Mtoto ni malezi. Mtoto akilelewa katika malezi mazuri atakuwa na maadili mazuri. Mwanafalsafa Anselm Stolz alipata kusema, “Ukimpa mtu samaki atamla mara moja, lakini ukimfundisha kuvua atakula samaki kila siku.”

Naye mwanafalsafa Albert Einstein alisema, “Ukifikiri mwaka mmoja ujao panda mbegu, ukifikiri miaka 10 ijayo panda mti, ukifikiri miaka 100 ijayo elemisha watu.” Kwa kupanda mbegu utavuna mara moja, kwa kupanda mti utavuna mara kumi, kwa kuelimisha watu utavuna mara mia. Malezi ni msingi wa maisha ya mwanadamu.

 

Mtoto akipata malezi mazuri ni vigumu kwake kupoteza mwelekeo wa maisha. Mtoto aliyepata malezi bora ni mvumilivu. Mwanafalsafa Socrates alipata kusema, “Mtu msomi ni mwenye sifa zifuatazo: Kwanza, ni mtu anayeweza kuyatawala mazingira yake, badala ya mazingira kumtawala yeye. Pili, anakabiliana na hali zote kwa ujasiri. Tatu, anayashughulikia mambo yote kwa uadilifu. Nne, hudhibiti starehe zake na wala haharibiwi na mafanikio yake.”

 

Nami nasema mtoto aliyepata malezi bora anayatawala mazingira yoyote yale badala ya mazingira kumtawala yeye, na pia anakabiliana na hali zote kwa ujasiri bila kukata tamaa.

 

Pia mtoto aliyepata malezi bora hatawaliwi na mafanikio aliyonayo ya maisha ya mtu, malezi ni urithi wa mtu. Malezi ndiyo mwelekeo sahihi wa maisha ya mtoto.

Mwanafasafa Laurance Lee alipata kusema, “Dunia haimlipi mtu kwa yale anayoyajua bali humlipa mtu kwa yale aliyoyapata.” Malezi anayotoa mzazi au mlezi ni tofauti na malezi ya dunia. Ndiyo maana ya methali hii: Asiyefunzwa na mamaye hufunzwa na dunia.

 

Matokeo ya kukosa malezi bora ndiyo kupata taifa ambalo halina viongozi wazalendo wala wawajibikaji. Ndiyo matokeo ya kupata viongozi wa maneno na si viongozi wa vitendo. Katika ngazi ya malezi ndiyo mtoto anafundishwa heshima yake binafsi na heshima kwa wengine.

 

Uzalendo wa mtoto unafundishwa kuanzia kwenye ngazi ya familia. Ni ukweli ulio wazi kuwa mafanikio ya mtu mzima yanachangia na malezi ya utotoni.

Malezi bora si bora malezi

Malezi ni shule, malezi bora ni tunda bora kwa familia na kwa taifa. Malezi bora yanahitaji uvumilivu, upendo na kukosolewa kwa kauli nzuri. Malezi hayanunuliwi wala kuuzwa.

 

Malezi bora ni msingi bora wa maisha ya mwanadamu. Mtoto ni kama maji. Maji ukiyaweka kwenye glasi yanachukua umbo la glasi, ukiyaweka kwenye bakuli yanachukua umbo la bakuli. Mtoto ukimlea katika hali ya uvivu atachukua umbo la uvivu.

 

Tunaposikia jina la watoto wa siku hizi, jina hili limetokana na wazazi wa siku hizi. Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo. Mtoto ni malezi na malezi yana sifa zake, gharama zake na masharti yake. Kama vile unavyolinda jicho lako lisiingiwe na mchanga ndivyo unavyotakiwa kulea mtoto wako asipumbazike na mambo ya ulimwengu.

 

Mtoto anaposhindikana ni  kama vile umemwaga unga baharini huwezi tena kuuokota. Mzazi au mlezi unatakiwa uwe mlezi saa 24, unapaswa uwe mlezi siku zote saba za wiki. Kumpenda mtoto ni pamoja na kumlea katika malezi yaliyo bora. Malezi hayahitaji maneno, yanahitaji vitendo.

 

Bora malezi

Kipima joto cha ulimwengu wa sasa kipo katika malezi na kimepatikana baada ya neno BORA MALEZI kutumika katika familia nyingi.

Rais wa Marekani, John Filzgerald Kennedy, mara baada ya kuapishwa mwaka 1960 alitamka maneno haya: “Ndugu zangu wananchi wa Marekani, msiulize Marekani itawafanyia nini bali jiulizeni mtaifanyia nini Marekani.” Kwa ujumbe wa Kennedy, malezi hayahitaji utegeaji.

 

Malezi hayana likizo na hili neno bora malezi limezaa maneno mengi. Mtoto aliyepata bora malezi hana nidhamu kwa wakubwa wala kwa wadogo, anaona yote sawa. “Ukitaka kuepuka inzi tupa kibudu”. Ukitaka mtoto wako akuletee sifa, akuheshimu na kujiheshimu mpe zawadi ya malezi bora.

 

Unajua ukipenda waridi uwe tayari kuvumilia na miiba yake. Unajua si kila aliye hospitalini ni mgonjwa wala si kila anayefanya kazi Tanesco kavuta umeme kwake. Ndiyo kusema kwamba si kila anayeitwa mzazi au mlezi anatoa malezi bora. Kwa hiyo, mzazi au mlezi unapaswa utoe malezi bora.

 

Malezi ni kulea na kujilea

Mzazi au mlezi unapomlea mtoto usisahau na wewe kujilea. Neno malezi ni ndugu wa neno ukuaji. Malezi ni mwendelezo wa ukuaji wa mwanadamu. Kila hatua ina malezi yake. Huwezi ukawa mlezi mzuri kama tabia yako si nzuri.

 

Mtoto ni kama maji, yanafuata mkondo wake. Wazazi na walezi wengine ni kikwazo cha tabia ya mtoto. Mwaka 2010 nilikutana na binti fulani. Binti huyo alikuwa na umri wa miaka 30, nilipomuuliza kwanini hajaolewa aliniambia haoni umuhimu wa kuolewa kwa sababu tabia ya baba na mama yake si nzuri. Akasema bora tu awe kapera. Hii inatokana na wazazi na walezi kutojilea wenyewe na kugeukia kulea watoto peke yao.

 

Kauli nzuri katika malezi ni muhimu

SURA YA 1

Kauli nzuri ni baraka, kauli nzuri kwa mtoto ni faraja kwa mtoto, kauli nzuri kwa mtoto ni upendo. Kauli ikitumika vizuri ni baraka na ikitumika vibaya ni laana.

Mtoto anahitaji kauli nzuri, ukiwa na kauli nzuri katika malezi mtoto atafurahia utoto wake. Jaribu kutafuta kauli nzuri, jaribu kuchagua maneno ya kuongea mbele ya mtoto.

 

Unapaswa kuwa na kauli nzuri wewe mwenyewe. Kwanza jitafakari je, kauli yako ni nzuri? Ni mbaya au uko katikati? Ifanyie marekebisho kauli yako, iboreshe iwe nzuri si tu katika malezi bali pia kauli yako iwe nzuri kwa kila mtu.

 

Watoto wengi wanakata tamaa ya maisha kwa sababu ya kauli ya wazazi na walezi wao. Kauli nzuri humfumbua mtoto macho. Kauli nzuri ni moyo wa familia, ni kiunganishi cha upendo. Kauli nzuri inatia hamasa ya kuendelea mbele kifikra. Moyo wa mtu unafarijika kwa kauli nzuri.

Utatabasamu ukisikia mke wako au mume anakwambia ‘nakupenda, nakujali, nakuthamini’, ndivyo moyo wa mtoto unavyofarijika unaposikia maneno yenye kauli nzuri.

 

2: Matusi katika malezi ni sumu

Kuna baadhi ya wazazi na walezi hawachagui matusi ya kuwatukana watoto. Unakuta mzazi au mlezi anamtukana mtoto matusi ya aibu ambayo hata hayawezi kuandikwa. Matusi kama mbwa, paka, bwege, ni hatari kwa mtoto.

 

Matusi huwa ni hatari kwa mtoto. Matusi huwa yanamuathiri mtoto kisaikolojia. Kuna baadhi ya watu hawana furaha katika maisha yao kwa sababu ya kukumbuka ukatili waliofanyiwa na wazazi au walezi wao.

 

Kuna watoto wengine wanazaliwa wakiwa na ulemavu au kuna wengine wanazaliwa wakiwa wazima, lakini baadaye wanapata ulemavu. Mtoto kama ana ulemavu epuka kumtukana matusi yanayoendana na hali aliyo nayo.

 

Unakuta labda mtoto ni mlemavu wa mkono, lakini mzazi au mlezi anamtukana matusi kama mkono mmoja wewe, au unakuta mtoto ni mlemavu wa ngozi au mlezi anamtukana matusi kama mzungu koko wewe.

 

Maneno ni zaidi ya upanga. Kwa sababu unapomtukana mtoto yale maneno yanakaa moyoni mwake na akilini mwake pia. Mlezi unatakiwa kuepuka matusi ya aina yoyote ile katika malezi.

 

3: Hasira katika malezi haitakiwi

Kila mmoja anajua hasira. Hasira husababishwa na watu, matukio, kumbukumbu au matatizo yako binafsi. Hasira hutufanya tukose furaha, kumbuka hasira na furaha ni adui wanaopingana. Hasira hufanya uhusiano wako na mke wako, mume wako, watoto wako majirani na wateja kuwa wabaya.

 

Hasira katika malezi haitakiwi, kumbuka msemo huu: “Hasira hasara.” Na neno ‘ningelijua’ huwa linakuja nyuma baada ya kufanya jambo fulani au kuchukua uamuzi fulani.

 

Hasira inaweza kukuharibia biashara yako kwa kuwakimbiza wateja wako, kukuharibia kazi, ndoa yako, heshima yako na mvuto wako kwa kuwa na makunyanzi ya kudumu usoni.

 

Katika malezi, hasira inaweza kukufanya usiwafahamu watoto wako walivyo kwa sababu watakuwa wanafanya mambo wakati ambao wewe hupo, lakini ukiwapo unawaona watoto wametulia, ukitoka tu wanafanya mambo yao.

 

Jaribu kuwaachia watoto uhuru fulani uweze kumfahamu kila mmoja tabia yake ili uweze kumrekebisha.

Namna ya kuepuka kukasirika, jiulize

 

Jiulize kwanini umekasirika. Je, kuna sababu ya kukasirika? Ukifahamu chanzo cha hasira yako jitahidi sana kutulia, halafu jiambie maneno mazuri kama: “Kwanini huyu aniumize?” Baada ya kujiambia maneno mazuri jiulize tena: “Kilichonikasirisha kitadumu muda gani, je, mwaka, mwezi, wiki, au saa kadhaa baadaye?” Utagundua kwamba ni kitu cha kupita tu.

 

Endelea tena kujiuliza: “Kinachonikasirisha kweli mimi sijawahi kukifanya kwa watu wengine? Huyu anayenitukana sasa hivi mimi sijawahi kweli kuwatukana watu wengine kama mume wangu, watoto wangu, mke wangu, jirani yangu, mfanyakazi wangu, mwajiri wangu? Je, ananifanyia kwa makusudi?

 

Neno ‘kujiuliza’ litasaidia sana katika kudhibiti hasira yako. Jaribu kujipatia muda wa kujiuliza kuliko kufanya uamuzi wa haraka. Njia ya kujiuliza kwanza itakusaidia.

Ukimya

 

Mother Teresa wa Calcuta, mtawa wa Kikatoliki, alisema, “Tunda la ukimya ni sala, tunda la sala ni imani, tunda la imani ni upendo, tunda la upendo ni huduma, tunda la huduma ni amani.”

 

Ukimya ni jambo muhimu sana. Badala ya kujibu kwa hasira, hebu jaribu kukaa kimya kama dakika tano au kumi utagundua kuwa jibu utakalolitoa litakuwa la utulivu zaidi. Ukimya unakusaidia kuepuka mambo mengi.

 

4: Amani katika familia ni muhimu katika malezi ya mtoto

Amani ni lulu iliyofichika, yenye bei kubwa sana, isiyoonekana kwa urahisi, inayotafutwa kwa tamaa ya nguvu. Amani ni jambo lenye kutamaniwa na kutafutwa na watu wengi.

 

Amani katika familia ni moyo wa malezi ya mtoto. Mfarakano katika familia unawafanya watoto wengi kukimbia makazi yao na kuishia mitaani. Mzazi au mlezi unatakiwa kujenga mazingira ya amani katika familia ili mtoto akue na kujilea katika hali ya amani.

 

Mt. Fransinko wa Asizi alisisitiza sana juu ya neno amani kwa kusema, “Bwana unifanye chombo cha amani yako, mahali palipo na chuki nilete mapendo, mahali palipo na ghadhabu nilete msamaha, mahali palipo na utengano nilete umoja, mahali palipo na wasiwasi nilete amani, mahali palipo na uongo nilete ukweli, mahali palipo na kukata tamaa nilete tumaini, mahali palipo na huzuni nilete furaha na mahali palipo na giza nilete mwanga.”

 

Kukosa amani ni zaidi ya vita, na amani si jambo la kuchezewa, bila amani hakuna mali, furaha, afya wala maendeleo. Kumbuka ukiwa na amani inakuwa rahisi kujipokea ulivyo na kuwapokea wengine walivyo, lakini ukikosa amani unaweza kutafsiri mambo kinyume cha yalivyo.

 

5: Msamaha katika malezi ni zawadi

Kusamehe ni zawadi. Msamaha unatibu majeraha ya chuki, majeraha ya ugomvi, majeraha ya matumizi mabaya ya nguvu. Baba au mama anaposhindwa kutoa msamaha kwa mwenzake anajijengea ukuta wa kutosamehewa na yeye.

 

Kama wanadamu “tunaumiza” na “kuumizwa” na tunapoumizwa tunakuwa wagumu wa kutoa msamaha. Msamehe mume wako anayekunywa pombe kupita kiasi, msamehe mke wako ambaye hakutunzii siri, msamehe mtoto wako aliyepata ujauzito akiwa shuleni.

 

Wanandoa wengi wana majeraha, wamejeruhi na kujeruhiwa. Hii inatokana na kudhaniana vibaya ndani ya uhusiano wao. Mwanandoa unapaswa kukaa chini na kutafakari kwamba hiyo ndoa ni yako. Kama ndoa ni yako kuna vitu vinavyohitajika kama upendo, msamaha, furaha, uhusiano mzuri na mengine mengi.

 

Ndoa nyingi zinapoteza mwelekeo kutokana na kukosa msamaha ndani ya uhusiano wao. Unakuta mume na mke wakitofautiana kauli, mmoja anaanza kumdhania mwingine vibaya, zaidi wengine wanaweka ukabila ndani yake, udini ndani yake, mtoto anajifunza mambo ambayo mzazi au mlezi anafanya.

 

Wakati mwingine mtoto anaweza kukwambia wewe mzazi kwamba baba msamehe mama au mama msamehe baba kwa sababu anaona hali inayoendelea si nzuri.

 

0688 477 091

By Jamhuri