Kuna baadhi ya mila na desturi tulizorithishwa na wazee wetu tunaambiwa hazifai. Lakini zipo mila na desturi ambazo zinaweza kuchangia kuimarishwa kwa mahusiano ndani ya jamii. Mojawapo ya desturi hizo kwa kabila la Wazanaki ni wimbo unaojulikana kama kibanziko.

Mzee wa Kizanaki, baba mwenye nyumba, anapokaribia nyumbani kwake wakati kiza kimeingia huimba kwa sauti ya juu wimbo ambao unamtambulisha yeye kwa wote wanaomsikia. Kwa desturi unakolezwa na unywaji pombe wa kiasi, na madhumuni yake ni kuwatangazia wote watakaomsikia kuwa mzee mwenye nyumba anakaribia nyumbani.

Mwanaume yoyote ambaye atakuwa nyumbani kwa huyu mzee, na ambaye atashindwa kutoa maelezo ya kuridhisha kwanini yuko pale, atafahamu kuwa ni wakati wa kuondoka haraka. Kila mzee wa Kizanaki ana kibanziko chake.

Mzee wa Kizanaki hanyati anaporudi nyumbani kwake ili aweze kufumania. Ni tabia ambayo hailingani na rika la uzee.

Katika mazungumzo na baadhi ya wazee wa Kizanaki nimefahamishwa kuwa wazee hupendelea kuimba kibanziko kama njia ya kuwatahadharisha waviziaji badala ya kushtukiza na kujiingiza kwenye makabiliano ambayo yanaweza kusababisha majeraha makubwa au hata kifo.

Wazee wanasimulia kuwa, pamoja na kuwepo desturi hii ya kibanziko, bado yapo matukio ya fumanizi waliyoshuhudia enzi za ujana wao. Enzi za ukoloni wale walioshikwa walidhalilishwa kwa kuvuliwa nguo, kuchapwa bakora, na kutozwa faini ya ng’ombe wawili.

Kama mtemi alikuwa mlalamikaji, basi yeye aliruhusiwa kupanga faini aliyoona inastahili.

Inasemekana kibanziko kilikuwa na madhumuni mengine ya ziada. Kwa kawaida, tendo hilo haramu lilifanyika mafichoni, kwenye mashamba au vichaka, mbali na nyumba yenye ndoa. Ilikuwa ni fedheha kubwa kwa mwanaume Mzanaki alipofumania nyumbani kwake. Kwa hiyo, kwa namna moja, uimbaji wa kibanziko ilikuwa njia ya kumpa mwanya ‘mwizi’ aondoke na kuepusha aibu kwa mume mbele ya jamii.

Yawezekana kuwa chimbuko la desturi hii ya kuwapa upenyo hawa ‘wezi’ ilitokana pia na ule utamaduni wa wazazi kuwapangia ndoa watoto wao. Enzi hizo mzee mmoja na mwenzake walikutana na kufanya makubaliano kuwa watoto wao wafunge ndoa.

Baadhi ya vigezo walivyoangalia wakati huo ilikuwa binti awe anatoka kwenye familia ambayo hawana sifa ya uchawi, asiwe na magonjwa ya kurithi, na awe mchapakazi, asiwe mvivu.

Huyo mzee atarudi nyumbani na kumuarifu mwanae wa kiume kuwa umewadia wakati wa kufunga ndoa na kuwa ameshatafutiwa mchumba anayefaa. Mzee alilipa mahari na ndoa kukamilishwa bila mjadala wa aina yoyote. 

Haya masuala ya kisasa ya mtoto kuwatangazia wazazi kuwa amepata mchumba waliyekutana naye chuoni au kwenye Facebook hayakuwepo wakati huo.

Kama lilijitokeza tatizo kwenye ndoa na masuala ya michepuko, basi suala hilo lilisababishwa na watu wawili ambao pengine walikuwa tayari wamefikiria mipango yao wenyewe kujikuta ile mipango yao kupanguliwa na maamuzi ya wazazi wao kuwapangia ndoa na mtu ambaye siyo chaguo lao.

Bila shaka kuwa jamii hiyo ambayo ilitambua kuwepo kwa ndoa nyingi za kupangwa na wazazi bila kushirikisha wanandoa, iliona haina budi kukubali kuwepo kwa desturi ya kibanziko kama njia ya kupunguza makali ya ndoa za kulazimishwa.

Mzee mwingine wa Kizanaki alinisimulia kuwa zama zile, na kwa sababu ya desturi ya ndoa za kupangwa, wanandoa wawili hawakuishi kwa kupendana. Mwanaume alimuamrisha mkewe wakati wote, na mke alikuwa mkaidi kwa desturi.

Mila na tamaduni wakati huo zilimpendelea mwanaume zaidi ya mwanamke. Mwanaume ambaye hakufurahia mahusiano yake ya ndoa siyo tu aliweza kuoa mke zaidi ya mmoja, lakini aliweza pia kujiongezea kitungo, mwanamke wa nyumba ndogo.

Na kwa kweli, katika simulizi nilizosimuliwa za nyakati hizo, sikuwahi kusikia kisa cha mke kumfumania mume. 

Tukirudi kwenye suala la ubaya wa mila na tamaduni, tunaweza kwa kiasi fulani kusema kuwa kibanziko, katika kuepusha ghadhabu za mume dhidi ya mke au ‘mwizi’ aliyefika nyumbani kwa mume, ni desturi ambayo yenye manufaa kwa jamii siyo wakati huo tu ila hata kwa sasa.

Ni fedheha ndiyo husukuma watu wengi, wanaume kwa wanawake, kuchukuwa hatua dhidi ya wale wanaowakuta kujikaribisha maeneo ambayo hawatakiwi. Asichokifahamu mwenye ndoa dhidi ya mwenza wake, hakiwezi kuleta madhara kwa mtu yoyote. Kinapokuwa habari ya mtaani ndiyo matatizo yanapojitokeza.

Wapo watu wengi wamefungwa gerezani kwa sababu ya kuchukua hatua dhidi ya watu waliowakuta kwenye fumanizi. Inawezekana wengi ya hawa wanaotumikia vifungo wangekiri leo kuwa ingekuwa bora kwao kudai au kutoa talaka kuliko kutumikia kifungo gerezani kwa sababu ya kujeruhi au kuua.

Lakini watu hawafungi ndoa ili kuruhusu vitendo ambavyo, kwa desturi, havikubaliki ndani ya ndoa. Kwa hiyo, kwa maana ile ya kuficha tu aibu ya mume, tunaona kasoro kwenye kibanziko.

Kwamba kwa nyakati hizi wanandoa wanachaguana wenyewe na kuwaarifu wazazi nia ya kufunga ndoa ni jambo jema, kwa sababu linapunguza kulazimisha wawili wasioelewana kuishi pamoja. Na kwa sababu hii, tungetarajia kuwa ndoa za siku hizi zingedumu muda mrefu zaidi kuliko zile za zamani. Ukweli ni kuwa ndoa za siku hizi hazidumu.

Wazee wetu walilazimishwa kuoana, na ndoa zao ziludumu kwa muda mrefu. Hawakuchunguza kwa karibu mienendo ya wake zao, na ndoa zao zilidumu. Hawakuelewana sana na wake zao, lakini ndoa zao zilidumu.

Vijana wetu siku hizi wanachumbiana wenyewe, wanafuatana kama kumbikumbi kila mahala, na huonekana wanapendana kwa kila hali, lakini ndoa zao hazidumu sana.

Pamoja na hitilafu zake, labda siyo wazo baya kuanza kufundishana kibanziko. Kama Wazanaki tumefundisha dunia nzima kutumia neno kung’atuka, haitakuwa jambo gumu kufundisha kutumia kibanziko.

2956 Total Views 1 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!