Mkataba wa mauziano ya nyumba kati Shirika la Bima la Taifa (NIC) na Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), uliofanyika Oktoba 8, 2009 unadaiwa kuwa ni batili kwa kuwa taasisi iliyonunua haina uhalali kisheria.

Mkataba huo unahusu nyumba zilizoko eneo la Kijitonyama, Dar es Salaam viwanja namba 75-78 kitalu namba 45 ‘B’ ukihusisha hati namba 186217/3, 186217/4, 86217/6 na 186217/7 zilizopangishwa kwa wafanyakazi wa Bima ambao bado wanaishi kwenye nyumba hizo.

Wafanyakazi hao wameishi katika nyumba hizo kwa kipindi cha kati ya miaka 12 hadi 20, kabla ya kufukuzwa kazi kutokana na maombi yao ya kuuziwa makazi hayo kwa utaratibu uliokuwa ukifanywa na shirika hilo wa kuuza nyumba kwa watumishi wake waliopangishwa.

Wafanyakazi hao walioitumikia NIC kwa kipindi cha kati ya miaka 32 na 38, wameieleza JAMHURI kwamba nyumba hizo ziliuzwa bila kuzingatia maagizo yaliyotolewa na Serikali Oktoba, 2009 kwamba ziuzwe kupitia Wakala wa Majengo ya Serikali (TBA) kwa bei ya soko ikiwa ni Sh bilioni 31.7.

Lakini nyumba hizo hazikuwekwa kwenye orodha ya mali zote za Bima zilizotakiwa kuuzwa kwa lengo la kulifufua Shirika hilo lililokuwa na hali mbaya kifedha na madeni makubwa na kuwekwa katika mpango wa kubinafsishwa.

Nyumba hizo hazikuwekwa kwenye orodha ya mali zilizotakiwa kuuzwa, lakini kwa dalili zinazoonesha ufisadi, ziliuzwa kwa utaratibu usieleweka na baada ya mauzo inaelezwa zilikabidhiwa kwa TBA ambao walikataa kuzipokea kwa utaratibu huo kwani awali hawakukabidhiwa.

Hata hivyo, utata wa mkataba wa Shirika la Bima na BAKITA unaelezwa kwamba taasisi hiyo haina uhalali wa kisheria kununua, kuuza ama kushtakiwa kwa sababu haikusajiliwa kwa jina hilo (BAKITA) bali National Kiswahili Council kwa mujibu wa sheria namba 7 ya mwaka 1983 kifungu cha 4  kinachohusu mabaraza.

Nyumba hizo ziliuzwa kwa BAKITA kwa Sh bilioni 1.5 ambazo zilitakiwa kulipwa katika awamu mbili – Sh milioni 750 kila awamu na mkataba huo kusainiwa na aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bima, Justine Mwandu, na Katibu wa Shirika, Ted Mwakifuna.

Kwa upande wa BAKITA, waliosaini mkataba huo wa mauziano ni aliyekuwa Katibu Mtendaji, Dk. Anna Kishe, na Katibu Mtendaji Msaidizi, Noel Karekezi.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Wakili Mchungaji Justine Kaleb, katika kitabu chake cha Jukwaa la Sheria akieleza kuhusu uhalali wa mkataba kisheria, anasema ni lazima uwe na mambo matano ikiwa ni pamoja na makubaliano, malipo halali, uwezo au mamlaka ya kuingia kwenye mkataba, hiari na uhalali wa jambo.

Kuhusu uwezo au mamlaka ya kisheria ya kuingia kwenye mkataba (capacity to contract) anasema; “Uwezo wa kuingia kwenye mkataba humaanisha mamlaka ya kisheria ya mtu kuingia kwenye mkataba. Ni agizo la kisheria kwamba mtu hawezi kuingia mkataba na mtu mwingine kama hana uwezo wa kisheria kuingia kwenye mkataba huo,” inaeleza sehemu ya kitabu hicho.

Kuhusu hiari (free consent) anaeleza; “Mkataba wowote ni lazima ufanyike kwa hiari kutoka pande zote mbili zenye nia ya kuingia katika mkataba. Mkataba wowote ambao unafanyika pasipo hiari ya mhusika, hufanya mkataba kuwa batili.”

Uhalali wa mkataba unaweza kubatilishwa kwa mtu kuingia katika mkataba kwa kulazimishwa, vitisho, kudanganywa au kughushi.

“Pia kuhusu uhalali wa jambo (lawful object), mkataba wowote ni lazima ufanyike juu ya kitu ambacho ni halali kisheria na si kitu ambacho hakiruhusiwi kufanyika kisheria. Chombo chochote cha sheria hakiwezi kutekeleza mkataba ambao hufanyika juu ya kitu kilichokatazwa kisheria, kilicho kinyume na sera za Serikali au kilicho kinyume na maadili ya jamii. Kwa mujibu wa kifungu cha 23 (1) cha Sheria ya Mikataba sura ya 345 kama ilivyorejewa mwaka 2002,” anaeleza Wakili Kaleb.

Hadi Juni 30, 2009 madai ya bima za maisha na zisizo za maisha yalifikia jumla ya Sh bilioni 24.10 na hivyo Kamati ya Fedha na Uchumi katika mpango wake wa kurekebisha Shirika hilo, uliofuatiwa na kikako cha Baraza la Mawaziri kilichojadili Waraka namba 41/2008 kwa kutoa maagizo ya Serikali kwamba Bodi mpya ya Ushauri na Menejimenti kuteuliwa na kusimamia marekebisho hayo.

Kamati hiyo ilitakiwa kusimamia kazi ya kuuza baadhi ya mali na majengo ya Shirika yasiyokuwa msingi wa biashara ya bima kupata fedha za kulipa madai, kugharamia marekebisho ya Shirika pamoja na kukidhi matakwa ya Sheria ya Bima namba 18 ya mwaka 1996.

Majengo ya Bima yaliyotakiwa kuuzwa chini ya utaratibu uliowekwa na Baraza la Mawaziri yalikuwa 42 nchini kote, yakiwamo maghorofa na viwanja visivyoendelezwa vilikuwa 14 katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Mbeya, Lindi, Mtwara, Rukwa, Mara na Iringa.

1573 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!