WAWATA St. Joseph na bei za vyakula za ‘kitalii’

Kwa kawaida watu wanyonge wamezitambua nyumba za ibada kama sehemu ya ukombozi! Haishangazi kuwaona kina mama, kina baba, watoto, wazee na watu wasiojiweza wakikimbilia makanisani na misikitini kunapotokea vurugu.

Haikushangaza kusikia mamia ya watu wakiwa wameuawa makanisani wakati wa Vita ya Kimbari nchini Rwanda mwaka 1994. Mkata Mitaa (MM) anaamini kuwa si wote waliouawa makanisani walikuwa Wakristo, bali hata Waislamu na wengine wasiokuwa na imani hizi za kimapokeo.

Ni kwa sababu hiyo, na kwa kutokana na kipato cha MM ambacho ni kidogo, amekuwa akipendelea kungia katika maeneo ya nyumba za ibada kupata chakula.

Miongoni mwa maeneo aliyoyachagua ni katika Kanisa la Mtakatifu Joseph (St. Joseph’s) jijini Dar es Salaam. Hapa ndipo ofisini kwa Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, kiongozi wa juu na mwenye heshima katika Kanisa Katoliki hapa nchini.

Hapo St. Joseph’s kuna mgahawa unaoendeshwa na Umoja wa Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA). Kunapikwa vyakula vya kila aina. Mapishi yao kwa kweli si haba, na pengine ni kwa sababu hiyo, hata mapadri na watawa wamekuwa wakimiminika hapo kununua chakula.

Pamoja na sifa za chakula kizuri, MM anasumbuliwa na kiwango cha bei. Alipoingia hapo akitaka auziwe ugali na nyama, akaambiwa alipe Sh 3,000. Alipotaka ugali kwa dagaa akatajiwa kiwango hicho hicho. Lakini cha ajabu ni kwamba kwenye nyama kimnofu kinachowekwa ni kama cha ‘kumtegea panya’ — ni kidogo kweli kweli.

MM akauliza bei ya ugali samaki. Akaoneshwa kijisamaki kidogo kweli kweli, lakini bei yake ikawa kuazia Sh 5,000 hadi Sh 5,550. Alipoomba sharbati (juisi) kwa sababu ni bora zaidi kiafya kuliko soda, akaambiwa kibilauli moja ni Sh 1,000.

Kuona hivyo MM akaamua kuvuka barabara. Akaenda upande wa pili kule kunakotumiwa kwa shughuli za boti na meli zinazokwenda na kutoka Zanzibar. Hapo akakuta bei ya ugali samaki ni Sh 1,500 huku vikisindikizwa na dagaa, mbogamboga, kachumbari na kadhalika. Sharbati bilauli moja ni Sh 500.

Baada ya kulinganisha bei ya sehemu hizi mbili, MM akawa ameshafikia uamuzi sahihi — uamuzi wa kuendelea kula kule baharini ambako Sh 2,000 zinatosha kabisa kumfanya aumalize mchana wake akiwa ameshiba vizuri.

Hadi hapo MM akawa hajui vigezo vinavyowafanya hawa WAWATA wawe na bei kubwa kiasi hicho, ilhali hata hapo walipo pengine hawalipi pango, na kama wanalipa, basi ni kiwango kidogo. Iweje kanisani kunakochukuliwa kama kimbilio la wengi kwa huduma kuwe ndiko kwenye bei za kitalii?

Pengine haya yanafanyika kwa sababu Mwadhama Polycarp Pengo hajawahi kubisha hodi hapo na kununua chakula. Siku akijaribu kuingia hapo, bila shaka atahoji iweje eneo hilo liwe maalum kwa wenye nazo, na masikini wakibaki pembeni.


1627 Total Views 3 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!