Alhamisi, Septemba 26, mwaka huu Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Seif Shariff Hamad, alizungumza na watu wanaodaiwa kuwa ni Wazanzibari wanaoishi Tanzania Bara, jijini Dar es Salaam.

Katika mazungumzo yake na watu hao, Seif Shariff Hamad alidai kuwa Wazanzibari wote hawataki rasimu ya Katiba mpya kwa sababu haina maslahi yoyote kwo.

Seif Shariff Hamad aliendelea kudai kuwa Wazanzibari wamekuwa watu wa kubururwa tu katika Muungano tangu ulipoanzishwa mwaka 1964. Pia alidai kuwa tayari Bara imepeleka Zanzibar mapandekezi ya watu waliopewa vitambulisho vya kura, ili baadaye rasimu ya Katiba mpya itakapopigiwa kura watu hao wawameze Wazanzibari kwa wingi wa kura, na kwa njia hiyo ionekane kwamba Wazanzibari wameunga mkono mambo wasiyo na maslahi nayo. Hayo ni madai mazito sana, tena yanatishia uhai wa Muungano. Ni muhimu tuyajadili. Kabla hatujazungumzia madai mengine aliyotoa Seif Shariff Hamadi, kuna maswali sita ambayo yanahitaji majibu yake kuwekwa wazi na Seif ili asiwekwe katika fungu la wachochezi hatari sana.

Kwanza, Seif anawasemea watu wa Zanzibar akiwa kama nani: Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar au Katibu Mkuu wa CUF?

Pili, kikao cha Wazanzibari waliomtuma kuja Bara likifanyika wapi? Lini?

Tatu, anajuaje kuwa Wazanzibari wote hawataki rasimu ya Katiba mpya? Je, tayari Zanzibar imepigia rasimu hiyo ya Katiba kura ya maoni?

Nne, Seif anadai kuwa Wazanzibari wamebururwa katika Muungano tangu ulipoanzishwa mwaka 1964. Je, Baraza la Mapinduzi la Zanzibar chini ya kiongozi wake, Sheikh Abeid Karume, halikukubali  kuanzishwa kwa Muungano huu? Ulikuwa uamuzi wa Nyerere peke yake?

Tano, kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012, Zanzibar ina Wazanzibari milioni moja na laki tatu. Maana yake ni kwamba ili mapandikizi ya watu waliopelekwa Zanzibar na Bara yawameze Wazanzibari katika kura ya maoni mapandikizi hayo lazima yawe na watu wasiopungua milioni moja na laki nne au zaidi. Watu hao wote wamewekwa wapi Zanzibar?

Sita, watu hao ambao Bara imewapeleka Zanzibar wamepewa vitambulisho wapi — Bara au Zanzibar? Wamepewa na nani?

Ni vyema Seif Shariff Hamad akaitisha mkutano na waandishi wa habari kujibu maswali hayo kwa lengo la kulinda heshima yake ili asionekane mchochezi na asiyeutakia mema Muungano.

Katika madai mengine, Seif Shariff Hamad amedai kuwa Wazanzibari wanataka Serikali tatu — mojawapo ikiwa Serikali ya Zanzibar yenye uwezo wa kuingia mikataba na mataifa mengine. Pia wanataka masuala ya uraia na uhamiaji yasiwe ya Muungano. Wanataka pia mipaka ya nchi ya Zanzibar ijulikane, Zanzibar iwe na mabalozi wake nje ya nchi, utamaduni wa Zanzibar utambulike, na kadhalika.

Seif Shariff Hamad amekamilisha madai yake kwa kusema kwamba Wazanzibari wataidai Serikali yao yenye mamlaka kamili kwa gharama yoyote ile hadi ipatikane. Inavyoonekana wamejipanga kweli kweli ikiwa ni pamoja na mapambano ya silaha.

Ukweli kwamba Zanzibar haihitaji Muungano tuna haja gani ya ushahidi mwingine baada ya maneno hayo ya Seif Shariff Hamad? Tazama! Zanzibar inataka masuala ya uraia na uhamiaji yasiwe ya Muungano, mipaka ya Zanzibar ijulikane, Zanzibar iwe na mabalozi wake nje ya nchi, utamaduni wa Zanzibar utambulike, na kadhalika. Hapo Muungano umebaki wapi?

Watanzania hatuna sababu tena ya kuendelea kufichana ukweli wa mambo. Ukweli wa mambo ni huu: Tanganyika imechoka na Zanzibar. Zanzibar ni walalamishi wasiochoka kulalamika. Sasa umefika wakati wa Tanganyika kuachana na Zanzibar. Kama Zanzibar imepanga kuondokana na Muungano kwa lengo la kurejesha Zanzibar utawala wa kisultani na iwe hivyo.

Sisi sote tunajua kuwa kitendo cha kurejesha usultani Zanzibar kitahusisha umwagaji mkubwa wa damu kwa sababu Waafrika halisi wa Zanzibar watakiona kuwa ni kitendo cha kusaliti Mapinduzi ya Januari 12, 1964 yaliyoleta Uhuru wa Waafrika wa Zanzibar.

Hivi kwanini iwekwe mipaka ya wazi ya kutenganisha Tanganyika na Zanzibar? Sababu uvamizi utakapofanyika wa kurejesha usultani Zanzibar, Tanganyika isivuke mipaka kuingia Zanzibar kutetea uhuru wa wananchi wa Zanzibar waliokuwa wamekandamizwa na utawala wa kisultani kwa miaka 132.

Leo Watanganyika wamefika mahali wanajiuliza wananufaika na nini katika kuungana na Zanzibar. Watanganyika huenda hawatakiwi Zanzibar. Hawana miradi yoyote kule Zanzibar ikilinganishwa na miradi waliyo nayo Wapemba Tanganyika.

Bora sasa Tanganyika ikubaliane na Zanzibar kuhusu masuala ya uraia na uhamiaji, Wazanzibari wote walioko Tanganyika warejee kwao Zanzibar kwa kuwa watakuwa wahamiaji haramu. Warejee kwao kisha waombe upya uraia wa Tanganyika ili waweze kuingia Tanganyika tena.

“Anza wewe nami namaliza, bora tusielewane vibaya,” ndivyo ilivyoimba Bendi ya Atomiki ya Tanga miaka ya 1970. Kama sherehe za miaka 50 ya Muungano mwaka 2014 zitakuwa za kuungana, na Muungano na iwe hivyo. Sikio la lufa halisikii dawa!


By Jamhuri