Mwalimu-Julius-Kambarange-Nyerere

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Watanzania mwaka huu wanaingia kwenye Uchaguzi Mkuu wa tatu, bila ya mwasisi wa Taifa hili, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Taarifa zinasema kwamba Nyerere alizaliwa mwezi kama huu, tarahe 13 (ya jana), mwaka 1922 na kwamba kama angelikuwa hai, jana angesherehekea miaka 93 tangu kuzaliwa kwake. Tutafakari.


Historia inatueleza kuhusu mambo mbalimbali yaliyopita. Historia ya Mwalimu Nyerere imeelezwa mara nyingi katika maeneo mbalimbali, lakini kwa kuwa muda unapita na wengine wanazaliwa wengine wakikua, historia hiyo haina budi kuwa ikiendelea kuelezwa.
Kutokana na umaarufu wake, watu wengi katika kila pembe ya dunia wamekuwa wakifuatlia na kutaka kujua historia yake. Gazeti la JAMHURI linakueleza historia hiyo kwa ufupi ya Mwalimu Nyerere.
Julius Kambarage Nyerere alikuwa Rais wa Kwanza wa Tanzania ambaye aliingia madarakani Oktoba 29, 1964 hadi Novemba 5, 1985, alipostaafu na kurithiwa na Alhaj Ali Hassan Mwinyi. Mwaka 1962 baada ya Uhuru hadi 1964 wakati wa Muungano alikuwa Rais wa Tanganyika.
Nyerere alizaliwa Aprili 13, 1922 katika Kijiji cha Butiama, mkoani Mara na kufariki dunia Oktoba 14, 1999 jijini London, Uingereza.


Mwalimu Nyerere alikuwa mtoto wa kiongozi wa kijadi, Chifu Nyerere Burito, na alipewa jina la Mwalimu kutokana na taaluma yake, akifundisha wanafunzi kabla ya kujiunga na masuala ya siasa.
Mwalimu Nyerere alianza kuhudhuria masomo katika Shule ya Msingi ya Serikali Musoma akiwa na umri wa miaka 12 ambako alimaliza programu ya mafunzo ya miaka minne kwa miaka mitatu na kwenda shule ya Sekondari ya Wavulana ya Tabora.


Baadaye alipata ufadhili wa kwenda Makerere, Uganda alikopata Diploma ya Ualimu. Alirejea Tanganyika (wakati huo) na kufanya kazi miaka mitatu katika Sekondari ya St. Mary’s mjini Tabora, ambako alikuwa akifundisha masomo ya Baiolojia na Kiingereza.
Mwaka 1949 alipata ufadhili wa kwenda masomoni kwenye Chuo Kikuu cha Edinburgh, Uingereza na alikuwa mwanafunzi wa kwanza kutoka Tanzania kupata nafasi katika chuo hicho ambako alipata shahada ya juu (MA) katika masuala ya uchumi na historia mwaka 1952.
Kwa elimu aliyopata chuoni hapo alianza na kuendeleza mfumo wa kijamaa uliounganishwa na baadhi ya nchi za Bara la Afrika na ambao ulikuwa na msukumo katika kupigania uhuru.


Aliporejea Tanganyika, Mwalimu Nyerere alichukua nafasi ya kufundisha masomo ya Kiingereza, Kiswahili na Historia katika Chuo cha St. Francis (sasa Sekondari ya Minaki) karibu na mji wa Dar es Salaam.
Akiwa shuleni hapo ndipo, kwa kushirikiana na viongozi wengine, walifanikiwa kuanzisha chama cha TANU. Harakati zake za kisiasa zilisababisha utawala wa kikoloni kumwangalia kwa makini na kumtaka kuchagua kati ya siasa au kuendelea kufundisha.
Kuna wakati alikaririwa akisema, “Nilikuwa mwalimu taaluma niliyoipenda kwa kuichagua mwenyewe, lakini niliingia kwenye siasa kama ajali.”


Alijiuzulu kufundisha na kujiingiza kwenye masuala ya siasa huku akishiriki kuwakusanya watu mbalimbali. Mwalimu Nyerere alisafiri sehemu mbalimbali nchini na kuongea na watu wa kawaida, machifu na wengineo mbalimbali kujaribu kuwashawishi kushiriki katika kudai uhuru.
Pia alizungumza kwa niaba ya chama cha TANU katika mkutano wa Umoja wa Mataifa, mjini New York, Marekani kuhusu nia ya kutaka kujitawala.


Uwezo wake wa kujenga hoja na umakini katika kuzungumza vilisaidia kufanya TANU ifanikiwe kuwezesha Uhuru kupatikana kwa njia ya amani bila umwagaji damu. Baadhi ya watu wanamtaja Gavana Sir Richard Turnbull kuwa alifanikisha Uhuru kupatikana.
Katika kipindi cha mwaka 1958-1960 aliteuliwa kuwa mmoja wa mawaziri katika Serikali ya kikoloni kabla ya kujiuzulu na kuingia kwenye Uchaguzi Mkuu na TANU kushinda, hivyo kuwa Waziri Mkuu wa Kwanza wa Tanganyika kuanzia Desemba 1961 hadi mapema mwaka 1962.
Baadaye akaendelea kupambana ili nchi iwe jamhuri na yeye kuwa Rais wa Kwanza wa Tanganyika kuanzia Desemba 9, 1962 ilipokuwa jamhuri.


Kipindi kilichofuata, Nyerere alikuwa chachu katika kuleta Muungano wa Tanganyika na Zanzibar baada ya Mapinduzi yaliyomwondoa madarakani Jamshid bin Abdullah, aliyekuwa Sultani wa Zanzibar.
    
HISTORIA YA NYERERE KISIASA
1958 – Mwanachama mwanzilishi wa TANU.
1958 – 1960 – Mjumbe wa Baraza la Kutunga Sheria.
1958 – Kiongozi wa upinzani bungeni.
1961-1962 – Waziri Mkuu, Serikali huru ya Tanganyika.
1962 – Alichaguliwa kuwa Rais wa Kwanza wa Tanganyika.
1963-1970 – Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afrika Mashariki.
1964-1985 – Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
1970-1985 – Mkuu wa Chuo Kikuu cha Tanzania.
1977-1990 – Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi.
1984-1985 – Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine.
1985 – Rais Mstaafu
1999 – Kufariki dunia kwa ugonjwa wa mkanda wa jeshi (leukemia) mjini London, Uingereza.
       
SERA ZA NYERERE KIUCHUMI
Alipokuwa madarakani, alitekeleza sera ya kiuchumi ya kijamaa pale alipotangaza Azimio la Arusha, na kuanzisha ushirikiano wa karibu na baadhi ya mataifa na hasa China.


Japokuwa baadhi ya sera kwa nchi za Magharibi zilionekana za kijamaa zaidi au kikomunisti, lakini Mwalimu Nyerere alikuwa na mapenzi makubwa na Bara la Afrika.
Mwalimu Nyerere aliwaonea huruma na kuwaamini zaidi wananchi wa vijijini katika maeneo mbalimbali ya Bara la Afrika na alithamini na kuheshimu utamaduni wao wa aina ya maisha yao. Aliamini kuwa maisha yanaweza kuboreshwa au kuendelezwa kwa kufuata misingi ya Ujamaa bila kuathiri utamaduni wa Waafrika.
Kilichokuwa kinahitajika, kwa imani ya Mwalimu Nyerere, ni kuendeleza ujamaa, jambo litakalofanya mfumo wa ubepari kusahaulika.
Mwalimu, kwa mujibu wa wanahistoria, aliamini kuwa nchi za Kiafrika zinatakiwa kurudi kwenye mfumo wa Ujamaa na Kujitegemea ambao ni wa jadi kwao.


Mfumo wa Ujamaa ulikuwa na faida zake, lakini kwa upande mwingine ulishindwa kuinua kilimo hadi ilipofika 1976 ambako uamuzi wa kuwalazimisha watu kwenda kuishi kwenye Vijiji vya Ujamaa ulipokoma.
Katika kipindi hicho, Tanzania ilibadilika kutoka kwenye taifa lililokuwa likiuza kwa wingi nje bidhaa za kilimo na kuwa taifa lenye kuagiza bidhaa hizo kutoka nje.


Mwaka 1985 Mwalimu Nyerere alitangaza kung’atuka madarakani, uamuzi ambao ulitoa nafasi ya kuwapo kwa mfumo mwingine wa uchumi, mfumo wa soko huria chini ya uongozi wa Ali Hassan Mwinyi.
Baada ya kustaafu, mchango wa Mwalimu Nyerere ulisaidia kuingia madarakani kwa marais wastaafu —  Mwinyi na Benjamin Mkapa. Mchango huo ni pamoja na kushiriki kwenye kampeni na kuhudhuria vikao vya uteuzi.
Baada ya kustaafu urais, Mwalimu Nyerere aliendelea kuwa Mwenyekiti wa CCM kwa miaka mitano hadi mwaka 1990 na hadi sasa anatambulika kama Baba wa Taifa.

SERA ZA NJE
Mwalimu Nyerere ni mmoja kati ya viongozi wa Afrika ambao walishiriki kikamilifu kupigania uhuru wa nchi zao na nchi nyingine za Afrika katika kipindi cha miaka ya 1960.
Nyerere alikuwa kiongozi ambaye alikemea kwa nguvu zake zote vitendo vya rushwa, huku mwenyewe akionesha hivyo kwa mifano.   Pia ni mwasisi wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) mwaka 1963.


Wakati wa utawala wake, Mwalimu Nyerere aliifanya Tanzania kuwa ni sehemu ya makazi ya wapigania uhuru wa nchi kadhaa za Kiafrika ikiwamo wa Chama cha African National Congress (ANC) na Pan African Congress (PAC) vya Afrika Kusini, FRELIMO ya Msumbiji wakati ikijiandaa kumwondoa madarakani Mreno aliyekuwa akiitawala nchi hiyo.


Alimsaidia Robert Mugabe (sasa Rais wa Zimbabwe) wakati wa kupambana na utawala wa walowezi na kwa kushirikiana na viongozi wengine kama Rais mstaafu Kenneth Kaunda wa Zambia, aliongoza nchi za ‘Mstari Mbele’ katika ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika.
Mwaka 1978 aliongoza Tanzania katika vita dhidi ya Uganda wakati huo ikiwa chini ya dikteta Idi Amin, na matokeo yake Amin alipigwa kiasi cha kukimbia nchi yake na kwenda kuishi uhamishoni.


Kwa ujumla sera za nje za Mwalimu Nyerere kimataifa zilikuwa za kutofungamana na upande wowote. Chini ya sera hizo, Tanzania iliweza kufaidika na uhusiano wa mataifa yote ya Magharibi na Mashariki.

NYERERE BAADA YA URAIS
Licha ya kustaafu urais na uenyekiti wa CCM, Mwalimu Nyerere aliendelea kuwa mkali na hasa kuhusu masuala ya kuongezeka kwa vitendo vya rushwa na kwa viongozi wanaojihusisha na rushwa.
Nyerere alisema anang’atuka na baada ya hapo alirejea kijijini kwake Butiama ambako, licha ya kuishi maisha ya kawaida, aliendelea na kutembelea nchi mbalimbali duniani na kukutana na viongozi wa kitaifa na alikuwa akizipigia debe nchi masikini na kuziombea misaada.


Inasadikiwa kuwa baada ya kustaafu, aliweza kusafiri katika nchi nyingi kuliko alivyofanya alipokuwa madarakani. Miongoni mwa majukumu makubwa aliyokuwa nayo baada ya kustaafu ni kuwa msuluhishi wa mgogoro wa Burundi mwaka 1996 hadi kifo chake.
Baada ya kifo chake, mwaka 1997 Kanisa Katoliki la Musoma lilifungua mchakato ambao unaomba Julius Nyerere kuwekwa katika kada ya utakatifu. Mwalimu alikuwa muumini mzuri na aliyekuwa akihudhuria bila kukosa ibada na kufunga mara kwa mara.

SHAHADA ZA HESHIMA ALIZOTUNUKIWA:

Chuo Kikuu cha (Marekani)
Chuo Kikuu cha Cairo (Misri)
 Chuo Kikuu cha Ibadan (Nigeria)
Chuo Kikuu cha Liberia (Liberia)
Chuo Kikuu cha Toronto (Canada)
Chuo Kikuu cha Howard (Marekani)
Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru (India)
Chuo Kiku ucha Havana (Cuba)
Chuo Kikuu cha Lesotho (Lesotho)
Chuo Kikuu cha Philippines (Philippines)
Chuo Kikuu cha Fort Hare (Afrika Kusini)
Chuo Kikuu cha Sokoine (Tanzania)

TUZO
Tuzo ya Nehru ya Uhusiano wa Kimataifa, 1976
Tuzo ya mchango wake kwa Dunia ya Tatu, 1982
Medali ya Nansen kwa kuhudumia wakimbizi, 1983
Tuzo ya Amani ya Lenin, 1987

Katika kipindi cha uhai wake, Mwalimu Nyerere pia alifanikiwa kutunga vitabu vingi mbalimbali na ambavyo vinatumika katika vyuo na taasisi nyingi duniani.

5222 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!