Tupande miti ili kukuza uchumi wetu (2)

Urahisi wa kutumia mkaa si bei yake, bali ni kutokana upatikanaji wake (unasambazwa sehemu nyingi mijiji na wauzaji wadogo wadogo) na mtumiaji halazimiki kuweka mkaa mwingi, bali ananunua kulingana na mahitaji ya kila siku pengine kwa kutumia Sh 500 au 1,000 kwa kwa siku.

Wakati akitaka kupika kwa kutumia gesi ni lazima anunue mtungi ikiwa ni gharama kubwa. (mtungi wa kilogramu 15 ni karibu Sh 60,000).


Ni wachache wanaomudu gharama hizo kwa mara moja, pia ni lazima mtumiaji awe na jiko la kutumia gesi ambalo pia linauzwa kwa bei kubwa. Kwa hali hiyo wengi tunakimbilia kutumia mkaa hata kama si nishati safi.

Hii inatokana na ukweli kwamba wakazi wengi mijini hawana uwezo wa kununua vifaa kama mitungi ya gesi na majiko au kutumia umeme kupikia.  Kadhalika, vijijini wanatumia kuni kama nishati ya kupikia, na sehemu zenye baridi kama mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na Kaskazini wanahitaji kuni nyingi zaidi kwa ajili ya kuongeza joto katika nyumba hasa miezi ya Julai hadi Novemba.

Kutokana na hali halisi kwamba wakazi katika miji na majiji wanaendelea kuongezeka, matumizi ya nishatimiti yamekuwa yakipanda sana. Jiji la Dar es Salaam pekee matumizi ya mkaa na kuni yanakadiriwa kufikia zaidi ya tani milioni moja. Tunapozungumzia kiasi hicho ina maana kuwa miti inayokatwa kutengeneza mkaa peke yake bila ya kujumlisha kuni na nguzo au mbao, ni zaidi ya tani milioni kumi za miti ya asili inakatwa na kuangamia bila huruma. Hiki ni kiasi kikubwa cha miti kwa matumizi ya jiji la Dar es Salaam pekee.

Tungetarajia kuwa watu wengi wanaoishi katika jiji hilo wasingetumia mkaa maana ni nishati chafu ukilinganisha na hali za maisha katika majiji.

Katika harakati za kupika chakula kwa kutumia mkaa, mpishi huchafuka mikono, na mavazi na pia huvuta gesi ya ukaa (carbon monoxide), tofauti kama angekuwa anapika kwa kutumia gesiasilia, gesi zitokanazo na mafuta (Liquified Petroleum Gas-LPG) au umeme.

Vilevile, kuna changamoto ya umasikini uliokithiri vijijini unaowafanya baadhi ya wananchi wajenge tabia ya kupenda kukata miti hovyo ili kujipatia riziki yao ya kila siku kupitia biashara ya mkaa, kuni, nguzo au mbao.  Wanafahamu fika kuwa mahitaji ya bidhaa hizo ni makubwa, hivyo wanunuzi na walanguzi wapo wengi tu.

Hali hiyo inakuwa kama motisha kwa wakazi wa vijiji kuendelea kujipatia kipato kwa kukata miti. Hali hiyo ya kukata miti hovyo inachangiwa na ukweli kwamba misitu mingi katika bara haina wasimamizi hata kidogo.

Wakati wanaovuna au kukata miti ya asili wanatakiwa wafanye hivyo kwa kupata kibali (leseni au ruhusa maalum kutoka serikalini), hawahangaiki kutafuta kibali kwa sababu wanafahamu kuwa misitu haina usimamizi wowote, hivyo ni kiasi cha mhusika kuingia na kufanya anavyotaka na hatimaye kuondoka bila ya kuulizwa na mtu yeyote.

Ingawa rasilimali misitu zinasaidia watu wengi kumudu maisha yao ya kila siku, matumizi yenyewe si endelevu maana yanasababisha misitu mingi kutoweka kwa kasi sana ukilinganisha na kasi ya kupanda miti au maeneo yaliyofyekwa kuweza kurejesha uoto wa asili kwa muda mfupi bila kuleta madhara kwa mazingira.

Utafiti juu ya miti inayofaa kuoteshwa nchini

Suala la kupanda miti si geni nchini maana miaka ya 1970 Serikali ilianza juhudi za kupambana na uharibifu wa ardhi kutokana na shughuli za kibinadamu zisizo endelevu. Kwanza, kwa kuanzisha mashamba ya Serikali ya miti katika maeneo mbalimbali nchini.

Uanzishwaji wa mashamba ya miti ulikuwa ni matokeo ya utafiti uliofanywa na watawala wa kikoloni kuanzia enzi za Wajerumani. Kwa mara ya kwanza Wajerumani waliazisha shughuli za utafiti wa misitu na miti (biological research station) mwaka 1902 katika eneo la Amani, Muheza mkoani Tanga.

Hata hivyo, mwaka wa 1928 Waingereza walihamisha shughuli za utafiti wa misitu kutoka Amani kwenda Muguga nchini Kenya na kuifanya kuwa kituo cha Afrika Mashariki kwa utafiti wa kilimo na misitu (East African Agricultural and Forestry Research Organization-EAAFRO).

Mwaka 1950 Waingereza walikitengeneza upya kituo cha Lushoto ili kiweze kujishughulisha na masuala ya utafiti wa misitu na miti kwa kuangalia zaidi changamoto za ndani ya nchi kuliko kwa mtazamo wa kijumla wa Afrika Mashariki kama ilivyokuwa kwa kituo cha Muguga.

Vilevile mwaka 1951 walianzisha kituo cha kufanya utafiti wa mbao mjini Moshi (Wood Utilization Reserch Center) ili kufahamu ubora na kwa matumizi mbalimbali kulingana na hali ya hewa kwa sehemu husika (local climatic conditions).

Kituo cha Muguga nchini Kenya kwa namna moja au nyingine kiliweza kujishughulisha na masuala ya utafiti wa kilimo na misitu kwa nchi tatu zilizokuwa chini ya himaya ya Waingereza.

Hata hivyo, nchi zenyewe (Kenya, Tanganyika na Uganda) ziliazisha na kujenga vituo vya utafiti wa misitu na miti kutokana na mahitaji halisi kwa nchi husika.

Hivyo, kwa upande wa Tanganyika vituo vilianzishwa sehemu kama Longuza wilayani Muheza, Tanga; Mtibwa-Turiani wilayani Mvomero mkoani Morogoro; Meru Mkoa wa Arusha; na Matogoro karibu na Songea mkoani Ruvuma. Kadhalika, katika maeneo ya Kawetire na Kiwira-Rungwe mkoani Mbeya; Shume-Magamba, Lushoto mkoani wa Tanga; Rondo mkoani Lindi; Sao Hill mkoani Iringa na eneo la Rubare katika Mkoa wa Kagera.


Aina ya miti ilizofanyiwa utafiti ilikuwa ni pamoja na mikalatusi (Eucalyptus species); miti aina ya “misindano” (Pine species); mi-cyprus (Cyprus tree species) na misaji (Teak-Tectona grandis). Utafiti huo ulihusisha maeneo na aina mbalimbali za miti ilipokuwa inatoka (provenance & species trials).

Kwa mfano, mbegu mbalimbali za miti aina ya mikalatusi ziliingizwa nchini kutoka Australia (ambako kuna zaidi ya aina 600 ya miti ya mikalatusi) kwa ajili ya kufanyiwa majaribio kulingana na aina ya mikalatusi na sehemu ambazo mbegu za mikalatusi zilikotoka: kwa mfano, kutoka Queensland au Western Australia.

Dk. Felician Kilahama ni Mwenyekiti wa Kamati ya Misitu, Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO).

By Jamhuri