Ni baba wa watoto wanne, mganga wa jadi aeleza siri imani ya utajiri wa kichawi

Maisha ya mtuhumiwa, Joel Nzuki, katika kesi ya mauaji ya watoto watatu wa familia moja yameelezwa kutokuwa na viashiria vya wazi kwa mhusika kuhusishwa na unyama huo, JAMHURI limeelezwa.

Kwa mujibu wa ndugu wa mtuhumiwa huyo, pamoja na wenzake wanaofanya biashara ya kuuza mbao pamoja katika soko la mbao, maarufu kama Kahawa Timber – mjini Makambako, mkoani Iringa, ni katika siku za mwisho kuelekea tukio hilo la mauaji ndipo mtuhumiwa alianza kuonyesha hali isiyokuwa ya kawaida.

Katika uchunguzi wake ulioshirikisha watu mbalimbali, wakiwamo ndugu na baadhi ya wafanyabiashara, wanakijiji na wakazi wengine wa mjini Makambako, JAMHURI limebaini kuwa hata hivyo mtuhumiwa huyo alikuwa mtu mwenye imani zinazoweza kuhusishwa na masuala ya ushirikina kwa kiasi fulani.

Safari yake ya maisha

Kwa mujibu wa umri wake wa miaka 35, mtuhumiwa alizaliwa mwaka 1984. Baba yake mlezi, ambaye ndiye baba mdogo mwenye watoto watatu anaodaiwa kuwaua mtuhumiwa huyo, Danford Nziku, alizungumza na JAMHURI akiwa nyumbani kwake kijijini Ikando, mkoani Njombe na kisha mwandishi wa gazeti hili kuzuru makaburi ya watoto hao watatu, na hata kaburi la bibi wa mtuhumiwa ambako mtuhumiwa huyo anadaiwa kuwa alikuwa akiweka fedha kwa ajili ya tambiko linalohusiana na masuala ya ushirikina yanayodaiwa kulenga kujipatia mali.

Katika mazungumzo yake na JAMHURI, Danford Nziku anasema: “Kijana huyo nilimlea mimi tangu akiwa mdogo  kabisa baada ya wazazi wake kufariki dunia. Na hata ugomvi baina yetu ulipoanza kwa madai kuwa mimi namloga, nilimweleza, kwa nini sikukuloga tangu ukiwa mdogo baada ya kuzaliwa na wazazi wako kufariki dunia, miaka yote hiyo nimekulea, kwa nini sijakuloga wakati wote huo?”

Mzazi mlezi huyo akaendelea kueleza: “Nilimlea na alipopata umri wa kwenda shule akaanza masomo, baadaye nikamsomesha shule ya ufundi wa makanika Ubaruku (Mbeya), baada ya kumaliza masomo yake hayo ya umakanika, akajifunza udereva, akaanza kujimudu kidogo kimaisha, na siku moja aliniambia ‘baba’ sasa nataka nikajitegemee, akaomba maeneo ambayo yalikuwa mali ya baba yake ili ayaendeleze, mambo yakawa hivyo.

“Maisha yakaendelea. Hata hivyo, siku moja alikuja na kusema anataka eneo la baba yake lenye ukubwa wa ekari 10, eneo lote anataka yeye. Bado nikamwambia haiwezekani, kwanza, eneo hilo si la baba yake tu, bali la babu yake, ambalo hata sisi wengine tuna haki nalo, kwa hiyo, wajukuu wote ni mali yao. Hapo ndipo ugomvi ulipoanza, na baadaye alianza kutoa madai kuwa ninamloga ili mambo yake yasiwe mazuri.

“Oktoba 10, 2018 alifika nyumbani kwangu akiwa na tairi la gari, mimi sikuwapo, alimkuta mke wangu (mama yake mdogo), mama huyo akamuuliza hili tairi la gari la nini? Akamjibu kwamba namtafuta baba (Danford), akiwa hapa ndipo utajua kazi ya hili tairi, kwa hiyo kazi ya hili tairi utaijua baadaye akirudi. Alipoona ninachelewa, alikwenda ofisi ya kiongozi wa kitongoji, hapo akalalamika dhidi yangu, kisha kiongozi wa kitongoji wakaongozana hadi ofisi ya mtendaji, nikapigiwa simu.

“Nilipofika akaulizwa hili tairi la nini? Akawaambia siwezi kujibu leo. Lakini maelezo yake yalikuwa malalamiko kwamba nimekataa kumpatia eneo la familia, vilevile mimi namfanyia vitendo vya uchawi kupitia mmoja wa watoto waliouawa. Huyu anao watoto wanne, mtoto wake mkubwa nadhani ana umri wa miaka 10. Sasa huyo mtoto mwenye miaka 10 anadai kwamba baada ya kuzaliwa shangazi yake (dada yangu mimi) ndiye aliyemtunza mkewe wakati wa kujifunzia, sasa anadai kuwa shangazi yake alichukua kitovu cha mtoto huyo na kukifanyia ushirikina, kwa hiyo alikuwa anadai apewe kitovu hicho. Shangazi yake anaitwa Rose Nyagawa, huu ulikuwa ugomvi mwingine. Katika hili, tuliamua kwamba koo mbili ziende huko kwa mganga wake anayempa tuhuma hizo kwenda kumsikiliza huyo mganga, hapa akagoma. Akasisitiza kudai kitovu.

“Viongozi wale walijitahidi kusuluhisha, wakataka tupeane mikono ya amani (kushikana mikono) ikawa hivyo, lakini mwenzetu bado alikuwa na dukuduku.”

Mzee huyo alisimulia pia madai ya namna ilivyokuwa siku ya kwenda kuwachukua watoto hao watatu ambao baadaye walikutwa wameuawa na kutelekezwa katika Mto Hagafilo, mkoani Njombe (hatuwezi kuweka maelezo hayo kwa kuwa tayari kesi imekwisha kufunguliwa mahakamani).

Mzee huyo ambaye alimtembeza mwandishi wetu katika makaburi ya wanawe watatu waliouawa, ikielezwa kuwa mkewe alijifungua watoto hao kwa njia ya upasuaji na amekwisha kushauriwa na madaktari kutokuendelea kujifungua kwa kuwa kufanya hivyo ni kuhatarisha maisha yake, vilevile JAMHURI lilifika katika kaburi ambako mara ya mwisho mtuhumiwa alizindika shilingi 15,000 baada ya kudaiwa kufanya mauaji ya watoto hao, lengo likiwa ni kujihakikishia tambiko hilo kutokumletea madhara kwa mujibu wa masharti ya mganga wake.

Kaburi hilo ni la bibi yake aitwaye Atupoha Mwinami, aliyefariki dunia mwaka 1998 na kuzikwa kijijini hapo (Ikando).

Eneo lake la kazi

Gazeti hili la JAMHURI lilifika eneo ambako mtuhumiwa huyo kwa miaka kadhaa amekuwa akiendesha biashara ya uuzaji wa mbao sambamba na wafanyabiashara wenzake kadhaa.

Katika mazungumzo yake na JAMHURI, Mwenyekiti wa soko hilo la mbao, David Msakala, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mtaa wa Rajab – Mahakamani, akizungumzia  maisha ya mtuhumiwa, alisema alikuwa mfanyabiashara mwenzao wa mbao sokoni hapo.

“Tuliishi naye bila kujua kwamba anaweza kuwa na tuhuma za namna hii. Inadaiwa chanzo cha haya ni uhasama na baba yake aliyemlea. Siku za mwisho kabla ya tukio hilo mwenzetu hakuwa katika utulivu wa akili, alikuwa mtu mwenye msongo wa mawazo hivi, aliwahi kutudokeza kuhusu kuwatuhumu baadhi ya wenzake kumfanyia mambo ya kishirikina, kwamba wamechukua nyota yake. Amewahi kuishi na wanawake wawili, mke wa kwanza walizaa naye na hawakuwa wakiishi pamoja, hadi hivi karibuni alikuwa na mkewe wa pili.

“Kibiashara, katika kipindi hiki cha mwisho ni dhahiri alionekana kuyumba. Alikuwa anauza mbao lakini baada ya mtaji nadhani kuyumba, akaamua kuuza mabanzi. Alikuwa anamiliki magari mawili aina ya Fuso lakini mwisho alibaki na gari moja la Fuso. Ni baba mwenye watoto wanne, wawili wa mke mkubwa, nadhani wengine wawili wa mke mdogo. Nadhani hawa watoto wa bi mkubwa, mmoja yuko kidato cha kwanza na mwingine darasa la nne, hawa wengine wawili wa bi mdogo watakuwa shule ya msingi.

Ilikuwaje tuhuma za mauaji?

Alipoulizwa na JAMHURI hali ilikuwaje baada ya kusikia mfanyabiashara mwenzao amehusishwa na tuhuma za mauaji ya watoto watatu wa baba yake mdogo, Msakala alijibu: “Wafanyabiashara wote hapa tulihamaki kwa sababu tulichokuwa tunajua ni kwamba tuliishi na mwenzetu, lakini ghafla tunasikia ni mtu hatari.

“Alikuwa mfanyabiashara mwenzetu na mwanachama mwenzetu kwenye chama chetu cha wauzaji wa mbao hapa sokoni. Baada tu ya hali hiyo, mimi kwa nafasi yangu ya mwenyekiti wa mtaa, tuliwataka wananchi wawe makini na watoto wao. Tukaamua wageni wote mtaani ni lazima waje na barua za utambulisho wa serikali ya mtaa au kijijini huko wanakotoka. Na hili watu wajue, sasa hivi ukija Makambako hauwezi kupokelewa mtaani hadi uwe na barua ya utambulisho kutoka huko unakotoka, waeleze tabia yako, lakini vilevile na sisi huko tunaweza kuwasiliana nao,” alieleza na kusisitiza kuwa kwa sasa (hadi alipozungumza na JAMHURI wiki moja iliyopita) hali ya taharuki Makambako na mtaani kwao alikokuwa akiishi mtuhumiwa imepungua, ingawa wazazi wameendelea kuwa makini na watoto wao.

  

Kauli ya Mganga Dk. Mwandulami

JAMHURI pia lilimtafuta mmoja wa waganga wa kienyeji wa tiba asili wa muda mrefu ambaye pia ni maarufu mkoani Njombe anayejitambulisha kwa jina la Dk. Anthony Mwandulami, ambaye haamini kwamba mauaji ya aina hiyo yanalenga kuwapa utajiri wahusika wa mauaji.

Katika mazungumzo yake na JAMHURI anaeleza: “Hakuna kiungo cha binadamu chenye kuweza kumsaidia mtu kupata utajiri. Kilichopo ama kinachosababisha mauaji hayo ni visasi.

“Kama mauaji ya watoto yamesababishwa na kupata viungo vyao basi watoto wa mitaani wasingekuwapo, wangeuawa,  lakini hawa wapo. Kwa hiyo kilichopo ni mauaji ya visasi.

Kisa cha mtoto mwingine

Katika hatua nyingine, JAMHURI lilishuhudia mazishi ya mtoto wa umri wa miaka minne, Meshack Mnyonga, katika Kijiji cha Ngalanga, aliyefariki dunia Februari 9 akiwa katika Hospitali ya Rufaa Mbeya akiendelea na matibabu baada ya kukatwa koromeo na mtu asiyejulikana.

Mtoto huyo katika mbio zake za matibabu Januari 19, mwaka 2019 aliruhusiwa kurudi nyumbani kwao Njombe kutokea Hospitali ya Rufaa Mbeya lakini ilipofika Februari 2, 2019 alirudishwa tena Hospitali ya Rufaa Mbeya, na hatimaye Februari 9, 2019 alifariki dunia.

Akizungumzia na JAMHURI kuhusu tukio hili wiki iliyopita, Balozi Aidan Chafumbwe, wa eneo la Mji Mwema, Kata ya Mjimwema, mkoani Njombe anasema: “Mtu alikuja kutoa taarifa mtoto amekatwa shingo, alichukuliwa hadi Kituo cha Afya Njombe Mjini na kisha Hospitali ya Kibena, sauti ilikuwa inatokea kooni badala ya mdomoni.

“Mama Ligwa (Jane Chanda) ambaye ndiye mjumbe katika kamati yetu aliongozana na mtoto huyo hadi Mbeya siku hiyo hiyo ya tukio kwa kuwa wazazi wa mtoto huyo hawakuwa wakijulikana, kwa hiyo jambo muhimu kwanza ilikuwa kuhakikisha mtoto anapata matibabu.

“Mtoto huyo alipatikana muda wa saa nne asubuhi, na hadi saa tisa alasiri safari ya kuelekea Mbeya ilianza. Tuliporudi baada ya kumsafirisha tulipata simu muda wa saa mbili kutoka kwa balozi wa eneo jingine kwamba kuna mtoto amepotea na balozi huyo akanieleza yupo na wazazi wa mtoto aliyepotea.

“Tuliwaeleza kuwa mtoto aliyepatikana amesafirishwa kwenda Mbeya kwa ajili ya matibabu zaidi. Siku iliyofuata wazazi wake walikwenda Mbeya kumpokea mama aliyesafiri na mtoto huyo, na mtoto aliendelea na matibabu na kwenda kuangaliwa tena hospitalini huko Mbeya kwa kadiri alivyopangiwa ratiba.”

Wanaamini katika tatizo gani?

Hapa balozi huyo anaeleza: “Misitu iliyoko kwenye maeneo ya makazi ni shida hapa Njombe, nadhani watu wa Idara ya Mipango Miji wanapoanzisha makazi wahakikishe hakuna misitu, utakuta watoto wanatembea mwendo wa mita hata 200 kando ya pori kwenda shuleni.

Hali inasikitisha, mtoto yule alichinjwa kama mtu anavyochinja mbuzi. Kijana mmoja ambaye ni fundi ujenzi ndiye aliyekuwa wa kwanza kumwona huyo mtoto akitokea porini, akivuja damu kooni.

Kuhusu hatua wanazochukua, kwa mujibu wa balozi huyo ni pamoja na kila balozi kuhakiki wakazi wake na hata wageni wanaoingia, na kwamba wameanzisha daftari la kuandikisha wageni wakazi.

Matukio ya mauaji mkoani Njombe yalitikisa taifa kuanzia mwishoni mwa mwezi Desemba mwaka jana, na hadi sasa watu kadhaa wanashikiliwa huku wengine watatu wakiwa wamekwisha kufikishwa mahakamani.

Waliofikishwa mahakamani kwa tuhuma za mauaji ya watoto watatu; Gilbert Nziku, Godlove Nziku na Gaspar Nziku ni pamoja na Joel Nziku (kaka wa watoto hao).

Please follow and like us:
Pin Share