Je, una akaunti ya benki nje ya nchi? Umewahi kujiuliza kuhusu usalama wa kadi yako? Hebu fanya mpango ukague kadi yako na ujiridhishe kama haijadukuliwa na fedha zako kutumika kulipa huduma ambazo hukuzitumia.

Mtandao unaojihusisha na matumizi ya kadi za benki za wizi katika ununuzi wa bidhaa na huduma umefikia tamati kwa kudhibitiwa na uongozi wa Shirika la Ndege la Air Tanzania, uchunguzi wa Gazeti la JAMHURI umebaini.

Uchunguzi wa JAMHURI unaendelea katika maeneo mengine ili kuthibitisha kama tatizo hilo lipo katika malipo ya huduma nyingine zaidi ya ununuzi wa tiketi za ndege.

Akizungumza na JAMHURI, Mkurugenzi Mkuu wa Air Tanzania, Mhandisi Ladislaus Matindi, amesema uhalifu huo uliibuliwa na Air Tanzania kupitia kitengo chake cha usalama wa ndani na kukabidhiwa kwenye vyombo vya usalama.

“Jambo hilo liligunduliwa na kitengo chetu cha usalama wa ndani kwa kushirikiana na vyombo vya dola, tumeusambaratisha mtandao huo,” anasema Mhandisi Matindi.

Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kwamba uhalifu huo hufanyika kwa kutumia taarifa za kadi za wateja zinazodukuliwa mitandaoni na vinara wa uhalifu na kisha kuuzwa kwa watoa huduma wasio waaminifu wakiwemo wakala wa uuzaji wa tiketi za ndege.

Baadhi ya wafanyakazi wa mashirika ya ndege ya Precisión Air na Fastjet ambao hawakutaka kutajwa majina yao gazetini, wanasema uhalifu huo umekuwapo kwa muda mrefu lakini haukuwahi kushughulikiwa ipasavyo.

Vyanzo vyetu hivyo vimesema baadhi ya wafanyakazi wenzao wamekuwa wakifukuzwa kazi kwa kujihusisha na uhalifu huo bila ya kuwa na mkakati endelevu.

JAMHURI limengundua kuwapo kwa makundi matatu yaliyoko katika mtandao huo wa kihalifu. Kundi la kwanza ni la chini kabisa likiwahusisha wakala wa uuzaji wa tiketi za ndege na watu binafsi ambao hutumia taarifa za kadi za benki zilizodukuliwa katika ununuzi wa bidhaa na huduma.

Kundi la pili ni wauzaji wa taarifa za kadi za benki zilizodukuliwa kwa ajili ya watumiaji wa taarifa hizo katika ununuzi wa bidhaa na huduma. Kundi la tatu linawahusisha wahalifu wa kimataifa wenye utaalamu wa mitandao ambao hudukua taarifa za kadi za benki mitandaoni bila wamiliki wa kadi kujua na kuziuza kwa madalali.

Gazeti la JAMHURI limebaini kwamba wadukuaji wa taarifa za kadi za benki mitandaoni wana mawakala wao sehemu mbalimbali duniani ambao hununua taarifa hizi kwa nia ya kuziuza kwa watoa huduma mbalimbali.

Mawakala hawa huwapa taarifa za kadi watoa huduma kama wauza tiketi za ndege kwa mapatano ya malipo kila taarifa hizo zinapotumika kununua tiketi.

Baada ya kupata taarifa za kadi zilizodukuliwa kutoka mitandaoni, watoa huduma hao wasio waaminifu huzitumia kwa mfano kukata tiketi za ndege mtandaoni, ambapo kinachohitajiwa ni hizo taarifa na uwepo wa pesa katika akaunti ya mtu aliyeibiwa taarifa za kadi yake ya benki.

JAMHURI limebaini kwamba bei ya tiketi wanayomwambia mteja anayehitaji tiketi inaweza kuwa nafuu kuliko bei halisi ya tiketi iliyo katika mfumo wa kuuza tiketi.

Hivyo, bei watakayolipa ili kupata tiketi katika mfumo wa ATCL kwa kutumia taarifa za kadi zilizodukuliwa kutoka mtandaoni ni bei halisi ya tiketi ya ATCL ambayo itakatwa kutoka katika akaunti ya mtu aliyedukuliwa taarifa za kadi yake.

Ili kutotiliwa shaka na wanunuzi wa tiketi hizi, mawakala wasio waaminifu hutengeneza tiketi nyingine yenye bei sawa na ile aliyopewa na mteja wake.

Wahalifu hao wa mtandao wamekuwa wakiuza tiketi kwa bei ya chini kuliko ile iliyowekwa na ATCL katika mfumo wa ununuzi wa tiketi kupitia tovuti (online) ili kuvutia wateja kutokana na ukweli kuwa hakuna gharama za ununuzi wa tiketi hizo zaidi ya pesa wanayolipa ili kununua taarifa za kadi za benki zilizodukuliwa.

Pesa wanayolipwa na wateja huingia mifukoni mwao huku akaunti ya mtu aliyedukuliwa taarifa za kadi yake ya benki ikilipia uhalifu huo bila mwenyewe kujua. Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kwamba baadhi ya abiria hununua tiketi hizo bila kufahamu kama kuna wizi umefanyika. Baadhi ya abiria hawana habari kuwa tiketi wanazouziwa zimetokana na matumizi ya taarifa za kadi za benki zilizodukuliwa.

JAMHURI limefahamishwa kwamba wanaoshiriki katika mchezo huo mchafu ni mawakala wadogo ambao hawana mtaji mkubwa na hawakusajiliwa na Shirikisho la Mashirika ya Ndege Duniani (IATA).  Mawakala walioonekana kujihusisha na mtandao huu wa kihalifu wako katika mikoa ya Mwanza, Mbeya, Arusha, Dar es Salaam na Zanzibar.

Gazeti la Jamhuri lilielezwa kuwa kwa kawaida mawakala wa tiketi za ndege huuza tiketi kwa makubaliano maalumu na mashirika ya ndege. Air Tanzania, kwa mfano, wakala hulipwa kiasi fulani cha fedha kama kamisheni ya kuliuzia shirika tiketi zake. Ikiwa tiketi imekatwa mtandaoni na kulipwa kwa kadi ya benki, kamisheni hiyo hailipwi.

Hiyo ina maana mawakala wa tiketi hawalipi kamisheni kwa uuzaji wa tiketi kwa kutumia taarifa za kadi za benki zilizodukuliwa. Hata hivyo, mawakala hao wanaoshirikiana na wadukuaji hukata tiketi mtandaoni na kupata fedha nyingi ambazo hulipwa na wateja lakini hazitumiki kukata tiketi kwani malipo ya tiketi hufanywa kupitia akaunti za wateja walioibiwa taarifa za kadi zao za benki.

Kundi la mawakala wanaohusika na uuzaji wa taarifa ya kadi za benki zilizodukuliwa na kuziuza kwa wauzaji wa tiketi za ndege linawahusisha wahalifu ambao wana uwezo wa kudukua taarifa moja moja au kuwa na mahusiano ya moja kwa moja na wadukuaji wa taarifa za kadi za benki walioko katika mitandao ya kihalifu nje na ndani ya nchi.

Kundi hilo ndilo lenye uelewa mpana na uhalifu huu. Kundi hilo limekuwa likiwauzia wakala wa tiketi taarifa zilizodukuliwa ambazo hutumika kununua tiketi kupitia mitandao ya makampuni ya ndege (online ticket purchase). Kundi hili linaonekana kuwa na washiriki mbalimbali wengi wao wakiwa hawana uhusiano wa moja kwa moja na uuzaji wa tiketi za ndege.

Katika kundi hilo amekutwa pia raia mmoja wa kigeni, ambaye baada ya kupekuliwa amekutwa na kadi zilizodukuliwa huku kadi hizo taarifa zake zikiwa zimesajiliwa katika mabenki yaliyoko nje ya nchi.

Mtandao huo kwa kutumia taarifa za kadi za benki zilizosajiliwa na mabenki yaliyoko nje ya nchi una nia ya kukwepa mkono wa sheria. Matumizi ya kadi zitolewazo na benki za Kitanzania yangerahisisha kukamatwa na kufumua mtandao wote.

Uamuzi wa ATCL kulishughulikia suala hili kisheria utasaidia kuliweka hadharani suala hilo na kuwafikisha katika mikono ya sheria wahalifu wanaojishughulisha na uharibifu.

Ili kuhakikisha madhara ya uhalifu huu yanamalizika, ATCL imeweka masharti kwa wasafiri walionunua tiketi kwa kutumia kadi za benki.

Mhandisi Matindi anasema wasafiri hao wanapowasili uwanja wa ndege kwa ajili ya safari hutakiwa kuonyesha kadi walizotumia kununua tiketi zao au nakala ya kadi hizo na nakala ya kitambulisho cha mtu aliyekununulia tiketi.

Mhandisi Matindi anasema pamoja na ukweli kuwa ATCL hupata pesa zake zote kupitia ununuzi ya tiketi kwa kadi za benki zilizoibwa, suala hilo linaweza kuharibu taswira ya kampuni, hivyo lazima lishughulikiwe na kukomeshwa kabisa.

By Jamhuri