Siri ya wizi wa Sh zaidi ya milioni 121 za Hospitali ya Wilaya ya Geita imefichuliwa.

Imewekwa wazi na aliyekuwa Mhasibu wa Idara ya Afya hospitalini hapo, Frank Maganga, akimtaja aliyekuwa Mganga Mkuu wa Wilaya, Dk. Omary Dihenga, kutumia wafanyabiashara kadhaa wa mjini Geita kuchota fedha hizo kinyume cha sheria.

 

Kupitia andiko lake kwenda kwa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE), Maganga anamtaja Dk. Dihenga kuwa alichota mamilioni ya shilingi za hospitali hiyo kinyume cha taratibu kwa kutumia kampuni mbalimbali za rafiki zake.

 

Amezitaja kampuni hizo kuwa ni  M/S Bulamba Enterprises iliyochota Sh milioni 16 kupitia hati ya malipo namba 46/12 na hundi namba 125829, M/S Kamena General Traders iliyochukua Sh milioni 24 kupitia hati ya malipo namba 47/12 na hundi namba 125830.

 

Kampuni nyingine ni M/S Daremo General Traders iliyopata Sh milioni 20 kupitia hati ya malipo namba 47/12 hundi namba 125900, S/M Bulamba Enterprises iliyochota tena Sh milioni 35.4 kupitia hundi namba 126172, pia kampuni hiyo ilichukua kiasi kingine cha Sh milioni 25.9.

 

Mhasibu huyo anadai kuwa Mganga Mkuu huyo alitumia kampuni hizo kuchukua fedha hizo kwa kisingizio kuwa walikuwa wazabuni wa kutoa huduma mbalimbali katika hospitali hiyo, jambo ambalo anasema halikuwa sahihi, hivyo kusababisha baadhi ya huduma kukwama hospitalini hapo.

 

Amesema mganga huyo alikuwa anashinikiza na kusimamia malipo na kuhakikisha yanafanyika mapema, lakini pia alikuwa anatumia kampuni hizo kupandisha bei ya vifaa ili apate faida binafsi.

 

“Mwezi Februari 2011, Mganga Mkuu aliagiza OPD Cards kwa M/S Bulamba Enterprises kwa bei ya shilingi 977 kwa kila kadi moja, ambapo kwa kipindi hicho bei haikuwa zaidi ya Sh. 150.

 

Kwa hiyo aliagiza kadi 59,570 kwa shilingi 977 ambazo gharama yake ni Sh 58,200,000,” inasomeka sehemu ya andiko la Maganga. Pia katika andiko hilo,  Maganga amenukuliwa akisema, “Nitasema kweli daima kwa kila kitu nitakapopaswa kujibu juu ya tuhuma hizo, siko tayari kuubeba uovu usio wa kwangu, Dk. Omary Abdallah Dihenga hawezi uongozi.”

 

Taarifa hizo za mhasibu huyo zimekuja siku chache baada ya  Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa  Mwanza, kuwafikisha Mahakama ya Wilaya Geita watumishi watano akiwamo Dk. Dihenga, kwa tuhuma za wizi wa Sh milioni 18.75 zilizokuwa za ujenzi wa zahanati katika wilaya hiyo.

 

Wengine waliofikishwa mahakamani ni aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Benson Tatala, Abdallah Zihila na Joseph Onditi – wote walikuwa watumishi wa halmashauri hiyo.

 

Mhasibu huyo anabainisha  kuwa shughuli mbalimbali hazikufanyika hospitalini hapo kwa kile alichokiita ‘malipo hewa’. Alizitaja shughuli hizo kuwa ni pamoja na semina zenye thamani ya Sh milioni 41.8. Pia posho kwa watumishi wanaoishi na virusi vya Ukimwi kiasi cha Sh milioni 10.35 hazikulipwa.

 

Pia ukarabati haukufanyika kwa fedha za Mfuko wa Afya kiasi cha Sh milioni 98.395, usimamizi haikufanyika inavyopaswa kutokana na wahusika kukosa posho ya kulipa maofisa na madereva.

 

“Watumishi wamekuwa wakilalamika kwa kipindi kirefu bila mafanikio hadi walipoamua kutumia TUGHE Tawi la Hospitali ya Wilaya ya Geita, watumishi hawa wameweza kulipwa fedha hizo  baada ya Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya kuwaonea huruma na kuamua kuwaazimia fedha za kulipa madeni hayo kutoka akaunti ya deposit kiasi cha Sh 26,200,000.

 

“Kwa kuwa mimi ndiyo mhasibu niliyesimamia zoezi hili la ulipwaji wa madeni haya, DMO huyo hakufurahishwa na tendo hilo na kuamua kuunda majungu na kuwatumia TUGHE Mkoa, ili mhasibu wa Idara ya Afya ndugu Frank Maganga ahamishwe idara ili kuficha ubaya wake,” inasomeka taarifa ya mhasibu huyo.

 

Wakati mhasibu huyo akiweka wazi hayo, JAMHURI imeona barua yenye kumbukumbu namba GDC/CPF.578/5 ya tarehe 10/10/2011 iliyoandikwa na kusainiwa na aliyekuwa Mweka Hazina wa halmashauri hiyo, Swai Venance, ikimhamisha Frank Maganga kutoka Idara ya Afya kwenda Idara ya Utawala siku chache baada ya kuandika waraka huo wa kumtuhumu Mganga Mkuu.

 

Pia JAMHURI imefanikiwa kuona barua yenye kumbukumbu namba GDC 14/10/2011/TUGHE ya 20 Oktoba, 2011 iliyoandikwa na TUGHE kwenda kwa Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) wakati huo akiwa Kapteni George Mkuchika, kumtaka amwondoe Mganga Mkuu huyo katika hospitali hiyo.

 

Wafanyakazi hao walipiga kura 110 na kura 109 zilitaka Mganga Mkuu huyo ahamishwe wakimtuhumu kuwa alikuwa amekwapua fedha za umma kwa kufanya malipo hewa kwa wazabuni kiasi cha Sh. 121,435,960.

 

“Tuhuma za wafanyakazi kwa DMO, dawa hakuna, hospitali imezidi kuwa chafu, vibarua hawalipwi pesa zao, walipodai walifukuzwa kazi, maji hayapatikani kama inavyopaswa, maji yanauzwa mitaani, vitendea kazi havipo na wagonjwa wanajisafirisha wanapopewa rufaa kwa ukosefu wa mafuta ya magari,” inasema barua ya TUGHE kwenda kwa Waziri.

 

Hospitali ya Wilaya ya Geita ina tuhuma za kutoa huduma mbaya kwa wagonjwa kwa muda mrefu sasa na kusababisha watu mbalimbali kuilalamikia.

Mwezi uliopita, akiwa katika ziara yake ya kiserikali wilayani Geita, Waziri wa Tamisemi, Hawa Ghasia, alitembelea hospitali hiyo na kukuta matatizo mengi na kulazimika kutoa miezi mitatu kwa Mganga Mkuu na Mkurugenzi Mtendaji wa wilaya hiyo kurekebisha hali hiyo.

 

By Jamhuri