Mashabiki na wapenzi wa soka nchini Hispania wanatajwa kuwa sababu kuu inayomfanya Kocha wa Timu ya Real Madrid, Jose Mourinho, kuikimbia timu hiyo kutokana na kukosa uhusiano mzuri na wadau hao.

Kocha huyo alijiunga na timu hiyo akitokea Klabu ya Chelsea. Aliihama klabu hiyo Septemba 2007, baada ya kutofautiana na mmiliki wa klabu hiyo, Roman Abramovich.

 

Kocha huyo mwenye tambo nyingi amesema huenda asiwe kocha wa klabu hiyo msimu ujao. Anaonesha kuwa na mapenzi makubwa na timu yake zamani, Chelsea (The Blues).

 

Mourinho amekuwa akikaririwa na vyombo vya habari Hispania na kwingineko akidai kuwa wapenzi na mashabiki wa soka nchini humo hawana mapenzi naye hali inayompa wakati mgumu katika utendaji wake.

 

Amesema anafahamu kuwa anapendwa na mashabiki na vilabu vingi nchini Uingereza, hivyo anafikiria kurudi kufundisha katika klabu za nchini humo.

 

“Nimesaini mkataba na Real Madrid mpaka mwaka 2016, lakini kwa timu kama Real Madrid ukipoteza mechi hata mbili hawatosita kuuvunja mkataba, ifikapo mwaka 2016 binti yangu atakuwa anaanza chuo na nataka nitafute mji mzuri ambapo mwanangu atasoma.

 

“Uingereza watu hawakufuatilii maisha yako kama Hispania na Italia, nahitaji kuilinda familia yangu .” amesema Mourinho. Hata hivyo, amesema bado hajafanya uamuzi ni wapi anaelekea baada ya kufikiria kuachana na klabu yake ya sasa.

 

Amesema, “Haina maana kuongelea hilo kwa sasa kama naenda ama la, kama naenda sitahitaji kutoa maelezo.” Ameongeza kuwa yeye ni kocha mtaalamu na bado anaiheshimu klabu yake ya sasa lakini akimaliza ligi atazungumza wapi anakwenda.

 

Hata hivyo, Mourinho ameliambia Gazeti la  Daily Star la nchini Uingereza kuwa ameamua kurudi kuwafundisha vijana wa Darajani, na tayari  ameandaa orodha ya wachezaji ambao watairudisha The Blues kwenye kilele cha mafanikio katika Ligi Kuu ya Uingereza, huku washambuliaji kama Hulk na Radamel Falcao wakiwa miongoni mwa orodha hiyo.

 

Mourinho alizaliwa Januari 26, 1963 mjini Setúbal, Ureno. Ni miongoni mwa makocha bora Ulaya na duniani. Amapata kuwa kocha wa timu za Benifica, UD Leiria, FC Porto, Chelsea FC, Inter Milan na Real Madrid.

Please follow and like us:
Pin Share