Kwanza, nianze kwa kutoa salamu za pongezi kwa Watanzania wote kwa kuadhimisha miaka 52 ya Uhuru wa nchi yetu jana.

Pili, ninatoa salamu za pole kwa wote tulioguswa na msiba wa shujaa wa dunia, Nelson Mandela. Mandela ataendelea kusimama kama muhimili na taa ya mfano kwa ukombozi wa kifikra kwa wanadamu wote.

Baada ya kusema hayo, leo ninapenda kuchambua namna fikra zinavyotengeneza ama kuua miito ya ujasiriamali kwa watu wengi.

Nikiwa muhula wa mwisho wa kuhitimu masomo ya shahada yangu ya kwanza, siku moja niliingia katika mjadala mzito na mama yangu mzazi. Alikuwa akishusha pumzi kuona kuwa mwanaye sasa ninaelekea kukamilisha ngwe ya elimu ya juu.

Mawazo na kiu yake kubwa ilikuwa ni kuona natafuta ajira mapema kitu ambacho mimi nilitofautiana naye, hivyo kuzusha malumbano ya kihoja na kimtazamo.

Wakati mama yangu akiamini mafanikio kupitia kuajiriwa, mimi niliamini (na ndivyo ninavyoamini na kuiishi imani hiyo), kuwa ukombozi wa kweli wa kiuchumi na kifedha utakuja kwa kuanza kujiajiri na hatimaye kuwa mwajiri wa wengine katika biashara ama shughuli zangu mwenyewe.

Haikuwa kazi rahisi kuubadilisha mtazamo wa mama yangu, hivyo nililazimika kutumia ushawishi wa hali ya juu na mifano hai. Kwa bahati nzuri nilikuwa nikibishana naye nikiwa tayari nimeshafanya ujasiriamali na yeye alikuwa shuhuda wa namna nilivyofanikiwa  na baadaye kufilisika kabla ya kuanza upya.

Hili tukio la kufilisika ndilo lililokuwa linampa ‘presha’ mama yangu kwa sababu alinihoji maswali mengi. “Mwanangu, biashara ni kama kubahatisha, hivi kweli na elimu yako hii unataka kuendelea kujiajiri? Je, itakuwaje ukifilisika tena? Huoni kama utakuwa mtu wa kubahatisha licha ya kuwa msomi? Kwanini usitafute ajira ili uwe na uhakika na mshahara wako kila mwezi?”

Bahati mbaya mimi nina ndugu na jamaa wengi ambao wanaamini mno katika mfumo wa kuajiriwa (huenda Watanzania wengi wako hivyo! Nikiwa nimepangua (kwa ushindi) mjadala huo na mama, nikakutana na ndugu yangu mwingine ambaye alinishangaa kuona nimebadili kutoka masomo ya sayansi kwenda kusoma masomo ya biashara. Kidato cha tano na cha sita nilisoma masomo ya sayansi, lakini ngazi ya chuo kikuu niliukana udaktari na kugeukia masomo ya biashara.

Yeye (ndugu yangu) alinipa kauli ifuatayo, ambayo hadi leo huwa ninaihesabu kuwa ni ya kitumwa, “Umeacha fani ya sayansi umekimbilia fani ya biashara, utapata shida sana. Fani za biashara siku hizi hazina ajira, wanaozisomea ni wengi mno. Ungebaki sayansi ungekuwa na uhakika wa ajira yako bila shida.”

Niliamua ‘kumpotezea’ kwa sababu mawazo yake na yangu niliona ni kama mbingu ilivyo mbali na nchi. Anawaza niajiriwe wakati mimi ninaumiza kichwa jinsi ya kuwapata wafanyakazi bora niwaajiri!

Fikra hizi za kusomesha watoto ama kusoma ili kuajiriwa ndizo zilizojaa katika fahamu za Watanzania wengi. Kwa bahati mbaya sana, kutokana na mabadiliko ya mifumo ya kisiasa na uchumi wa dunia, matumaini ya kila anayehitimu masomo yake kuajiriwa yanazidi kuyeyuka siku hadi siku. Hapa Tanzania hadi sasa kuna nafasi chache za ajira ikilinganishwa na idadi ya wasomi inayotapikwa na vyuo vikuu na vile vya kati.

Ukiacha hilo la ajira kuwa chache, bado kuna changamoto kwa wale wanaobahatika kuajiriwa. Changamoto hii ni kutotosheleza kwa mishahara (na marupurupu) inayotolewa ikilinganishwa na hali ngumu ya maisha pamoja na malengo anayokuwa nayo mwajiriwa.

Tena lipo jambo linalozidisha mbinyo na misongo miongoni mwa wasomi wetu kutokana na imani ambazo huwa nazo kuhusu maisha. Wengi wawapo masomoni huwa na ndoto za mchana za kuajiriwa leo na kutajirika kesho! Wanapoingia kazini na kukutana na uhalisia kuwa mambo siyo rahisi kama wanavyodhani, hapo ndipo huwa kinaanza kizaazaa! Udokozi, wizi na ufisadi huanzia hapa. (Japo kuna kazi hazina cha kuiba)!

Kwa hiyo, wanaoajiriwa na wale wanaokosa ajira, wasomi na wasiosoma wote wanajikuta katika changamoto moja kubwa, ‘msongo wa maisha’. Kwa maana hii, mtu apende ama asipende analazimika kufikiria kiutofauti ili kujiokoa. Suluhisho kubwa la changamoto hizi ni ujasiriamali.

Na hii ni dhahiri kwa sababu, mabadiliko ya kiuchumi na kisiasa yanasababisha matatizo, na matatizo siku zote ni fursa. Uhai wa ujasiriamali unategemea uwepo wa fursa. Ni bahati ilioje kuwa dunia ya leo (ikiwamo Tanzania) imekuwa na fursa nyingi za kiuchumi na kibiashara kuliko wakati mwingine wowote tangu kuasisiwa kwa Taifa hili. Ni suala la kujizoeza kufikiri na kuona tofauti na wengine.

Hivyo basi, utagundua kuwa suala la kusoma ama kusomesha huku kukiwa na mawazo kuajiriwa ni sawa na kujiandalia utumwa. Hali iliyopo sasa haimtambui mtu aliyeshikilia vyeti vyenye maksi nyingi ila mazingira yatambeba yule tu mwenye uwezo wa kupambana na kutatua changamoto za maisha zinazomzunguka (bila kujali elimu yake).

Tanzania ya leo lazima tuanze kujiokoa na kuokoa kizazi kijacho, tujenge mazoea ya kutengeneza ajira badala ya kulalamika kila kukicha kuhusu ukosefu wa ajira. Kama nilivyosema awali, ujasiriamali ndiyo eneo pekee linaloweza kutoa mamilioni ya ajira pamoja na kuwapa watu wengi uhuru wa kweli wa kiuchumi na kifedha. Kwanini kuwapo na fikra hasi kuona kuwa ujasiriamali si ajira kamili wakati ujasiriamali ndiyo unaoweza kuwapa watu uhuru wa kweli wa kiuchumi na kimaisha?

Natambua kuwa dhana ya ujasiriamali kuchukuliwa ‘poa’ kumechangiwa na mwenendo na utamaduni wa makundi kadhaa katika jamii nyingi. Kundi mojawapo ni la baadhi ya wafanyakazi wa kuajiriwa ambao wamekuwa na vimiradi vidogo vidogo vya ujasiriamali. Lengo lao kubwa huwa ni kupata faida fulani ambayo itasaidia kukabiliana na kutotosheleza kwa mishahara yao. Kwao hawa ujasiriamali siyo kazi ambayo inaweza kusimama peke yake na kumpa mtu uhuru wa kiuchumi na kimaisha.

Kundi hilo lina madhara makubwa kwa Taifa kwa sasa na wakati ujao. Hebu chukulia watoto wa mfanyakazi ambaye anaendesha vijimradi vya kijasiriamali labda kwa kuajiri watu ama baada ya kutoka kazini kwake ili kukabiliana na mshahara usiotosheleza. Picha inayojengeka katika fikra za watoto wake ni kuona kuwa ujasiriamali ni harakati za ‘kuganga njaa’.  Watoto hawa wanapokuwa moja kwa moja hawatakuwa na imani na ujasiriamali hata kidogo.

Lakini ninaomba kuwatambua wafanyakazi ambao hufanya ujasiriamali wakiwa ‘serious’. Kikawaida hawa huwa na malengo ya kufikisha mtaji ama hatua fulani kabla ya kuachana na ajira na baadaye kuwa mabosi katika shughuli zao wenyewe. Hata inapotokea wameendelea kufanya kazi (walikoajiriwa) ni kwa sababu wanapenda na kufurahia kufanya kazi hizo na siyo kwa ajili ya uhitaji wa fedha.

Wengine wanaopanda mbegu hasi za ujasiriamali kutoaminika ni wajasiriamali ambao licha ya kwamba wanafanya biashara na ujasiriamali kwa mafanikio makubwa, lakini wanashawishi familia, watoto na jamii zao kuamini kuwa ujasiriamali na biashara siyo kazi za kufanya. Hawa utawasikia wakiwaambia watoto wao kauli kama hizi;

“Usiangalie mali za mimi baba yako, urithi pekee ninaokupa wewe ni kukusomesha ili uje uwe na kazi yako”. Kauli hii kwa haraka haraka inaonekana ni yenye busara kubwa, lakini kutokana na mabadiliko yanayotokea sasa duniani, hii  ni imani ya kufisha. Siku huyu mtoto akikosa ajira, utamkuta ameshika bango na anaandamana barabarani kudai ajira (sijui nani atakuwa akidaiwa hiyo ajira)!

Kwa upande mwingine wajasiriamali wenyewe kuna kauli ambazo huwa tunazitumia ambazo zinatuondolea heshima mbele ya fikra za jamii na kutujazia hisia hasi. Hebu fuatilia tofauti ya mfanyakazi wa kuajiriwa na mjasiriamali kauli wanazotoa kabla ya kuondoka asubuhi kuelekea

katika mishughuliko.

Mfanyakazi ambaye huenda analipwa mshahara wa chini ya shilingi laki tano kwa mwezi anaaga kwa kusema, “Ninaenda kazini, tutaonana jioni.” Lakini mjasiriamali ambaye ana uhakika wa kuzalisha wastani wa faida ya shilingi milioni mbili kwa mwezi anaaga kwa kusema, “Ninaelekea kuhangaika, ninaenda kuchakalika, tutaonana jioni!”

Kabla hujaingia katika kufanya biashara zako tayari umeutangazia ubongo wako kuwa kuna mahangaiko siku hiyo! Ndiyo maana si ajabu kuona kuwa wafanyabiashara wengi licha ya kuwa wanatengeneza mamilioni ya faida kwa mwezi zaidi ya wafanyakazi wa kuajiriwa; lakini bado hawajiamini ukilinganisha na wafanyakazi wa kuajiriwa.

Binafsi katika ujasiriamali nimeizoeza akili yangu kujitambua kuwa mimi ndiye bosi hata kama niwe katika biashara yenye mtaji mdogo kiasi gani. ‘I am my own boss’. Shida ya wajasiriamali wengi huwa hawathamini hata maeneo wanayofanyia kazi. Kama ni dukani, ni vema ukaweka hata meza fulani ya kisasa na kiti cha ‘kujiachia’ ili akili yako inavyoingia kazini iwe inapata uhuru wa kifikra na kufurahia mazingira ya biashara.

Unapojitambulisha kwa watu usijitambulishe kinyonge, ongea kwa kujiamini. Wajasiriamali tunawajibika kujitoa asilimia zote kufanya biashara pasipo manung’ununiko. Haina tija kuwa katika  ujasiriamali huku tukitamani tena kuajiriwa.

Unapochukua hatua ya kuufurahia ujasiriamali uufanyao, ndipo utakapogundua kuwa ujasiriamali ni ajira kamili na kazi inayoweza kukupa fedha za kutosha na muda wa kutosha kufurahia maisha.

0719 127 901

[email protected]

By Jamhuri