Miundombinu (Infrastructures) duni inachangia kukuza umaskini wetu. Watu wanazidi kuwa maskini kwa vile miundombinu iliyopo haileti unafuu wa kupunguza gharama za usafiri kwa abiria na mizigo.  Kwa muda wa miaka 52 sasa tangu tumepata uhuru tumeshindwa kugundua kwamba kuna barabara moja muhimu sana ambayo ingejengwa hapa Tanzania ingesaidia kupunguza umaskini wetu kwa kiasi kikubwa. Kitendo cha kutokuwepo kwa barabara hiyo kimechelewesha maendeleo ya nchi hii kwa kiasi kikubwa.

Kuna haja ya barabara hii ya jibu sahihi (Solution Road) kwa maendeleo ya nchi hii kujengwa na Serikali yoyote itakayoingia madarakani katika kipindi kijacho cha 2015 – 2020 kuharakisha maendeleo na kuwapunguzia wananchi gharama na muda mrefu kusafiri. Barabara hii ni ile ya MDUARA itakayouzunguka mkoa wa Dodoma, yaani tukiweka ncha ya Kompasi yatu katikati ya mji wa Dodoma na kuzungusha Penseli duara kwenye pande zote za mkoa huo, tutapata barabara hiyo itakayorahisisha usafiri kwa kila mkoa wa Tanzania kama ilivyooneshwa kwenye ramani.

Kwa mfano, ukitokea Singida kwenda Morogoro/Dar es Salaam siyo lazima upitie mjini Dodoma, bali unaingia kwenye barabara ya mduara na kutokea Kilosa hadi Morogoro, na baadaye Dar es Salaam. Ukitokea Mbeya kwenda Arusha huna haja ya kupita Chalinze ndipo urudi kwenda Arusha, bali unaingia kwenye barabara ya mduara kupitia Manyoni – Kiteto hadi Arusha. Ukitoka Mtwara na Lindi huna haja ya kuja Dar es Salaam ndipo uende Mwanza au Bukoba, bali unaitafuta barabara ya mduara, unaifuata hadi utakapoikuta njia ya kwenda Mwanza.

Ukitokea Mwanza unataka kwenda Mbeya, Ruvuma au Mtwara na Lindi huna haja ya kwenda mpaka Morogoro ndipo uamue kwamba unapita Dar es Salaam au Songea, bali unaingia moja kwa moja kwenye barabara ya mduara na kufupisha safari yako.

Kitakachotakiwa ni kuhakikisha kwamba mikoa yote itakayoguswa na barabara hii ya mduara inaziunganisha barabara zote za mikoa na wilaya kurahisisha maunganisho (connections) na mafupisho (short cuts) ya usafiri. Barabara hii ya mduara itasaidia kupunguza umaskini wetu.

 

Email:  norjella@yahoo.com Mobile: +255 782 000 131

 

1040 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!