*Kikao cha siku moja walipata Sh milioni 7

*Mjumbe mmoja asaini posho mara mbili

*Mkewe Mudhihir ambaye si mjumbe alipwa

 

Ufisadi unazidi kuwaandamana viongozi wa CCM. Safari hii, Mbunge wa Viti Maalumu, Anna Abdallah, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho pamoja na wajumbe wa Bodi hiyo, wanatuhumiwa kujilipa mamilioni ya shilingi. Ulaji huo umefichuliwa na Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Rose Kamili, katika hotuba yake ya makaridio ya mapato na matumizi ya mwaka wa fedha wa 2012/2013

 

BODI ZA MAZAO YA BIASHARA NA MAENDELEO YA KILIMO

Mheshimiwa Spika, kilimo cha mazao ya biashara hapa nchini kwa sasa kina changamoto nyingi. Changamoto hizo ni pamoja kukosa soko na bei za uhakika za mazao hayo.

Malengo ya kuwa na bodi hizi za mazao ilikuwa ni kuwasaidia wakulima kupata masoko na bei nzuri kwa mazao yao. Ila cha kusikitisha bodi hizi badala ya kupigania haki za wakulima, zimekuwa zikijali masilahi ya wajumbe wake huku wakulima wakiachwa bila msaada wowote.

 

Mheshimiwa Spika, kwa kuonyesha jinsi bodi za mazao sizivyowatendei haki wakulima wa nchi hii, naomba kunukuu sehemu ya hotuba ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni aliyoitoa hapa bungeni mapema Juni 25, 2012. Nanukuu:

 

“Mheshimiwa Spika, changamoto kubwa tuliyonayo ni kwamba mfumo wetu wa kilimo cha mazao ya biashara kimehodhiwa na Bodi za Mazao ambazo kazi yake kubwa ni kunyonya (extractive behaviour) wakulima badala ya kuwaendeleza. Bodi za mazao yote hapa nchini kama zilivyoundwa baada ya kuvunja Mamlaka za Mazao, zimeonyesha kushindwa kabisa kusimamia mazao yao.

 

Mkulima ndiye anayeathirika na Bodi za Mazao kutokana na maamuzi yao ambayo hayazingatii haki za wakulima na bodi hizi kuongozwa kisiasa zaidi na makada wa CCM wakiwamo wabunge kuliko utaalamu.

 

Ni hakika basi kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) hakiwezi kukwepa lawama ya kilio cha wakulima wa nchi hii, kwa kushindwa kuongoza bodi hizi na kuzigeuza vitegauchumi”, mwisho wa kunukuu.

 

Bodi ya Korosho na matumizi mabaya ya fedha za wakulima

Mheshimiwa Spika, kwa kukazia hoja ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, naomba nitoe mfano wa Bodi ya Korosho jinsi inavyowanyonya wakulima wa korosho katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Pwani na Ruvuma kwa kujilipa posho nyingi na marupurupu mengine huku wakiwaacha wakulima wa korosho wakiteseka na kuhangaika huku na huko kama kondoo wasio na mchungaji bila kutatua matatizo yao.

 

Bodi ilipokea kiasi cha Sh bilioni 2 kati ya mwezi Oktoba 2011 na Januari 2012 kutokana na ushuru wa mazao ya nje (export levy) ya korosho kwa msimu wa mwaka 2010/2011. Kiasi hicho kilikuwa ni kwa ajili ya shughuli za kuendeleza tasnia ya korosho nchini.

 

Kwa masikitiko makubwa, fedha hizo hazikutumika kufanya shughuli kama ilivyotarajiwa, na badala yake zilitumika kugharimia vikao vya bodi ya wakurugenzi na safari za viongozi (menejimenti ya bodi) ambazo hazijaleta tija kwa tasnia nzima kama ilivyokusudiwa.

 

Hayo yanapata ushahidi kutokana na matumizi ya kulipa posho kwa wajumbe wa bodi wanaounda Kamati ya Ajira na Uwekezaji ambayo wajumbe wake ni wanne, lakini aliwekwa na mke wa mjumbe katika malipo.

 

Kwa kikao cha siku moja kilichofanyika Novemba 29, 2011 wajumbe wa bodi hiyo walilipwa posho kama ifuatavyo:

1.  J. Bwanausi – Mjumbe wa Bodi:  Huyu alilipwa jumla ya Sh 1,550,000, ikiwa Sh 750,000 ni posho ya kawaida (per diem) na Sh 800,000 ni “working session” kama ilivyoandikwa kwenye fomu ya malipo.

 

2. Anna M. Abdallah – Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi: Huyu alilipwa jumla ya Sh 1,800,000 kwa mchanganuo ufuatao: Posho ya kikao Sh 500,000, usafiri Sh 300,000;  posho ya kawaida (per diem) Sh 900,000 na usafiri Dar es Salaam Sh 100,000.

 

3. Jerome Bwanausi – Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi: Huyu alilipwa kwa mara nyingine tena kwenye kikao hicho hicho jumla ya Sh 1,550,000 ikiwa posho ya kikao ni Sh 400,000; usafiri wa ndege Sh 300,000; posho ya kawaida (per diem) Sh 750,000 na usafiri Dar es Salaam Sh 100,000.

 

4. Mudhihir M. Mudhihir – Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi: Huyu alilipwa jumla ya Sh 1,550,000 ikiwa posho ya kikao ni Sh 400,000; usafiri wa ndege Sh 300,000; posho ya kawaida (per diem) Sh 750,000; usafiri Dar es Salaam Sh 100,000.

 

5.    Mrs. Mudhihir M. Mudhihir – Mke wa Mudhihir M. Mudhihir: Huyu alilipwa jumla ya Sh 875,000 kwa mchanganuo ufuatao: Posho ya kikao Sh 200,000; usafiri Sh 300,000; posho ya kawaida (per diem) Sh 375,000.

 

Mheshimiwa Spika, jumla ya fedha zote zilizolipwa (kwa watu watano) katika kikao hiki cha Wakurugenzi wa Bodi ya Korosho cha Novemba 29, 2011 ni Sh 7,325,000. Licha ya matumizi ya fedha hizi kuwa hayana tija kwa kuwa matatizo ya wakulima wa korosho hayajapatiwa ufumbuzi hadi sasa, utaratibu walioutumia wajumbe hawa kujipatia fedha hizi una dalili za kifisadi ndani yake.

 

Hii ni kwa sababu mke wa Mudhihir M. Mudhihir ambaye si mjumbe wa kikao aliingia kwenye kikao na kulipwa posho. Utaratibu uliotumika kumlipa mke wa Mudhihir haueleweki na hata viwango vilivyotumika kukokotoa malipo yake pia havifahamiki.

 

Dalili ya ufisadi mwingine katika Bodi hii ni kwa Mjumbe wa Bodi, Jerome Bwanausi kulipwa posho hiyo mara mbili. Katika fomu za malipo kwa Bwanausi, fomu moja ameandika jina lake kwa kifupi yaani J. Bwanausi na tarehe ya kuchukua fedha ameandika ni tarehe 28/11/2011 wakati katika fomu ya pili ya malipo ameandika jina kamili yaani Jerome Bwanausi na tarehe ya kuchukua fedha kaandika 29/11/2011.

 

Mheshimiwa Spika, mazingira kama hayo yanaibua hisia kuwa Bwanausi alijipatia fedha hizo kwa njia ya udanganyifu, na hivyo kuwaaminisha watu kuwa alitumia nafasi yake kama Mjumbe wa Bodi ya Korosho kuchukua fedha za wakulima wanyonge wa korosho.

 

Kambi ya Upinzani tunaitaka Serikali kutoa majibu juu ya bodi hizi za mazao na utaratibu wa kulipana posho jinsi ulivyo. Aidha, tunamtaka Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kufanya ukaguzi maalumu (special audit) kwenye matumizi ya bodi hii.

 

By Jamhuri