Wiki iliyopita Gazeti la JAMHURI liliandika habari kuhusu binti wa shule anayedaiwa kutiwa mimba na mjomba wake. Hapa chini ni mwendelezo wa mahojiano ya wahusika wa tukio hilo. Endelea…

Saimoni anasema kisa hicho kimetengenezwa na mama yake mzazi ili kukwamisha suala la mirathi, anasema familia yake wameamua ‘kumbambikia’ tuhuma hiyo kama njia ya kumficha mtuhumiwa halisi aliyetajwa kwa mara ya kwanza kuhusika na ujauzito huo.

Anasema Mei mwaka jana walimu wa shule aliyokuwa anasoma binti aliyebebeshwa ujauzito walifanya uchunguzi wa mimba kwa wanafunzi na kumubaini binti huyo kuwa na ujauzito wa miezi mitano.

Walimu hao kwa kushirikiana na bibi yake walimfikisha Kituo cha Polisi Kimara Matangini na kupewa Fomu ya Polisi Namba Tatu (PF3) ya kwenda Zahanati ya Kimara kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Kutokana na hali hiyo, polisi wa Kimara Matangini walitoa kibali cha kumkamata mtuhumiwa huyo, kwa mujibu wa kitabu cha kumbukumbu za matukio ya kipolisi, kibali hicho ni namba Kim/RB/2503/2018.

Saimoni anasema baada ya mtuhumiwa huyo kukamatwa na kufikishwa Kituo cha Polisi Mbezi Louis kwa tuhuma za kumtia mimba mwanafunzi ambaye pia ana umri chini ya miaka 18, aliachiwa bila sababu za msingi kuelezwa, wala kutoa taarifa kwa walimu na walezi wa mtoto huyo.

Saimoni anasema baada ya kuanza kulifuatilia suala hilo Agosti, mwaka jana akianzia ngazi ya shule alipokuwa anasoma binti huyo hadi kituo cha polisi, mtuhumiwa huyo alikamatwa kwa mara ya pili kwa ripoti ya polisi (RB) KMR/RB/7100/2018 na kupelekwa Kituo cha Polisi Gogoni kilichopo Kibamba, Ubungo ambako pia aliachiwa tena kwa dhamana.

Mjomba mtu, ambaye ndiye mtuhumiwa namba moja sasa, anasema mtuhumiwa aliyeachiwa ilitokana na binti pamoja na wanafamilia kutoa ushahidi mbele ya polisi kuwa wahusika wa ujauzito huo wako watatu, huku wakisisitiza kuwa mhusika mkuu ni Saimoni Elias ambaye ni mjomba wake.

Kutokana na ushahidi huo, polisi walilazimika kufanya mahojiano na Saimoni kwa ajili ya kupata ukweli, lakini wakasema suala hilo liachwe hadi mtoto atakapozaliwa ili iwe rahisi kubaini sura ya mtoto imefanana na nani kati ya waliotajwa kuhusika pamoja na kuchukua vipimo vya vinasaba.

“Mimi kama mjomba mtu suala hili linaniuma sana, hayo yote yanayosemwa ni mipango ya mama, mtoto ameshazaliwa sasa niko tayari yule mtoto apimwe vinasaba ili ijulikane mtoto ni wa nani?” anasema Saimoni.

Ameliambia Gazeti la JAMHURI kuwa kinachomsikitisha zaidi ni polisi kutolichukulia suala hilo kwa uzito unaostahili, badala yake wanalihusisha na mgogoro wa urithi wa nyumba uliopo katika familia hiyo.

Saimoni anasema mbinu zinazotumiwa na mama yake kupitia kwa mjukuu wake (binti) huyo ni mbaya, kwani zinamnyima haki binti huyo aliyetiwa mimba. Anasema lengo la kufanya hivyo ni kutaka kumtumikisha binti ili kujipatia kipato kutoka kwa mtuhumia wa kwanza, kwani ameahidi kutoa fedha za matumizi na malezi kwa mtoto aliyezaliwa.

Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kwamba anayetuhumiwa (jina limehifadhiwa), awali alikuwa mpangaji wa bibi huyo na alikuwa  mwalimu wa masomo ya jioni (tuition) wa binti huyo katika kituo cha Kimara – Dawasco.

Gazeti la JAMHURI limefika kwenye kituo hicho na kuambiwa na majirani walio karibu na kituo hicho kuwa hakuna mwalimu mwenye jina hilo, na kuongeza kuwa watu wenye jina hilo ni wengi.

Bibi Anna John, ambaye ni mama yake Saimoni Elias, ametafutwa na Gazeti la JAMHURI ili kueleza juu ya sakata hilo, bibi huyo amekataa kuzungumzia zaidi suala hilo huku akisema hataki kusikia jina la Saimon Elias likitajwa katika maisha yake yote.

“Tumbo langu halijawahi kuzaa mtoto mwenye jina kama hilo, tena sitaki kukumbushwa huo mkosi muda huu, mwambieni aliyewatuma kuja kwangu kuniuliza habari hizo ana mpango wa kuniua.

“Nasikia hadi tumbo linatetemeka, yaani nasikia moyo unaniuma sana, huyo kijana nilishampa laana kwa mambo aliyonifanyia….naomba uondoke tu usiendelee kunichokonoa,” anasema Anna John huku akibubujikwa machozi kwa hasira.

Godson Munisi, Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Kimara Stop Over, anasema familia hiyo inaficha ukweli kuhusu suala la ujauzito wa mtoto huyo na kuongeza kuwa Saimon Elias amehusishwa kwenye tuhuma hizo kama njia ya kukwamisha juhudi zake za kutaka haki itendeke.

“Huyu mama (Anna John) anawatumia watoto wake na wajukuu zake kujipatia kipato kutoka kwa wanaume wanaowataka kimapenzi, huyu si wa kwanza, yupo mwingine alipewa ujauzito akaachishwa shule pia.

“Watu wengi wakija kwa ajili ya kutaka kupata taarifa kuhusu mwanafunzi huyo kuzalishwa, huyo mama huwa analeta vituko sana, kuna askari alikuja kwa ajili ya kufanya upelelezi akamsingizia kuwa amevamia nyumbani na kumletea fujo,” anaeleza Munisi.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Kimara Stop Over, Magreth Mugyabuso, anabainisha kutokuwa na ufahamu wowote kuhusu sakata la ujauzito wa binti huyo na kutaka afikishwe ofisini kwake ili aeleze kwa kina ni nani aliyempa ujauzito huo.

Mtendaji wa Mtaa wa Kimara Stop Over, Erick Taratibu, anasema suala hilo limekaa kifamilia, hivyo hata uamuzi wake unahitaji busara za kutosha.

“Ukilitazama vizuri unaona kabisa kuwa chanzo cha hayo yote ni kulipiziana kisasi, kuna aliyetaka kutumia suala la mimba ya mwanafunzi kuwaangamiza wenzake, vilevile kuna ambao wametumia nafasi hiyo hiyo kutaka kumuangamiza anayewafuatilia.

“Kama mjomba mtu anasema yuko tayari vinasaba vyake vipimwe na vya mtoto ili ukweli ubainike mimi naona hiyo ndiyo njia sahihi halafu hatua nyingine zifuate,” amesema Taratibu.

Mkuu wa shule ya sekondari aliyokuwa anasoma binti huyo, Nsembo Kwandika, amelieleza JAMHURI kuwa baada ya mwanafunzi huyo kupimwa na kukutwa na ujauzito bodi ya shule ililazimika kumfukuza shule.

“Sisi tulifuata taratibu zote ikiwa ni pamoja na kumfukuza shule, kuhusu aliyetajwa kuhusika kwenye sakata hilo mimi simfahamu, kwa sababu wakati linatokea sikuwepo mimi nimekuta faili, nilipofika na kukabidhiwa shule kitu cha kwanza nilichofanya ilikuwa ni kumfukuza shule,” anasema Kwandika.

Askari wa Dawati la Jinsia katika Kituo cha Polisi Gogoni, ambako suala hili limekuwa likishughulikiwa, waliliambia Gazeti la JAMHURI kuwa sakata hilo wanalifahamu lakini hawako tayari kulitolea ufafanuzi hadi wapewe kibali na mkuu wa kituo hicho.

Hata hivyo JAMHURI lilifanya jitihada za kumpata Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni (RPC), Murilo Jumanne, na kulieleza kuwa hana taarifa kuhusiana na sakata hilo, hivyo apewe muda wa kulifuatilia.

Mzazi wa binti huyo, Laurent Adamu, anasema kuwa kuna fununu anazisikia kwamba mtuhumiwa ameingia makubaliano ya kumtunza mtoto na kwamba baada ya mkubaliano hayo alitafutwa mtu mwingine wa kumsingizia kusababisha ujauzito huo pale ambapo polisi watakapokuwa wakija kuwafanyia upelelezi.

1511 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!