MK Group na ngoma za maghorofani

*Ilikommbolewa na Miraji Shakashia akiwa shule ya msingi 

TABORA

Na Moshy Kiyungi

Kuna wanaodai kuwa muziki wa dansi umekufa kwa kulinganisha na ilivyokuwa miaka ya 1960 na 1990.

Wakati huo karibu kila mji ilikuwapo bendi ikitoa burudani kwa wakazi wa eneo husika.

Ipo miji iliyokuwa na bendi moja au zaidi!

Mfano Morogoro; Morogoro Jazz, Cuban Marimba na Super Volcano. Tabora; Tabora Jazz, Nyanyembe Jazz, Kiko Kidds na Milambo Jazz.

Tanga kulikuwa na Atomic Jazz, Jamhuri Jazz, Amboni Jazz na kadhalika.

Jiji la Dar es Salaam lilisheheni bendi lukuki katika miaka hiyo.

Kulikuwa na Kilwa Jazz, Western Jazz, NUTA Jazz, Dar Jazz, Super Matimila, Orchestra Safari Sound, MK Group, Maquis du Zaire, DCC Mlimani Park Orchestra, Kilimanjaro Band ‘Wana Njenje’, Vijana Jazz na nyingine nyingi.

Miongoni mwa bendi hizo ni Mlimani Park Orchestra, Kilimanjaro, Msondo na Vijana Jazz ndizo bado zinajikongoja hadi sasa.

Makala hii inaiangazia bendi ya MK Group iliyokuwa inaporomosha muziki katika hoteli za kitalii nchini.

Kabla ya kuanzishwa kwake, kulikuwa na bendi ‘mama’ ya African Stars iliyoanzishwa Julai 1, 1994 katika Hoteli ya Bahari Beach.

Mmiliki wa bendi hiyo alikuwa Ali Baraka, ambaye baadaye alianzisha bendi dada tatu; MK Group, MK Beats na MK Sound.

Mtunzi na mwimbaji Aboubakar Kasongo Mpinda ‘Clayton’ akisaidiana na Mbombo wa Mbomboka wakapewa jukumu la kuanzisha MK Group.

Wakawakusanya wanamuziki mahiri akina Kalala Mbwebwe, Paul Vitangi, mwanadada Rahma Shari na Green Simutowe aliyekuwa akiimba nyimbo za Kizungu.

MK Group ilisheheni magwiji wa kushika gitaa akina Monga Stanii, Kasongo Ilunga, Joseph Mulenga ‘King Spoiler’, Kawelee Mutimanwa, Omari Makuka aliyekuwa akipiga gitaa la kati ‘rhythm’ na Andy Swebe akiliungurumisha gitaa zito la besi.

Saksafoni alikuwa ni ‘Super Sax’ Mafumu Billal ‘Bombenga’ na tarumbeta zilipulizwa na Abdallah Tuba na Kayembe Ndalabuu ‘Trubloo’, kinanda alibofya Asia Darwesh ‘Super Mama Lao’ na kwa upande wa tumba alikuwapo Sidy Morris ‘Tanzania One’.

Bendi hii iliachia vibao vikali kama ‘Nikupe ukweli’, ‘Chako ni chako’, ‘Kibera’, ‘Tukale sangara’, ‘Nishike mkono’, ‘Kigeligeli’, ‘Kimasala’, ‘Madawa ya kulevya’, ‘Maria Maria’, ‘Losa’, ‘Mwintope’ na nyingine nyingi zilizokonga nyoyo za mashabiki wa muziki wa dansi.

Kwa umahiri wa wanamuziki hao, MK Group ikajizolea sifa lukuki ambapo kila mwisho wa wiki walikuwa wakipiga muziki katika Hoteli ya New Africa, Ukumbi wa Bandari Grill uliokuwa ukifurika wakicheza ngoma hizo kwa mtindo wa ‘Ngulupa’ huku wakipulizwa na upepo mwanana kutoka kwenye viyoyozi vilivyokuwa ukumbini humo.

Aliyekuwa kiongozi wa MK Group, Kasongo Mpinda ‘Clayton’, aliwahi kusimulia jinsi bendi ilivyopatwa na misukosuko baada ya mpiga gitaa Joseph Mulenga ‘King Spoiler’ kuacha muziki kwa sababu ya maradhi huku Kawelee Mtimanwa akijiandaa kwenda Ulaya, hivyo kuiacha bendi bila mpiga gitaa la solo.

Busara za viongozi zilitumika kwa kumfuata Miraji Shakashia ‘Shakazulu’; wakati huo akiwa mwanafunzi Shule ya Msingi Mlimani.

“Shakashia alikuwa bado mdogo, kwa hiyo tulilazimika wakati mwingine kukodi teksi kwenda Makongo kumtafuta alikokwenda kucheza na watoto wenziwe aje kupiga gitaa,” anasema Clayton.

Anasema mashabiki wa ‘ngoma za maghorofani’ walivumilia, wakisubiri kwa saa kadhaa ili Shakashia aletwe kupiga solo.

MK Group baada ya kumaliza mkataba wa kupiga muziki Hoteli ya New Africa, waliingia mikataba mingine katika hoteli za Morogoro na Luna kwa nyakati tofauti mjini Morogoro.

Wakati wa uhai wake, Kasongo Mpinda ‘Clayton’ alizungumza na mwandishi wa makala hii nyumbani kwake Mwananyamala, akieleza jinsi Shakazulu alivyoiokoa bendi yao kwa kupiga gitaa katika nyimbo zote zilizokuwa zikicharazwa na Joseph Mulenga na Kawelee Mutimanwa.

Baada ya mikataba yao kumalizika mjini Morogoro, walireja Dar es Salaam na kuwa mwisho wa bendi hiyo.

Kifo cha MK Group hakikuwa cha upweke, kwani hata bendi zake dada; MK Beat na MK Sound, nazo ziliyeyuka katika anga ya muziki, zikiiacha bendi mama ya African Stars ‘Twanga Pepeta’ chini ya Kampuni ya ASET ikitamba hadi sasa.

Baadhi ya wanamuziki wanaotajwa katika makala hii wamekwisha kutangulia mbele ya haki.

Mungu aziweke roho zao pahala pema peponi waliotutangulia. Amina.

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu namba: 0713331200, 0736331200, 0767331200 na 0784331200.