Tetemeko kubwa la ardhi lililotokea Januari 2010 na kuusambaratisha mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince, lilikuwa ni tukio lililoleta mabadiliko katika mikakati ya kushughulikia majanga yanayotokea maeneo ya mijini.

Mabadiliko hayo yalikuja kwa sababu mikakati ya kukabiliana na majanga maeneo ya mijini ambayo ilikuwa inatumika wakati huo ilionekana haifai kutokana na mazingira yaliyokuwepo kwenye mji huo.

Kanuni za kibinadamu za ujenzi wa kambi za wakimbizi zikaonekana hazifai kulingana na kile kilichotokea Port-au-Prince. Kimsingi, kanuni hizo zilishindwa kufanya kazi kutokana na aina ya mazingira ambayo watoa misaada walilazimika kufanya kazi ndani yake. Tofauti na maeneo ya vijijini, mijini kulikuwa na mazingira tofauti na mivutano mingi ya makundi tofauti ya watu na taasisi.

Hata hivyo, kumekuwa na mwitikio mdogo sana katika kufanya mabadiliko hayo na miaka kumi baadaye bado mikakati ya kukabiliana na majanga maeneo ya mijini bado haijaweza kukidhi mahitaji.

Kwa mujibu wa Shirika la The New Humanitarian (TNH) ambalo hujishughulisha na habari za majanga na misaada ya kibinadamu, mahitaji ya kufanya mabadiliko ya mikakati ya kukabiliana na majanga mijini yaliyoonekana wakati wa tetemeko la Haiti, bado yapo hadi leo hii.

Shirika hilo linatoa mifano kadhaa ikiwamo yale yanayotokea Syria ambako kutokana na vita zaidi ya asilimia 60 ya wakimbizi na asilimia 80 ya watu wasio na makazi ndani ya nchi hiyo wanaishi maeneo ya mijini.

Aidha, mikakati ya kushughulikia watu katika miji kama vile Kabul na Mogadishu, inakabiliwa na changamoto nyingi kutokana na mambo mbalimbali kama vile mazingira. Mathalani, ukame na mapigano ni kati ya mambo yanayotatiza utoaji wa huduma vizuri kwa watu walioathirika na vita katika maeneo hayo, huku watu wengi wakilazimika kuishi katika makazi yasiyo maalumu katikati au pembezoni mwa miji.

Lakini kwa upande mwingine, idadi ya watu imekuwa ikiongezeka sana mijini huku watu wengi kutoka maeneo ya vijijini wakikimbilia mijini kutokana na sababu za kiuchumi au majanga kama vile mafuriko, ukame, njaa na majanga mengine yanayotokana na mabadiliko ya tabia nchi.

Lakini mbinyo mijini hautokani tu na ongezeko la watu kutoka vijijini wakikimbia majanga na mapigano. Miji yenyewe, kutokana na ubovu au kutowepo kabisa miundombinu, inakabiliwa na matatizo lukuki.

Maeneo ya miji katika baadhi ya nchi kama vile Iraq, Libya, Syria na Yemen – yamegeuka kuwa maeneo ya mapigano, wakati magenge ya kihalifu yamekuwa kama ‘watawala’ katika miji mingi ya nchi za Amerika ya Kusini na Kati.

Changamoto

Mabadiliko ambayo mwaka 2010 yalionekana muhimu kutekelezwa hayajatekelezwa hadi leo kwa kiasi cha kuridhisha kwa sababu kuna changamoto kubwa sana katika maeneo ya mijini. Kuna masuala ya fedha; kuna masuala ya wenyeji na tamaduni zao; pia kuna watoaji wengi wa misaada ya kibinadamu ambao kila mmoja ana programu zake, sera zake na mipango yake – kuwaunganisha wote hawa chini ya mkakati mmoja limeonekana kuwa ni jambo gumu sana.

Ili kuyashinda hayo yote, wataalamu wanapendekeza kuwepo kwa ushirikiano katika ngazi mbalimbali. Moja ni ushirikiano kati ya mashirika yanayotoa misaada, na pili, ushirikiano na jamii husika. Hii itasaidia makundi yote kuwa katika msimamo mmoja wakati wanaposhughulikia majanga katika maeneo ya mijini.

Haya yatawezekana iwapo mambo kadhaa yatafanyika. Moja ni kukusanya takwimu na taarifa muhimu kuhusiana na nini hasa kinapaswa kufanywa katika kushughulikia majanga katika maeneo ya mijini; kujenga mfumo ambao utawezesha misadaa kuwasaidia wenyeji kujenga uwezo na kujenga mfumo wa maisha ya kujitegemea; kubadili matarajio ya watoa misaada kutoka kuamini kuwa wanachokifanya ni kazi ya muda mfupi; na kuwekeza katika mafunzo na maarifa miongoni mwa jamii zilizopatwa na majanga.

Ebola

Moja kati ya majanga yaliyotikisa mwaka 2019 ni ugonjwa wa Ebola. Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ndiyo nchi ambayo imeathirika sana na ugonjwa huu ambao hivi sasa inaaminika kuwa umedhibitiwa baada ya mgonjwa wa mwisho kuruhusiwa kutoka hospitalini wiki chache zilizopita.

Janga la Ebola mwaka jana ni janga la pili kwa ukubwa kuwahi kutokea duniani, lakini halikuwa ni janga pekee lililoisibu Kongo katika mwaka huo.

Katika Jimbo la kaskazini mashariki la Ituri, takriban watu 300,000 walilazimika kuyakimbia makazi yao kutokana na mlipuko wa magonjwa ambao haukutangazwa sana na vyombo vya habari wakati mamia kwa maelfu wengine wakipata shida kama hiyo kusini mwa Jimbo la Kivu.

Kulikuwa na mlipuko wa ugonjwa wa surua ambao uliua watu 5,000 huku watu wengine 470 wakifariki dunia kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu.

Wakati juhudi za kupambana na Ebola zilionekana kuzaa matunda kuelekea mwishoni mwa mwaka jana, lakini watoa misaada walilazimika kukatisha shughuli zao mara kwa mara kutokana na mapigano yasiyokwisha nchini humo. Hii ina maana kuwa kama kusingekuwa na mapigano, pengine Ebola ingedhibitiwa mapema zaidi na kupunguza idadi ya watu walioathirika.

Mapigano baina ya vikosi vya serikali na wanamgambo yaliibuka mara kwa mara na baadaye likaibuka tatizo jingine pale wakazi walipoanza maandamano wakidai kuwa Vikosi vya Kulinda Amani vya Umoja wa Mataifa havina maana kwao kwa sababu vimeshindwa kuwalinda dhidi ya wanajeshi, wawe ni waasi au wa serikali.

Hata hivyo, ingawa Ebola na magonjwa mengine yanaonekana kuwa yamedhibitiwa, lakini wakazi wa maeneo yaliyokumbwa na magonjwa hayo bado wataendelea kutegemea misaada kwani majanga hayo yameharibu kabisa mifumo ya kijamii. 

Kwa upande mmoja, itabidi watu wasaidiwe kurejea katika hali ya kawaida katika jamii, kuandaa mazingira ya ajira kwa watu wengi, kuwapokea wale waliokimbia maeneo yao na pia kuwasaidia waliopona Ebola dhidi ya unyanyapaa, kwani wanaonekana kama watu walioleta balaa katika jamii.

Ukiangalia ukubwa wa Kongo na ubovu wa miundombinu, hili ni jukumu kubwa sana na inahitajika mipango kabambe kuhakikisha inatekelezwa kwa ukamilifu na ufanisi, la sivyo, wananchi wa Kongo wataendelea kutaabika.

Magonjwa mengine

Kwa kawaida mapigano yanadhoofisha mifumo ya afya katika jamii. Mapigano pia yanadhoofisha huduma nyingine za kijamii kama vile upatikanaji wa maji safi na salama, hivyo kusababisha kulipuka na kusambaa kwa maradhi mbalimbali ya kuambukiza.

Kuna uwezekano mdogo sana wa mambo kubadilika mwaka huu na kama nchi zisipokuwa na uangalifu, mambo yatazidi kuwa mabaya licha ya uelewa kuongezeka.

Mwaka uliopita, mathalani, surua ililipuka na kusambaa katika nchi za Angola, Cameroon, Chad, DRC, Madagascar, Nigeria, visiwa kadhaa katika Bahari ya Pacific, Ufilipino na Ukraine. Idadi ya waliougua duniani kote ilikuwa ni mara tatu ya wale waliogua mwaka uliotangulia na katika baadhi ya maeneo kama vile Samoa, utoaji mdogo wa chanjo ulihusishwa na ubishi wa wenyeji kukubali kuchanjwa.

Hali hii inaonekana kuwa inaweza kuendelea mwaka huu na dalili zimeshaanza kuonekana. Wakati wakazi wa Samoa wakigoma kupokea chanjo, wakazi wa DRC waligomea misaada wakati wa mapambano dhidi ya Ebola, wakiamini kuwa huo si ugonjwa bali ni janga lililoanzishwa na wakubwa ili wafanye biashara zao. 

Waliamini kwa dhati kabisa kuwa jamii zao zimefanywa kama vyombo vya majaribio ya kisayansi na hivyo watoa misaada walikumbana na hasira za wenyeji mara kwa mara na kuifanya kazi yao kuwa ngumu sana. Vurugu kama hizo dhidi ya watoa misaada hazitokei Kongo peke yake.

Huko Pakistan, utoaji wa chanjo ya polio umekuwa na shida baada ya wataalamu wanaotoa chanjo hiyo kushambuliwa mara kwa mara, wakijikuta katikati ya mapigano yanayoendelea nchini humo. Hali kadhalika, watu wanaotoa misaada ya huduma za afya katika maeneo kama Gaza, Libya, Iraq, na Syria nao wamejikuta wakishindwa kufanya kazi kwa ufanisi kutokana na kushambuliwa mara kwa mara.

Kama hilo halitoshi, hivi sasa watoa misaada ya kiutu sasa wanakabiliwa na hatari nyingine; dawa ambazo zinatumika kutibu hasa majeraha yanayotokana na mapigano na magonjwa kama kifua kikuu sasa zinaonekana hazifanyi kazi sawasawa.

Mathalani, baadhi ya maeneo ya Iraq karibu theluthi moja ya wagonjwa wote wanaonyesha usugu wa dawa ambazo zinatumika kuwatibu. Lakini hofu si tu kwa dawa hizo kupoteza nguvu ya kutibu, bali pia dawa zenyewe hazipo za kutosha.

Kuna upungufu mkubwa duniani wa viua vijasumu (antibiotics) kama vile penicillin na co-trimoxazole (ambazo kwa kiasi kikubwa hutumika kutibu magonjwa nyemelezi kwa watu walioambukizwa virusi vya ukimwi). Mbaya zaidi, kuna ripoti za migongano baina ya watengenezaji na watafiti wa dawa hizi duniani.

Mtikisiko wa uchumi

Wakati teknolojia za kutabiri majanga kama vile mafuriko na njaa zikikua, lakini inakuwa vigumu kuwa na hatua za kukabiliana na majanga hayo kwa sababu kadhaa ikiwamo kuporomoka kwa uchumi. 

Utabiri unaweza kuonyesha eneo fulani litakumbwa na janga fulani muda fulani, hiyo inaweza kutoa maandalizi ya kukabiliana na janga hilo. Lakini mara nyingi kunakuwa na mwitikio mdogo na hata yale majanga ambayo yalifahamika inakuwa vigumu kukabiliana nayo kwa sababu kunakuwa na upungufu wa rasilimali za kukabiliana nayo.

Mbinyo wa kiuchumi, vikwazo na kupungua kwa ruzuku na michango kwa taasisi zinazotoa misaada ya kibinadamu ni jambo linalotatiza sana juhudi za kukabiliana na kupunguza madhara ya majanga.

Mabadiliko ya kisiasa sehemu nyingi duniani yamekuwa na athari kubwa sana kwa uamuzi kuhusu kiwango cha ruzuku ambacho kinapaswa kutengwa kwa ajili ya kukabiliana na madhara ya majanga. Hivyo, kila mara dunia imejikuta katika wakati ambapo inashindwa kukabiliana na majanga ambayo yalishajulikana kitambo kuwa yatatokea.

Kuporomoka kwa uchumi, hasa miongoni mwa nchi tajiri, nalo ni jambo linaloathiri sana kazi ya kukabiliana na madhara ya majanga. Nchi ambayo inapambana kuinua uchumi wake mara nyingi hukimbilia kuongeza kodi, jambo ambalo linayalazimisha mashirika yanayochangia shughuli za kukabiliana na majanga kupunguza au wakati mwingine kufuta kabisa ruzuku wanazozitenga kwa ajili hiyo kutokana na kubanwa katika kodi.

Mapinduzi ya kijeshi nayo huvuruga sana kazi za kukabiliana na madhara ya majanga. Chukulia mathalani Sudan. Vurugu zinatokea, shughuli za uchumi zinasimama, kiongozi anapinduliwa, vurugu zinaendelea, bei za bidhaa muhimu kama mafuta na chakula zinapanda, wananchi wanaandamana zaidi kupinga hilo, nchi inasimama kwa sababu hakuna shughuli yoyote inayoendelea huku wanasiasa wakiendelea na vikao kwa kile kinachoelezwa kuwa kutafuta suluhisho.

Lebanon ilipofikiria kuongeza kodi katika masuala ya intaneti watu waligoma, shughuli zikasimama kwa siku kadhaa na serikali ikaangushwa. Kama kulikuwa na mipango iliyokuwa imepangwa na serikali hiyo, yote ilivurugika. Serikali mpya itakayoingia madarakani haitakuwa na mipango ile ile kukabiliana na madhara ya majanga kama ilivyokuwa kwa serikali iliyopita. Kila kitu kinaanza upya!

Madhara

Mambo yanayotokea hayawezi kusababisha misaada ya kibinadamu ikasitishwa ghafla, lakini yataendelea kuathiri shughuli za misaada kwa muda mrefu na inaweza kuwa ndiyo mwanzo wa mwisho wa shughuli hizo.

Kampuni ya hesabu za kiuchumi ya Moody imewahi kusema: “Siasa zisizotabirika zinatengeneza mazingira yasiyotabirika ya uchumi na sekta ya fedha.” Moody ilitoa kauli hiyo wakati inazungumzia mambo yanayotokea Lebanon na Uturuki.

Moody inaungana na tahadhari kama hizo ambazo zilishawahi kutolewa awali. Umoja wa Mataifa umeshasema kuwa asilimia 40 ya watu wanaohitaji misaada ya kibinadamu wanaishi katika nchi ambazo zinakabiliwa na madeni makubwa.

Nchi zinazoendelea na nchi maskini zinadaiwa kiasi cha dola 55 trilioni za Marekani na kuifanya Benki ya Dunia kutamka kuwa “kiasi, kasi na wimbi la deni hivi sasa ni jambo ambalo linapaswa kuifanya dunia itafakari upya.”

Biashara duniani inayumba vibaya katika kipindi cha miaka kumi na hivi sasa iko katika hali mbaya katika kipindi hicho. Mtikisiko wa uchumi ni jambo ambalo tayari limeshatabiriwa na limeanza kujitokeza kupitia mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya corona.

Dunia inabidi sasa ianze kujiuliza ni nini kinasababisha hali ya madeni ifikie hapo ilipo? Je, ni kukopa bila mipango? Wizi na rushwa? Kushindwa kukabili majanga? Au ni sababu gani hasa?

Inabidi kutafuta majibu ya maswali hayo, kwa sababu wakati nchi zinazoendela na maskini zikijikuta katika mkwamo wa madeni, nchi tajiri nazo zinakabiliana na tatizo la aina jingine kabisa. Corona imetikisa masoko ya hisa na sekta ya uzalishaji kiasi kuwa ajira zimepukutika na bei ya mafuta inaporomoka. 

Uchumi wa nchi tajiri ukivurugika, kwenye nchi maskini hali itakuwa mbaya zaidi na suala la kukabiliana na majanga litawekwa benchi kabisa na kusahauliwa. Watakaoumia ni wengi.

By Jamhuri