Awali ya yote napenda nichukue fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu ambaye kwa mapenzi yake anatujaalia afya njema.
Si kwamba sisi tunastahili kuliko waliokufa, bali sisi kuwapo kwetu hadi leo ni kwa rehema na neema yake tu Mwenyezi Mungu.


  Kutokana na hali hiyo, tunaendelea kupumua na kuyafanya yote tunayofanya kila siku. Hivyo ni lazima tulihimidi na kulisifu jina lake takatifu: kila mwenye pumzi na amsifu Mwenyezi Mungu aliye kiini cha uhai wetu pamoja na mema yote.
 Baada ya utangulizi huo mfupi, naomba kupitia makala hii tusaidiane katika kulitafakali suala zima la AMANI ndani ya nchi yetu. Sasa tunasema ni takribani miaka 54 tangu Tanganyika ipate Uhuru kutoka kwa wakoloni (Waingereza) na ni miaka 51 tangu Tanganyika na Zanzibar ziungane na kuwezesha kuanzishwa na kuwapo Taifa la Tanzania likiongozwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano.


Miaka 50 si kidogo kwa maisha ya binadamu: ni muda wa kutosha. Hivyo tunamshukuru sana Mungu Mwenyezi kwa kutujaalia kuishi kwa miaka hiyo kwa utulivu, umoja na amani.
Hata hivyo, kwa miaka ya hivi karibuni kumekuwapo na malalamiko kutoka miongoni mwetu kwamba kumekuwa na dalili au viashiria vya uvunjifu wa AMANI katika nchi yetu.


Hali ya uvunjifu wa amani imekuwa ikiongezeka hasa kwa miaka ya hivi karibuni. Mathalani, mauaji ya Watanzania wenye ulemavu wa ngozi (albino) yameshamiri kwa miaka ya karibuni, na ni kiashiria kimojawapo kwamba kupitia mauaji hayo ambayo inaelekea ni kutokana na imani za kishirikina, tunahatarisha amani ndani ya Tanzania.


Kwa mfano, inasemekana kuwa wapo wanaotafuta viungo vya albino kwa ajili ya kuvitumia kwenye shughuli zao za machimbo ya madini au kwenye shughuli za uvuvi, na wengi kuvitumia kutafutia nafasi za uongozi.
 Haya yote yanafanyika kutokana na mawazo potofu na ni hali ya hatari kwa amani katika jamii yetu. Kwanza, hofu inakuwa kubwa sana kwa jamii; pili ni vigumu kuwalinda albino kwa msingi kuwa wanaotafuta viungo vyao ni watu wenye dhamira mbaya sana na watatumia kila aina ya hila kuweza kumdhuru albino.
Vilevile, kwa miaka ya hivi karibuni Watanzania wengi wamekuwa wanalalamika kuwa polisi, wakiwa chombo maalum cha kitaifa, kinachotakiwa kuwalinda raia wote pamoja na mali zao; badala yake polisi wamewageuka raia kwa kuwapiga kwa kutumia virungu, mabomu ya kumfanya mtu atokwe na machozi pamoja na maji ya kusababisha mwili kuwashwawashwa na hata bunduki za moto.


Haya yote yanahatarisha maisha ya Watanzania na badala ya kuwahakikishia usalama na kuishi kwa amani, inaonekana ni kinyume chake. Pamoja na ukweli kwamba kwa kiasi kikubwa polisi wanafanya kazi nzuri lakini ikitokea polisi wachache wakazitumia vibaya nafasi walizonazo wakiwa polisi, basi jamii inaona Jeshi la Polisi halifai au halitimizi wajibu wake vizuri kwa raia.


 Kwa upande mwingine tunajiuliza kwa nini watu wapigwe, hata kama wamevunja sheria za nchi wakati chombo cha kutoa haki, yaani Mahakama kipo? Kama kutatokea wavunja sheria za nchi badala ya polisi kuwapiga waliovunja sheria, wawakamate na wawafikishe mbele ya Mahakama ili haki itendeke kupitia mkono wa sheria.
Polisi kutumia rungu au silaha ya aina yoyote ile na kuwapiga raia siyo sahihi hata kidogo. Hii ni hali ya kuhatarisha amani, pia ni vitendo vya kuashiria hali ya kushindwa kutenda haki. Kwa hali hiyo polisi wanakuwa hawazitumii nafasi zao kama maafisa wa kulinda na kudumisha usalaama wa raia na hivyo kuhatarisha uwepo wa AMANI nchini.


Tujiulize imekuwaje mpaka hali hiyo inayoashiria kutoweka kwa AMANI ambayo tumeizoea na tumekuwa nayo zaidi ya miaka hamsini sasa ianze kujitokeza siku hata siku? Mimi naamini kuwa suala zima la kuhakikisha kuwa tunaishi kwa amani ni jukumu la kila mmoja wetu kwa nafasi zetu tulizo nazo katika familia, jamii na kama taifa la Tanzania.
Nafasi uliyonayo wewe au niliyonayo mimi ndani ya familia ikitumika vizuri na ipasavyo, amani ndani ya familia itakuwapo. Lakini kinyume cha hapo yaani tusipofanya yanayotakiwa kuyatimiza kwa faida ya familia zetu, siyo siri kwamba amani ndani ya familia zetu italegalega.
Mathalani, baba ukitumia vibaya nafasi uliyonayo kama mkuu wa familia kwa kuzitumia vibaya rasilimali za familia kwa manufaa yako binafsi, halitakuwa jambo jema kwa familia yako. Kwa kufanya hivyo unasababisha ukosefu wa furaha ndani ya familia na furaha ikikosekana upendo katika famlia nzima hautakuwapo na mwishowe ni kukosa amani. Hivyo amani ikikosekana katika familia nyingi hali kama hiyo itajitokeza katika jamii na kwa Taifa pia.


Tujiulize je, tunatumia vipi nafasi tulizo nazo katika nchi na hasa tunapokuwa viongozi au watawala kwa ngazi zote: kuanzia vijijini hadi taifa, kuhakikisha kuwa amani inakuwapo wakati wote au tunatumia nafasi tulizo nazo kuhatarisha amani iliyopo?
Kusema kweli nafasi inaambatana na cheo au madaraka, kitu kinachotakiwa kuambatana na kutimiza wajibu wetu ipasavyo kwa faida ya wote. Hili likifanyika vizuri na kwa maadili makubwa yaani kila mwenye nafasi akatimiza wajibu wake kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa iwe katika familia zetu, kwenye jamii na katika taifa letu: matunda au matokeo yake yatakuwa ni UPENDO, KUTENDA HAKI na mwisho wa hayo yote ni kuwapo kwa AMANI.


Bila kupendana kwa dhati na kutendeana haki kifamilia, kijamii na kitaifa hatuwezi kuwa na amani ya kweli. Kwanza, ndani ya mioyo yetu na pili, katika mazingira yanayotuzunguka yaani ndani ya jamii na Taifa. Panapokuwa na hali ya kupendana, haki na amani na hata maendeleo endelevu yatapatika na watu kufurahia maisha katika familia, jamii na ndani ya Taifa lao.


Lakini iwapo nafasi tulizo nazo: kama viongozi ndani ya familia zetu, kama viongozi wa Serikali kwa ngazi zote (rais, makamu wa rais, waziri mkuu, mawaziri, makatibu wakuu, wakurugenzi, makamishna na kadhalika); viongozi wa vyama vya siasa; viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini (mashehe, maaskofu, mapadri, wachungaji, wainjilist, mitume, wazee wa kanisa au waamini wote na kadhalika); wakuu wa mashirika ya umma na sekta binafsi (ikiwamo wenye viwanda, machimba madini, wenye biashara mbalimbali, mabenki au taasisis za fedha na kadhalika); pia tukiwa kama wanajeshi, polisi, magereza, mahakama (mahakimu, majaji, wasajili wa mahakama, mawakili na kadhalika), wakuu wa vyombo vya habari na wanahabari wote (waandishi, watangazaji, wapiga picha na kadhalika); wakuu wa shule na vyuo (pamoja na wanafunzi kwa ngazi zote), wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, watendaji tarafani na katika kata na vijijini; viongozi katika Serikali za Mitaa (ikiwamo madiwani); viongozi wa asasi zisizo za kiserikali; viongozi ndani ya sekta binafsi, na nafasi yetu kama Watanzania wote (wafanyakazi, wakulima na wafugaji): tutazitumia vibaya ieleweke kuwa badala ya kuzaliwa haki katika familia, jamii au taifa tutazalisha chuki na kukosekana upendo wa kweli ndani ya Taifa letu.


 Ikiwa hivyo ndivyo, chuki itazaa shida nyingi na migogoro kibao na hatimaye nyufa na migongano ya kimaslahi hatimaye ni kukosekana AMANI. Vilevile, kila mmoja wetu akae akijua kuwa ikikosekana amani Taifa halitatawalika kidemokrasia bali itakuwa ni kutumia mabavu tu na wananchi hawatakuwa na nafasi au fursa za kutulia ndani ya Taifa lao.
Kutokana na maeleza na ufafanuzi nilioutoa kupitia makala hii, naomba suala la kudumisha AMANI ndani ya nchi yetu tuliangalie kwa pamoja na kwa umakini kubwa. Kila mmoja wetu ajipime na kujiuliza anaitumia vipi nafasi aliyonayo katika nchi yetu ili kuweza kudumisha amani tuliyokuwa nayo kwa miaka mingi?
Kama wewe ni kiongozi ndani ya serikali tawala, au ni kiongozi ndani ya vyama vya siasa, au wewe ni mshauri mkuu wa rais, au wewe ni mwenye madaraka ya kufanya uamuzi au kutunga sera, mwenye madaraka ya kusimamia utekelezaji wa sheria mbalimbali za nchi, uwe ni mchumi, mchambuzi (analyst), uwe ni mwenye kupanga mipango (planner) au uwe ni mfanyabiashara, mkulima, mfugaji na kadhalika: ujiulize na ujipime utaitumia vipi nafasi uliyo nayo kuiletea Tanzania maendeleo endelevu ikiwa ni pamoja na kudumisha amani?


Je, kwa kuzingatia nafasi uliyonayo katika jamii unajitahidi kuzalisha HAKI au unazalisha CHUKI? Je, nafasi yako inaashiria kuwapo AMANI au VITA? Katika kuyatafakari haya yote, tusisahua kuwa nafasi tulizonazo katika jamii na taifani zinaambatana na kutimiza wajibu wetu vizuri.
Je, ni kweli unatimiza wajibu wako kwa kutenda haki na bila kubagua mtu yeyote? Kutenda haki kwa wote na kwa kuzingatia taratibu, kanuni na sheria za nchi ni jambo la msingi sana. Vilevile, kutendeana haki ndani ya familia zetu (baba, mama na watoto na wengineo tunaoishi nao ikiwamo watumishi katika nyumba zetu) na haki katika jamii kwa ujumla wake, itatuhakikishia kuwapo na amani ya kweli kwa faida ya wote.


Kwa siku hizi za karibu kila kona ninayopita utasikia wengi wakilalamika kuwa “Tanzania siasa imekuwa karibu na kila kitu wakati hali ya maisha inazidi kuwa ngumu kila kukicha”. Je, kuna nini ndani ya nyanja za siasa katika nchi yetu mpaka wengi tuone kila kitu kuwa ni siasa? Bila shaka na kwa mtazamo wa wengi katika siasa kuna nafasi ya kupata “madaraka na kujihakikishia “ulaji wa kila aina” ikiwa ni pamoja na fursa za kujinufaisha na kutajirika haraka”.


Kama hivyo ndivyo, ni dhahiri kuwa wengi wetu tunavutiwa kuwa wanasiasa iwapo baadhi ya wataalamu kuvutiwa na kukimbilia siasa badala ya kubobea zaidi katika taaluma zao. Je, kuna visababishi gani vinavyowavutia hasa baadhi ya wataalamu wazamie katika siasa kuliko taaluma walizozisomea?
Nini hasa kimesababisha hali kuwa hivyo? Kikubwa ni jinsi wanasiasa walivyotumia nafasi zao kama viongozi na wafanya uamuzi (leaders and decision-makers) kuweza kujipendelea na kujiwekea fursa za kujinufaisha kimaslahi na kuhalalisha kisheria.


Mathalani, ni mamilioni ya shilingi wanayolipwa baada ya miaka mitano ya ubunge kama mafao ya kutumikia umma kwa kipindi hicho kifupi. Si hilo tu, hata mshahara na marupurupu ya mbunge ni kivutio kizuri na hali hiyo inawafanya watu wapende kuwa wabunge kwa sababu watanufaika zaidi kuliko kitu kingine.
 Hakuna mtumishi mwingine katika utumishi wa umma anayeweza kupata fedha kiasi hicho kwa muda mfupi katika utumishi wake isipokuwa ni mbunge tu. Pengine wapo wachache ambao wameajiriwa kwenye taasisi za kimataifa ambazo kwa uwezo wao kifedha, zinaweza kuwalipa Watanzania mishahara mikubwa na marupurupu ya kutosha.


Pamoja na hayo yote, je, waheshimiwa wabunge wanazitumia vipi nafasi zao kama wabunge katika kuhakikisha kuna haki na amani ndani ya Taifa letu? Je, mheshimiwa Spika, mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu, waheshimiwa mawaziri, mheshimiwa mwanasheria mkuu (akiwa bungeni), waheshimiwa wenyeviti bungeni, waheshimiwa wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge na wajumbe wa kamati mbalimbali wote katika ujumla wao wanazitumia vipi nafasi walizo nazo ndani ya Bunge la Jamhuri wa Tanzania?    


 Tujiulize, je, kupitia Bunge tunadumisha HAKI na AMANI nchini mwetu? Wakati mwingine huwa tunasikia wakisema Mheshimiwa Spika na Bunge lako Tukufu; je, utukufu wa Bunge umejengeka katika misingi gani? Au ni vigezo vipi vinatumika kuashiria utukufu bungeni? Je, ni sawa kwa mheshimiwa mbunge kutumia nafasi yake akiwa ndani ya jengo la Bunge kutumia lugha isiyoridhisha? Kwa mfano, kumkashifu mbunge mwenzake au kutosema ukweli wakati anatakiwa kusema ukweli daima na fitina kwake kuwa ni mwiko?


Kupitia makala hii, niwaombe sana Watanzania watakaopata nafasi katika Serikali ya Awamu ya Tano ya Utawala wa Tanzania; na wale ambao tayari wanazo nafasi mbali mbali za kufanya uamuzi na pia watunga sera; wote wazitumie nafasi hizo kwa manufaa ya Watanzania wote.
  Haipendezi hata kidogo kuona au kusikia baadhi ya walio na nafasi nyeti katika uongozi wa Taifa letu, wanazitumia nafasi walizopewa kupitia ridhaa ya wananchi: kwa kupigiwa kura au kwa kuteuliwa na mamlaka husika, na wakazitumia nafasi hizo kwa manufaa yao binafsi huku wakiwaacha wananchi wakiteseka. Kama Taifa linaloendelea ni vizuri kuwapo utaratibu mzuri wa kuratibu ipasavyo shughuli za kitaifa kwa lengo la kuhakikisha tunatenda haki; tunadumisha upendo kati ya Watanzania na mwisho ni kuona Watanzania tunaishi kwa AMANI na furaha.


Hali kama hiyo itakuwa na tija iwapo kutakuwa na misingi mizuri kwa viongozi wa ngazi zote kuwa na nidhamu ya hali ya juu; kuwa wenye maadili mazuri na kuwajibika ipasavyo kwa Watanzania ambao ndiyo wanaowaweka kwenye uongozi au kuwawezesha kuwa na madaraka.
  Haya yakiwapo, yakazingatiwa na kuheshimiwa na wote wenye NAFASI za kufanya uamuzi au kwa wanaoratibu na kusimamia sheria za nchi na kila mmoja akatimiza wajibu wake vizuri, tutakuwa tumeweka misingi imara ya kudumisha amani nchini mwetu.
INAWEZEKANA TIMIZA WAJIBU WAKO, TENDA HAKI NA DUMISHA AMANI NCHINI KWA FAIDA YETU SOTE.

By Jamhuri