MISITU & MAZINGIRA

Misitu ya Asili na Maendeleo ya  Jamii Tanzania (5)

Sehemu ya nne, Dk. Felician Kilahama alieleza namna wezi wa rasilimali za umma wanavyokwenda vijijini na kujitwalia maeneo ya misitu kwa mwavuli wa uwekezaji, lakini baadaye huishia kukata miti na kutoweka. Sehemu hii ya tano anaeleza namna vijiji vinavyonyonywa. Endelea

Kampuni huweza kufanya biashara ya gesiukaa (carbon trading) kadri miti inavyozidi kukua na kuviacha vijiji vikiambulia sehemu ndogo tu ya mapato husika. Vijiji na pengine watu binafsi katika sehemu mbalimbali nchini wanatoa kirahisi ardhi yao kwa wawekezaji kutokana na sababu kubwa mbili:

(i)  Kwanza, kutokuwa na uelewa na upeo mzuri wa kuiona ardhi na rasilimali misitu iliyo juu yake kama ni nguzo muhimu na hatimaye kuweza kutumia rasilimali hizo za asili kujiletea maendeleo endelevu. Kwa bahati mbaya ardhi na misitu ya asili vinaonekana kuwa ni vitu vipo-vipo tu na watu wako tayari kutumia wapendavyo. Ukosefu wa elimu ya kutosha unawafanya Watanzania vijijini kutothamini sana ardhi na misitu ya asili wakati ni rasilimali muhimu kwa maendeleo yao iwapo wataitumia kwa umakini sana. Vilevile, wataalamu hatujaweza kufanya kazi yetu ipasavyo ikiwa ni pamoja na kuwaelimisha juu ya umuhimu wa kuwapo rasilimali hizo na faida zake katika maisha yetu ya kila siku. Isitoshe, kuweza kuchukua hatua sahihi kuthamini na kutumia ardhi na misitu kwa faida yao;

(ii) Wawekezaji kutoka nje wakijua kuwa rasilimali zilizo muhimu kwa maendeleo ya vijiji ni pamoja na ardhi na misitu ya asili; na kwa kutambua kuwa wengi vijijini ni masikini na wenye uelewa mdogo; wanatumia mwanya huo kupata faida ya haraka kwa kutumia rasilimali zilizo vijijini badala ya kuwasaidia wanavijiji na jamii kwa kuwajengea uwezo imara na hivyo kuwawezesha kutumia rasilimali hizo kuleta maendeleo endelevu vijijini. Kama wangelifanya hivyo wawekezaji vijijini wangekuwa wamechangia kwa kiasi fulani kupunguza changamoto zilizopo na kiwango cha umasikini vijijini.

Matarajio Kwa Vijiji/Jamii Kutokana na Misitu ya Asili

Kufanikiwa kwa Mpango wa Usimamizi Shirikishi wa Misitu unategemea zaidi juhudi, maarifa na dhamira ya jamii husika katika kutaka kujiletea maendeleo. Wanavijiji hasa katika sehemu zenye misitu ya asili, ni muhimu wakaelimishwa ipasavyo ili watambue wajibu wao katika kuthamini, kutunza na kuhakikisha rasilimali misitu katika vijiji vyao inatumika kwa faida yao na si kinyume cha hilo.

 

Bila ya kuwa na elimu ya kutosha na kila kijiji kikawa na mpango mzuri wa matumizi ya ardhi na rasilimali misitu ndani ya eneo la kijiji chao; pia kuwa na uongozi bora na (si bora uongozi), kutaendelea kuwapo ubabaishaji usiowaletea maendeleo halisi. Watabaki kuwa masikini siku zote.

 

Matarajio ni kuwa vijiji vina uongozi imara na wenye dhamira ya thabiti ya kuwatoa wanakijiji wenzao hapo walipo na kuwasogeza mbele kwa kutumia rasilimali na fursa zilizopo katika kijiji chao. Usiwe ni uongozi wa kubweteka tu na kuridhika na hali walionayo kwa kuruhusu rasilimali ardhi na misitu zikiwanufaisha watu wachache; na kibaya zaidi kwa wale wasioishi kijijini hapo. Naamini kuwa chini ya mpango wa Usimamizi Shirikishi wa Misitu Vijijini na kuwajengea uwezo, wanakijiji wataweza kusimamia vizuri na kutumia rasilimali walizonazo ipasavyo na kuhakikisha vijiji na wanajamii wanapata manufaa yafuatayo:

i.  Watapanga ni jinsi gani ardhi ya kijiji inapaswa kutunzwa na kutumiwa katika misingi ambayo ni endelevu kwa manufaa ya kizazi hiki na vizazi vitakavyofuata;

ii. Wataweza kuongeza kipato kutokana na ushuru wa magogo, mbao, mkaa, nguzo na mazao mengine yatokanayo na kuwapo msitu wa asili; pia makusanyo mengine yatokanayo na tozo za mazao ya misitu kama asali kutokana na ufugaji nyuki au kutengeneza bidhaa kama vikapu au mikeka kwa kupata malighafi kutoka msituni;

iii. Kutakuwapo uhakika wa matumizi endelevu wa mazao ya misitu bila kuathiri uwezo wa msitu kujiendeleza kiikolojia. Pengine msitu unaweza kuwa ni sehemu ya makazi kwa viumbe wengine kama ndege na wanyama wa aina mbalimbali kuweza kuishi na hivyo kuwa eneo zuri la kuwavutia watalii na hatimaye kijiji kupata mapato zaidi kutokana na shughuli za utalii.

Kwa hali hiyo na kwa dhamira thabiti ya kuwaletea maendeleo halisi Watanzania wenzetu wanaoishi vijijini kwa kutumia rasilimali ardhi na misitu ipasavyo; tutakuwa tumetoa mchango mkubwa katika mkakati wa taifa letu wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini Tanzania (MKUKUTA). Mafanikio mengine yatayopatikana ni pamoja na:

i. Kuongezeka kwa misitu iliyotangazwa kuwa misitu ya hifadhi na kumilikiwa na vijiji au jamii. Mpaka sasa misitu 409 imeshatangazwa kuwa misitu ya vijiji. Mwelekeo uwe wa lengo la kufikisha vijiji kama 4,000 viwe vimetangaza misitu mingi zaidi na yenye ukubwa wa zaidi ya hekta milioni 10 kutoka hekta milioni 2.3 za sasa ifikapo 2020;

ii. Misitu ambayo haijatangazwa iwekewe mkakati mzuri wa kuitumia bila ya kuleta madhara makubwa kwa misitu husika na mazingira kwa jumla. Serikali Kuu kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii isimamie na kudhibiti uharibifu wowote kwa faida ya jamii na taifa letu;

iii. Maafisa Misitu na Nyuki katika halmashauri za wilaya, maafisa watendaji vijijini na ngazi ya kata wajengewe uwezo wa kusimamia misitu hasa kuweza kuchukua hatua za haraka  pale uharibifu wa misitu utakapoanza kujitokeza, ili wasiendelee kuwa watazamaji tu wakati hali inazidi kuwa mbaya;

iv. Miongozo mbalimbali ya kusaidia watendaji vijijini ikiwamo serikali za vijiji kuandaa sheria ndogo iandaliwe na wahusika waelimishwe namna ya kuitekeleza;

v. Juhudi za makusudi  zifanywe na Serikali kusaidia na kuwezesha jamii au watu binafsi kuanzisha miradi mbalimbli ya kiuchumi, ikiwa ni pamoja na ufugaji wa nyuki au samaki na kuanzisha vitalu vya miche ya miti ili wapate miche mingi na kuipanda katika maeneo yao kwa matumizi ya baadaye.

 

Itaendelea

Mwandishi wa makala haya, Dk. Felician Kilahama ni Mwenyekiti wa Kamati ya Misitu ya Dunia, yaani Committee on Forestry-COFO iliyo chini ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kilimo na Chakula (FAO). Ni Mkurugenzi Mstaafu wa Idara ya Misitu na Nyuki katika Wizara ya Maliasili na Utalii. Alistaafu Desemba 2012. Anapatikana kwa simu na. HYPERLINK “tel:0756%20007%20400”0756 007 400.