Tukumbuke serikali ni chombo muhimu sana katika maisha ya jamii. Na ni chombo cha hatari
kwa watu wale wale inayowatumikia. Tunapozungumzia juu ya maisha na maendeleo ya watu
katika jamii, ni dhahiri shahiri tutazungumzia siasa na muundo wa serikali inayotawala katika
jamii hiyo.
Sikusudii kueleza chimbuko au asili ya serikali kupitia mifumo ya maendeleo ya jamii ya
utumwa, ukabaila, ubepari na ujamaa. Naitazama serikali katika muundo wake, kudumisha
maslahi yake na kutunza amani ya nchi.
Katika hoja hii ni vyema nikakumbusha mambo matatu makubwa muhimu. Mosi, serikali ni kitu
kinachotokana na jamii yenyewe siyo nje ya hapo. Pili, husimamia maslahi ya watu wenyewe.
Tatu, serikali popote pale ni chombo cha amri na mabavu, kwa sababu madhumuni ya kuwapo
kwake ni kutawala.
Kimsingi, tangu zamani hadi sasa serikali ni chombo maalumu kinachosimamia maslahi ya watu
na kutunza amani yao. Kwa misingi hiyo, serikali lazima itunge sheria, na pawepo vyombo vya
nguvu kama sheria, mahakama na majeshi ya kuhakikisha kuwa sheria hizo zinafuatwa, na
wale wanaozivunja wanakiona cha mtema kuni.
Ndiyo sababu katika nchi nyingi duniani zinaweka KATIBA ambayo ina kazi tatu; Mosi, katiba
huweka mipaka ya madaraka ya serikali, yaani ni kiasi gani serikali ina uwezo juu ya maisha na
uhuru wa wananchi.
Pili, katiba huweka mipaka ya madaraka ya vyombo mbali mbali vya serikali kama bunge,
mahakama, baraza la mawaziri na kadhalika. Na tatu, katiba huelekeza na kuongoza
mwenendo wa serikali kwa jumla, kama vile chaguzi za viongozi na kadhalika.
Duniani kumekuwapo miundo mbali mbali ya serikali. Kuna serikali za kifalme ambapo msingi ni
utawala wa mtu mmoja na hurithishana vizazi vya ukoo huo huo wa kifalme. Kuna muundo wa
serikali ya kikoloni, taifa moja huitawala nchi nyingine kama mali yake.
Aidha, kuna mtindo wa serikali ya kidikteta ambayo mtu mmoja au watu wachache hujichukulia
madaraka ya kutawala nchi kwa mabavu kama wanavyopenda. Vile vile, kuna muundo wa
serikali wa kidemokrasia ambapo kimsingi viongozi wa serikali huchaguliwa na watu (umma)
kwa muda maalumu.
Katika muda huo maalumu wa utawala wa serikali, watu huwa na sauti juu ya serikali yao
kupitia bunge walilolichagua, na watu wanaendelea kuwa na uhuru wa kuabudu, uhuru wa
kutoa maoni, na uhuru wa kufanya mikutano.
Ukiangalia miundo niliyoeleza kuna tofauti moja kubwa ya miundo ya serikali: za kifalme,
kikoloni na kidikteta zinasimamia maslahi ya watu wachache. Ukweli ni serikali za kidhalimu na
kinyonyaji. Na serikali za kidemokrasia zinasimamia maslahi ya walio wengi bila ubaguzi wa
aina yoyote.
Serikali za muundo wa kidemokrasia zinakubalika na kupewa nafasi pana ya kuongoza na
kutawala na wananchi, kutokana na kuzingatia na kufuata sheria, utawala bora na haki za
binadamu. Lakini mara kadhaa serikali hizi zinarubuniwa na serikali dhalimu na watu binafsi
wenye hiana. Hapa ndipo penye vita ya uchumi.
Hekima inatufanya wananchi tutambue, tuthamini na tulinde utu wetu, uhuru na ukombozi wetu.
Serikali yetu chini ya Sheria na Utawala Bora, na Haki za Binadamu ituongoze na itulinde katika
vita na mafisadi, ili tuweze endelea kuishi salama, tulivu na amani.
Ni busara tubaki njia kuu ya demokrasia ya kweli kuliko kutamani njia mchepuko iliyopambwa
na unafiki, usaliti na uasi wa watu wachache. Tukumbuke, “Tusikubali kubadili bura yetu na
rehani.”

1528 Total Views 3 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!