Itakuwa si haki kukaa bila kuona na kuthamini mchango wa serikali katika kuleta maendeleo ya nchi.

Kwa namna moja ama nyingine, mambo mengi ya kimaendeleo yamekuwa yakifanyika siku hadi siku hapa nchini kwetu, ambayo ukiyatazama yameendelea kutupa sifa sisi kama taifa.

Sifa ambazo zinatufanya kutembea kifua mbele kwa wenzetu kutokana na serikali hii kupigana kiume kuhakikisha sifa hizo zinaendelea kudumu kwa vizazi vya sasa na hata vya baadaye.

Kwa kuzingatia hilo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli wakati anaingia madarakani aliahidi kuboresha masuala mbalimbali, ikiwemo elimu, afya, miundombinu ya maji, umeme, barabara, kilimo na usafiri wa anga.

Yote haya anayafanya kuhakikisha kuwa Watanzania wanapata maendeleo ya kweli na kulenga kuwa taifa linafikia uchumi wa kati na wa viwanda ifikapo mwaka 2025.

Hivi karibuni, tumekuwa tukishuhudia ukuaji mkubwa wa sekta ya anga ambapo serikali kupitia Rais Magufuli ilihakikisha inalifufua Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), kwa kununua ndege 11 aina tofauti tofauti ili kuhakikisha inakuza sekta hii.

Serikali haikuishia tu katika ununuaji wa ndege hizo, bali pia ilisema itajenga na kuboresha viwanja vya ndege mbalimbali kikiwemo Kiwanja cha Msalato, Songwe, Tabora, Mtwara na Mwanza. Lengo likiwa ni kuviwezesha viwanja hivyo kufikia kiwango cha kimataifa cha kuruhusu ndege kubwa na ndogo kuweza kutua katika viwanja hivyo.

Kwa mantiki hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, anayeshughulikia Sekta ya Ujenzi, Mbunifu Majengo, Elius Mwakalinga, alifanya ziara ya kikazi katika Kiwanja cha Ndege cha Mtwara ili kujionea kazi za upanuzi wa kiwanja hicho ambacho ni moja kati ya viwanja 11 ambavyo vimo katika mkakati wa kuboreshwa.

Wakati akiwa katika ziara hiyo, Mwakalinga alisema kuwa ameridhishwa na mradi wa upanuzi wa ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Mtwara ambao unajengwa na mkandarasi M/S Beijing Construction Engineering Group Company Ltd na kugharimu Sh bilioni 50.3. 

Akizungumza wakati akikagua kiwanja hicho ambacho utekelezaji wake umefika asilimia 31, Mwakalinga alifafanua kuwa kukamilika kwake kutafungua fursa nyingi za uwekezaji katika mkoa huo na kutasaidia kurahisisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Hata hivyo, Mwakalinga alibainisha kuwa mkandarasi anaendelea kutekeleza kazi zake vizuri kwani kazi nyingi za awali ambazo zinahusisha upanuzi wa uwanja huo zimefanyika kwa asilimia kubwa.

“Hadi sasa kazi inaendelea vizuri, ukiangalia kazi nyingi za awali zimeshafanyika, kinachotakiwa kwa sasa ni kwa mkandarasi kuendelea na hatua zinazofuata ili kukamilisha kazi hiyo kwa mujibu wa mkataba,” anasema Mwakalinga.

Ametaja kazi hizo za awali ambazo zilikamilishwa na mkandarasi huyo kuwa ni kuchimba eneo kwa ajili ya kuacha nafasi ya kuweka tabaka mbalimbali za barabara ya kurukia na kutua ndege pamoja na kuweka lami nyepesi juu ya tabaka lililochanganywa na saruji katika barabara hiyo ambayo imefika asilimia 46.

Aidha, ameongeza kuwa kiwanja hicho ambacho kilijengwa kwa mara ya kwanza na kuanza kutoa huduma katika miaka ya 1952/53 hakikidhi mahitaji ya ukuaji wa uchumi, hivyo serikali imeamua kupandisha daraja kiwanja hicho ili kuweza kuhudumia ndege kubwa za ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mkoa wa Mtwara, Mhandisi Dotto Chacha, amesema kuwa upanuzi wa kiwanja hicho unahusisha ujenzi wa barabara ya magari ya kuingia na kutoka kiwanjani pamoja na maegesho ya magari.

“Tunatarajia ujenzi huu utakidhi viwango vya kimataifa kwa kuongeza daraja kutoka ‘code 3C’ ya sasa kwenda ‘code 4E’ na itahusisha ujengaji wa uzio wa usalama kuzunguka kiwanja, uwekaji wa mfumo wa umeme wa akiba, vifaa vya zimamoto pamoja na taa na alama za kuongozea ndege,” anafafanua Chacha.

Licha ya uboreshaji wa sekta ya anga, serikali pia inaboresha miundombinu kama ya barabara katika mkoa huo ambapo katika ziara hiyo Mwakalinga alikagua Barabara ya Mtwara – Nanyamba – Tandahimba – Newala – Masasi sehemu ya Mtwara – Mnivata (Km 50) na kusema kuwa utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 75.67.

Mwakalinga amebainisha kuwa asilimia hiyo inahusisha ujenzi wa makalvati madogo 41 kati ya 43 pamoja na ujenzi wa makalvati makubwa manne kati ya sita ambayo nayo yamekamilika kwa asilimia mia moja.

Awali wakati akielekea mkoani Mtwara, Mwakalinga alikagua mzani wa sisi kwa sisi uliopo mkoani Ruvuma na kuwataka watumishi wa mzani huo kuwa mfano wa kuigwa na watumishi wengine kwa kuepuka vitendo vya rushwa na kufanya kazi kwa uadilifu.

Kwa ujumla, Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoani Mtwara unaendelea kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kadiri inavyopokea fedha kutoka serikalini na kwamba miradi hiyo ikikamilika itafungua na kukuza fursa za kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa Mkoa wa Mtwara na mikoa jirani pamoja na nchi jirani ya Msumbiji.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

By Jamhuri