MISITU & MAZINGIRA

Misitu inavyokinufaisha Kijiji cha Nanjilinji ‘A’ (2)

Sehemu ya kwanza, Dk. Felician Kilahama, akiwa Mwenyekiti wa Bodi ya MCDI, anaeleza ziara yake katika Kijiji cha Nanjilinji ‘A’, akiwa na wajumbe wa Bodi. Pia anaeleza kuwa wafadhili kutoka Shirika la Kimataifa la Kuhifadhi Viumbehai na Mimea Ofisi za Denmark na Tanzania, walikuwapo.

Hivyo katika msafara huo alikuwapo Maj Manczak ambaye ni Mshauri Mwandamizi kwa masuala ya Afrika yahusuyo nishati na bidhaa nyingine za misitu (Senior Advisor, Energy, Forest & Timber for Africa) kutoka WWF Denmark.

 

VileVile maofisa kutoka WWF-Tanzania (Isaac Malugu, Forest Programme Officer; Gerald Kamwenda, Conservation Manager na Filipina Shao, Forest Landscape Coordinator). Kwa kiasi kikubwa misaada ambayo imetolewa na wahisani imekuwa ikitumiwa na MCDI kuwajengea wananchi uwezo wa kusimamia na kutumia rasilimali misitu waliyonayo ndani ya mipaka ya vijiji vyao katika misingi ambayo ni endelevu na kwa faida yao.

 

Kijiji cha Nanjilinji ‘A’ kipo karibu kilometa 300 kutoka Kilwa Masoko na ni mwendo wa karibu saa tatu kuweza kukifikia. Mei 23, 2013 msafara wa kwenda huko kijijini uliondoka Kilwa Masoko saa 11 alfajiri na kuwasili kijijini Nanjilinji’ ‘A’ saa moja asubuhi. Baada ya kufika hapo tulifanya mapumziko mafupi na kubahatika kupata kifungua kimya kutoka kwa wajasiriamali wanaofanya biashara ndogo ya migahawa hapo kijijini. Hata hivyo, ujio wetu siku hiyo ulikuwa neema kwao maana waliweza kufanya biashara nzuri ukijumuisha na chakula cha mchana.

 

Baada ya kupata kifungua kinywa msafara ukiwa na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kutunza na Kusimamia shughuli zote za msituni yakiwamo masuala ya uvunaji miti iliyokomaa, tulikwenda kwenye eneo la msitu wa kijiji unaojulikama kama Mbumbula. Msitu huo una ukubwa wa hekta 61,273.7 ikiwa ni karibu asilimia 35 ya eneo zima la kijiji lenye hekta 175,732.8.

 

Msitu huo uko umbali wa kilometa zaidi ya 60 kutoka Nanjilinji  ‘A’ tulipopata kifungua kinywa. Tuliwasili eneo la msitu hasa uvunaji wa miti unakofanyika majira ya saa tatu asubuhi. Tukiwa katika eneo hilo tuliweza kupata maelezo mazuri kuhusu shughuli zinavyofanyika kutoka kwa Katibu wa Kamati ya wanakijiji 16, inayosimamia masuala yote ya uvunaji na utunzaji msitu, Hamisi Mkweo.

 

Katika maelezo yake alisema kuwa kabla ya kufanya juhudi za kuuhifadhi msitu huo, mwaka 2011 wataalamu kutoka MCDI walitembelea Nanjilinji ‘A’ na kukutana na uongozi wa kijiji na kueleza umuhimu wa kuhifadhi eneo la msitu wa asili kwa faida ya kijiji.

 

Baada ya MCDI kupata ridhaa ya uongozi wa kijiji kilichofuata ni kuwahamasisha wanakijiji na kuwaelimisha juu ya kuhifadhi na kutunza msitu wa asili uliopo katika eneo la kijiji. Katika kufanikisha azma hiyo, kijiji kilitakiwa kutayarisha mpango mzuri wa matumizi bora ya ardhi (village land use plan) ili msitu utakaotengwa kwa uhifadhi uwe ni sehemu ya mpango huo.

 

Hivyo, baada ya wanakijiji kupatiwa elimu ya uhifadhi na matumizi bora ya ardhi, waliridhia eneo lenye msitu wa asili (Mbumbula) lihifahiwe na msitu huo utumike kwa faida ya wanakijiji wote. Kijiji kilichagua Kamati ya kusimamia shughuli za msitu huo ya watu 16 – wanaume tisa na wanawake saba –  ikiongozwa na Shaweji Hauu (Mwenyekiti) na Hamisi Mkweo akiwa Katibu. Kamati inawajibika kwa Serikali ya Kijiji chini ya uongozi wa Jafari Mohammed Nyambate (Mwenyekiti wa Kijiji) akisaidiwa na Ofisa Mtendaji, Issa Namalungo.

 

Baada ya kuwasili katika eneo la msitu uliohifadhiwa na unatumika kwa faida ya wakazi wote wa Nanjilinji ‘A’ tulipata maelezo kutoka kwa walinzi msitu (Forest Guards) ambao ni wajumbe wa Kamati ya kusimamia msitu. Ilielezwa kuwa kwa mara ya kwanza MCDI ilitembelea kijiji chao Mei 15, 2011 kwa lengo la kuwahamasisha wakazi wa Nanjilinji ‘A’ ili wachukue hatua madhubuti na kuhifadhi sehemu ya msitu ikiwa ni njia mojawapo ya kujiletea maendeleo endelevu.

 

Baada ya kukutana na wananchi na kuwaelimisha ipasavyo, mkutano wa kijiji uliofanyika baada ya ziara ya MCDI ulikubali wazo la kutenga sehemu ya msitu kwa madhumuni ya kuuhifadhi kwa matumizi endelevu ili wanakijiji waweze kunufaika na kuwapo rasilimali msitu katika eneo lao. Makubaliano ya wanakijiji yalikuwa ni pamoja na kuandaa mpango mzima wa matumizi bora ya ardhi ya kijiji ili msitu uwe ni sehemu ya mpango huo.

 

Baada ya makubaliano hayo na eneo lenye msitu wa asili la ukubwa wa hekta 61,273 kutengwa kwa madhumuni ya kulitumia kuleta maendeleo kijijini, Kamati ya kusimamia eneo hilo kama sehemu ya mpango wa matumizi bora ya ardhi ya kijiji, kwa kushirikiana na wataalamu wa MCDI, iliandaa mpango wa kusimamia msitu huo (forest management plan).

 

Baada ya kuupitia na kuujadili, hatimaye mpango wa matumizi bora ya ardhi ya kijiji ulipitishwa na Serikali ya Kijiji ili uweze kutumika. Kijiji kiliweza kutunga na kuweka sheria ndogo kwa lengo la kusaidia usimamizi wa msitu na kuhakikisha kuwa rasilimali zilizomo zinanufaisha jamii nzima katika kijiji.

 

Vilevile wanakijiji waliweza kufahamu ni aina gani za miti iliyokomaa na inafaa kuvunwa kwa ajili ya kuuzwa ili kukipatia mapato kijiji.

 

Moja ya sheria ndogo zilizopitishwa ilihusu bei ya kuuza mazao yatakayovumwa kutoka katika msitu wa kijiji. Iliazimiwa kuwa viwango vya bei au tozo kwa mazao mbalimbali visiwe chini ya viwango ambavyo vimeainishwa na Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii na kuchapishwa katika Matangazo ya Serikali (Government Notice).

 

Itaendelea

 

Dk. Felician B. Kilahama, Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki Mstaafu na Mwenyekiti wa Kamati ya Misitu Duniani-chini ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo-FAO, Rome, Italy.