichukua embe lile na kujiuliza: “Kwa nini lilianguka kutoka juu na kushuka chini na lisipae kwenda juu zaidi?” Huyu alikuwa Isaac Newton na huo ndio ukawa mwanzo wa ugunduzi wa kanuni ya uvutano (force of gravity). Kama Isaac Newton angekuwa si mtu wa kufikiri, angeweza kulila embe lile au kulitupa kwa hasira, sasa sijui kanuni ya uvutano ingetoka wapi!

Profesa wa kike mashuhuri alinunua kifaa cha kuwekea vyombo kilichohitaji kuungwa kwa nati ili kitumike. Alipofika sebuleni alijaribu kukiunganisha, lakini alishangaa baadhi ya nati zikisalia na hakujua ni mahali gani zilipaswa kuwekwa. Hivyo, aliamua kukiacha kile chombo baada ya kushindwa kukiunganisha na kurudi kazini. Jioni aliporejea alipigwa mshangao mkubwa baada ya kukuta kifaa kile kimeunganishwa vizuri na tayari kimeanza kutumika. Alimwita yaya na kumuuliza swali hili: “Nani ameunganisha kifaa hiki?” Yule dada wa kazi alijibu: “Ni mimi.” Profesa akamuuliza: “Umewezaje?” Yule dada akajibu: “Kama haujui kusoma na kuandika unatumia akili.” Kuna muda utahitaji akili za ziada ili uweke mambo sawa. Jifunze kufikiri.

“Kichwa kikubwa bila kufikiri ni mzigo kwa miguu,” ni methali ya Kiafrika. Kila kukicha watu wanalalamika kwa nini hawaoni maendeleo au hata nchi zao haziendelei. Jibu lipo wazi – watu wengi ni wavivu.

Watu wengi wakizungumzia uvivu, akili zetu hufikiri kuhusu wale tu wasiofanya kazi. Mpendwa msomaji, hebu nikwambie, kuna watu wanafanya kazi za kutoa jasho kila siku lakini bado ni wavivu.

Uvivu ninaozungumza hapa ni uvivu wa akili. Huu ndio unaoua watu wengi kuliko uvivu mwingine wowote unaoufahamu.

Haiwezekani mtu anaanza kuuza duka tangu mtoto ameanza dasara la kwanza hadi anahitimu la saba duka bado ni lile lile. Anafungua kila siku na kufunga amechelewa, lakini hakuna mabadiliko yoyote. Huyo ni mvivu.

Nchi za Asia kama ukikuta babu ni machinga wa vyombo vya jikoni, mtoto atapambana na kufungua duka aachane na umachinga. Mjukuu naye atajitahidi afungue stoo kubwa ya vyombo. Njoo sasa mtaani kwako, unakuta mama ni mama ntilie, mtoto anakuwa muuza ‘mataputapu’, yaani bora hata mama yake.

Tukijua kupambana na uvivu wa akili tutafika mbali. Mifumo mingi ya watu kufikiri imejikita katika kutengeneza pesa za kupeleka mkono kinywani wala hawawazi vingine. Kuna uvivu wa hatari unaotakiwa kukemewa.

Kuna nchi ambazo unakuta ina asilimia 7 ya wakulima, lakini wanalisha nchi nzima na kuzalisha ziada ya kuuza nje ya nchi. Kwingine unakuta kuna asilimia 30 ya wakulima, lakini nchi hiyo inakumbwa na baa la njaa.

Tunahitaji watu wanaoweza kufikiri kwa mapana na kuona ni kwa namna gani tunaweza kuondokana na uvivu huu. Tunahitaji mapinduzi katika sekta mbalimbali. Kutoa jasho tu hakumaanishi unafanya kazi kwa viwango. Umiza kichwa ufikirie kuzalisha zaidi, fikiria ni kwa namna gani unahitaji kufanya zaidi ya ulivyo leo.

Tafakari na fikiria unawezaje kwenda hatua ya ziada zaidi ya walipofika waliokutangulia. Tuache uvivu jamani.

Please follow and like us:
Pin Share