Uharibifu misitu: Janga linaloiangamiza Tanzania (3)

Nini kifanyike ili kuiokoa misitu ya asili isiendelee kuharibiwa na kutoweka? Yafuatayo yanafaa kuzingatiwa na kufanyiwa kazi ipasavyo:

(i)Kuhamasisha na kuelimisha umma wa Tanzania Bara, juu ya umuhimu wa kutunza misitu ya asili na kuhakikisha rasilimali hii muhimu inatumiwa kwa uangalifu mkubwa na katika misingi endelevu kwa faida ya kizazi hiki na vijavyo

(ii) Kupiga vita ubadhirifu na ufisadi uliokithiri kwa matumizi ya rasilimali za umma, ikiwamo uharibifu misitu ya asili na matumizi ya wanyamapori yasiyo endelevu au yasiyoleta tija kwa umma wa Tanzania. Suala la msingi hapa ni kuhakikisha kuwa maliasili tuliyonayo inawanufaisha wananchi wengi vijijini na ambao wamegubikwa na umasikini (persistent and widespread poverty) na kushindwa kumudu maisha ipasavyo.

 

(iii) Viongozi wote na kwa ngazi zote wawajibike na wachukue hatua za makusudi kabisa kwa minajili ya kupunguza uharibifu wa misitu ya asili katika maeneo wanayoyasimamia. Hii inamaanisha kuwa kama misitu ya asili inapatikana katika eneo la kijiji, Mwenyekiti na Halmashauri yake wawajibike na wahakikishe misitu inatunzwa na kutumiwa kwa njia endelevu.

 

Kijiji kiwe na mpango wa matumizi bora ya ardhi na eneo la msitu lihifadhiwe na kuandaliwa Mpango wa Usimamizi na kuutekeleza ipasavyo. Viongonzi wengine kama Mkuu wa Wilaya (DC), Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri (DED), Maafisa Watendaji Tarafa, Kata naVijiji wahakikishe na kuvisaidia vijiji kusimamia misitu iliyomo katika maeneo ya vijiji wanavyovisimamia.

 

(iv) Wanasiasa kwa ngazi zote ikiwa ni pamoja na madiwani, wabunge, Baraza la Mawaziri pamoja na viongozi wengine wa ngazi za juu kama wakuu wa mikoa, wahimize utunzaji wa misitu ya asili kwa faida ya Watanzania wote. Haipendezi na haina tija hata kidogo, viongozi wanapokuwa na lugha za kugongana katika suala zima la kutunza na kusimamia rasilimali zetu za alisi.

 

Kwa mfano, tunaposema mipaka ya misitu iliyohifadhiwa kisheria iheshimiwe na Watanzania wasivunje Sheria ya Misitu Namba 14 ya 2002 (au Sura Na. 323 Re 2002) iwe ni hivyo. Kusitokee kiongozi mwingine wa ngazi za juu serikalini au mwanasiasa – awe ni diwani au mbunge au kiongozi mwingine wa chama cha siasa – kwenda kinyume cha suala la usimamizi wa Sheria ya Misitu kwa kuhamasisha wananchi kuvamia misitu iliyohifadhiwa kisheria kwa shughuli za kilimo, kufuga/kuchungia mifugo au kujenga nyumba bila kufuata Sheria na Kanuni zake.

 

Nichukue fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza sana baadhi ya viongozi wetu, hususan wakuu wa mikoa ya Iringa, Kilimanjaro, Kigoma, Pwani, Tabora, Tanga, na wilaya za Mpwapwa, Namtumbo, Gairo, Handeni, Mbeya, Mbozi na Urambo kwa ujasiri wao wa kupambana na wanaoharibu misitu ya asili katika maeneo wanayoyasimamia.

 

Inawezekana wapo wakuu wa mikoa au wilaya wanaofanya kazi nzuri ya kupambana

na uharibifu wa misitu ya asili ambao sikuwataja hapa kwa kutopata taarifa zao, lakini wote kwa pamoja wazidishe kasi ya mapambano kwa faida ya Watanzania wote.

 

Vilevile niwashukuru baadhi ya wananchi wenye mapenzi mema kwa nchi yetu, ambao mara kwa mara wamekuwa wakishirikiana na uongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kutoa taarifa ambazo, kwa namna moja au nyingine, zimesaidia sana wizara kuweza kuchukua hatua za kuiokoa misitu ya asili isiendelee kuvamiwa na kuharibiwa na watu wachache kwa tamaa zao binafsi

(v) Kipekee niwashukuru wanahabari wote wa vyombo mbalimbali vya habari ikiwa ni pamoja na magazeti, runinga, redio na kwa kutumia mitandao mbalimbali, kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kueneza elimu ya mazingira kupitia vyombo vyeo.

 

Naamini kwa kupitia nguvu ya uandishi waliyonayo (power of the pen – magazetini) na kupitia nguvu la ulimi (power of the tongue – kwa upande wa redio na runinga), kwa pamoja tunaweza kubadilisha mtazamo na mawazo hasi walionayo baadhi ya wadau wa misitu ya asili, kuwa chanya (change negative perceptions to positive and conservation ariented attitudes).

 

Niwaombe sana mlipe kipaumbele suala la kuhifadhi misitu ya asili kwa faida ya Taifa letu na kwa ajili ya maendeleo ya watu wake, na kuhifadhi mazingira kwa ajili ya maendeleo endelevu.

(vi) Mwisho, nimalizie kwa kusema kuwa “PENYE NIA PANA NJIA” pia kwa kawaida huwa tunasema kuwa “UMOJA NI NGUVU NA UTENGANO NI UDHAIFU”. Kwa dhamira ya kweli ya kuiokoa misitu ya asili hasa iliyohifadhiwa kisheria, ni vizuri wanahabari wote pamoja tukawa kitu kimoja na kuielimisha jamii juu ya madhara yatokanayo na matumizi yasiyo endelevu.

 

Elimu ya mazingira ni muhimu sana, hivyo nawasihi sana tusaidiane katika kuiokoa Tanzania isiwe jangwa kwa miaka michache ijayo. Asante sana kwa ushirikiano wako mzuri na MWENYEZI MUNGU AKUBARIKI – “MISITU NI UHAI TUITUNZE ILI ITUTUNZE. PIA MISITU NI MALI ITUMIKE KWA UANGALIFU MKUBWA.”

 

By Jamhuri