Makundi ya kuhasimiana ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), yameendelea kukiburuza chama hicho kwa kuimarisha mkakati wa kupachika wagombea wao kwenye nafasi mbalimbali ikiwamo Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC-CCM).

Habari zinasema makundi hayo yameendelea kusuguana wakati kila upande ukitaka kuhakikisha watu wake wanachaguliwa kushika nyadhifa muhimu ndani ya chama hicho tawala, kwa lengo la kupata ‘mashiko’ katika Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2015.


Kivumbi hicho cha kujinyooshea mapito ya Uchaguzi Mkuu ujao, kimezidi kushika kasi katika vikao vya juu vya CCM vinavyoendelea mjini Dodoma, kupitia na kuchuja majina ya wagombea nafasi mbalimbali katika chaguzi zinazoendelea ndani ya chama hicho.

Wadadisi wa masuala ya siasa wanatabiri kuwa uchaguzi wa viongozi wa CCM mwaka huu hautakuwa na mabadiliko makubwa, kutokana na taswira ya makundi ya kuhasimiana kuendelea kujiimarisha ndani ya chama hicho.


Chuki binafsi, uroho wa madaraka na kutafuta maslahi binafsi ni miongoni mwa matatizo yanayotajwa kuchangia kuwapo kwa makundi ya kuhasimiana yanayoendelea kukitafuna chama hicho.


Habari zaidi kutoka ndani ya CCM zinasema vigogo wengi wanaoshika nyadhifa mbalimbali ndani ya chama hicho, hususan tangu Serikali ya Awamu ya Pili nchini, wamejiandalia mazingira mazuri ya kuendelea “kuula”.


“Hapa tusitarajie mabadiliko makubwa maana hata ile mbinu ya kurudisha nafasi za u-NEC (ya CCM) wilayani kwa lengo la kupata viongozi wapya haina ‘mashiko’, tutarajie kuwaona vigogo walewale wakipewa nafasi,” kimesema chanzo chetu cha habari.


Tayari wajumbe wa Sekretarieti ya CCM waliokutana mjini Dodoma hivi karibuni, kufanya mchujo wa awali wa majina ya wagombea nyadhifa mbalimbali ndani ya chama hicho tawala, wamebariki majina ya watu waliowahi kuwa maarufu serikalini.


Habari kutoka Dodoma zinasema Mbunge wa Bariadi Mashariki, Andrew Chenge, Edward Lowassa (Monduli), Dk. Mary Nagu (Hanang) na Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye ni miongoni mwa waliokubalika mbele ya Sekretarieti hiyo. Lowassa na Sumaye ni miongoni mwa makada wachache wa CCM wanaoelezwa kuwa na nguvu kubwa ndani ya chama hicho, lakini pia wanaojipanga kusaka kwa nguvu kubwa urais mwaka 2015.


Kutokana na hali hiyo, vigogo hao na wengine wanaowania urais kupitia CCM, wanadaiwa kuongeza kasi ya kupigana vikumbo kwa gharama yoyote kuhakikisha wanafanikisha azma yao ya kuwa na wapambe wengi katika ngazi mbalimbali za uamuzi ndani ya chama hicho.

Ni dhahiri kuwa kupitishwa kwa majina ya vigogo hao na wengine wenye ushawishi mkubwa, ni kinyume cha mbinu mpya ya CCM ya kurejesha nafasi za ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho wilayani, kwa lengo la kupata ‘damu mpya’.


Wakati vigogo hao wakiangukiwa na neema hiyo, wagombea ujumbe wa NEC-CCM, Mbunge wa Nzega, Dk. Khamis Kigwangalla, na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa chama hicho Taifa, Hussein Bashe, ‘wamechinjwa’ katika Sekretarieti hiyo iliyoketi chini ya Katibu Mkuu, Wilson Mukama.


Inaelezwa kuwa sababu ya majina ya Dk. Kigwangalla na Bashe kukosa sifa mbele ya Sekretarieti hiyo, ni malumbano waliyofanya wakati wakichukua fomu za kuomba kuteuliwa kugombea ujumbe wa NEC-CCM katika ofisi ya chama hicho wilayani Nzega.


Habari zinasema wagombea hao vijana walizozana kiasi cha kufikia hatua ya kutoleana bastola, jambo linalotazamwa kama la kukiaibisha na kukidhalilisha chama hicho tawala mbele ya umma. Chanzo chetu cha habari kimedokeza kuwa mvutano baina ya Dk. Kigwangalla na Bashe ni matokeo ya mkakati wa siri unaoratibiwa na vigogo wachache, kwa lengo la kuwazibia mwanya wa kupata uongozi ndani ya CCM.


Hata hivyo, kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM kilichokutana kuanzia jana (Jumatatu) kinatarajiwa kukamilisha mchujo rasmi leo (Jumanne) mjini Dodoma, na kutoa mapendekezo ya mwisho kuhusu wanachama watakaogombea nyadhifa mbalimbali ndani ya chama hicho.


Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa, Nape Nnauye, ametoa ufafanuzi unaowatia matumaini Bashe, Dk. Kigwangalla na wengineo waliofyekwa pale aliposema kwamba Sekretarieti ya CCM haina mamlaka ya kuengua majina ya wagombea ndani ya chama hicho.


Uchaguzi wa mwaka huu unasubiriwa kwa hamu kubwa kutoa picha ya nguvu ya CCM katika kipindi hiki cha ushindani mkubwa wa kisiasa, kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka 2015. Taswira ya chaguzi za chama hicho mwaka huu imegubikwa na malalamiko mbalimbali kutoka kwa baadhi ya wagombea, wanaohisi kuchakachuliwa katika mchakato wa uchaguzi huo kuanzia ngazi za wilaya na mkoa.


Mbunge wa Musoma Vijijini mkoani Mara, Nimrod Mkono, amekikaripia chama hicho akisema kwamba ‘patachimbika’ ikithibitika kuwa jina lake limepigwa panga katika ngazi ya mkoa. Hata hivyo, kwa mujibu wa habari za hivi punde inasadikika kuwa jina la mbunge huyo limerudishwa.


Kwa upande wake, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, hivi karibuni aliinyooshea CCM kidole akidai kuwa imeruhusu mafisadi kuingia na kuvuruga chaguzi zinazoendelea.


“…Tumepata aibu kubwa ndani ya chama chetu wakati chaguzi zetu zikiendelea, viongozi wamepitisha vipaza sauti vya mafisadi, kazi yao kubwa ni kulinda maslahi ya mabwana zao na kuwafurahisha,” ni kauli ya Sitta kama alivyokaririwa na vyombo vya habari.


Bado matumaini ya wengi ni kwamba Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete, atasimama kidete kuhakikisha chaguzi zinazoendelea ndani ya chama hicho, zinawezesha kupata viongozi bora watakaomudu ushindani wa kisiasa kwa sasa na wakati wa Uchaguzi Mkuu ujao.

1101 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!