Mke wa mfanyabiashara Peter Zakaria, Anthonia Zakaria, amekiri kosa la uhujumu uchumi na kuhukumiwa kulipa faini ya Sh milioni 54.

Alikuwa akishtakiwa kwa kosa hilo baada ya kujipatia mali za Chama Kikuu cha Ushirika Nyanza cha mkoani Mwanza.
Mali hizo ni jengo lenye ghorofa tatu na eneo kilipojengwa kituo cha mafuta, Barabara ya Nyerere jijini Mwanza.
Mali hizo zilimilikiwa na Nyanza (1984) na baadaye mwaka 2002 familia ya Zakaria ilizinunua kutoka Nyanza.

Rais John Magufuli ametangaza vita dhidi ya wahujumu uchumi, akiwataka wote walionufaika na mali hizo kinyume cha sheria wafikishwe mbele ya vyombo vya sheria.

Amekaa rumande katika Gereza la Butimba kwa zaidi ya mwaka, wakati kesi yake Na. 3 ya mwaka 2018 ilipokuwa ikiendelea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza.
Januari 23, mwaka huu mahakama hiyo ilimtia hatiani na mwenzake, Timoth Kilumile, kwa makosa matatu baada ya kukiri. Mashtaka yaliyowakabili ni ya kula njama, kujipatia mali kwa njia ya udanganyifu, na kuisababishia hasara serikali.
Baada ya kukiri makosa hayo, mahakama iliwahukumu kifungo cha miaka minane jela au kulipa faini ya Sh milioni 27 kila mmoja. Washtakiwa walilipa faini.

Nje ya mahakama, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Biswalo Mganga, amesema Anthonia na Kilumile walitumia ujanja ujanja kupata mali hizo.

 “Jengo hili mnaloliona pamoja na hii sheli ni mali ya Nyanza, lakini mwaka 2002 kuna watu wajanja walitumia ujanja ujanja kuhakikisha kuwa wanalichukua. Wakatumia hoja zao za ujanja na madalali wengine walishafariki. Walikuwa kundi la watu wengi…
“Wakafungua kesi mahakamani, kesi ikaenda na wanasheria wa Nyanza kwa sababu walikuwa sehemu ya njama zile wakahakikisha Nyanza inashindwa na jengo linaondoka. Jengo hili mwaka 2002 lilichukuliwa kwa Sh milioni 42. Upelelezi umefanyika tukaja kufungua kesi Namba 3 ya mwaka 2018, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza.
“Kesi imeendelea, watuhumiwa Zakaria na mwenzake Kilumile wakiwa ndani. Leo hii (Januari 23, 2019) wamekiri makosa yao mbele ya mahakama.
“Hii ni baada ya mimi Mkurugenzi wa Mashtaka nchini kutoa kibali ili Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Mwanza iendelee na kesi hiyo, ambayo ni kesi ya uhujumu uchumi,” amesema.

 Amesema ingawa jengo walilinunua kwa Sh milioni 42, wao mwanzoni walikuwa wanadai Sh milioni 49.
“Nyanza wao na watu wa DPP ambao walikuwa sehemu ya njama hizo wakalipa milioni 49 pamoja na kwamba jengo liliuzwa kwa Sh milioni 42, bado Nyanza ikalipa tena milioni 49. Sasa unaweza ukaona kulikuwa na mchezo wa aina fulani.
“Hili jengo si mali ya Anthonia Wambura Zakaria. Ni mali ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Sasa, kwa sababu kuna wapangaji, ninyi watu Meneja wa Nyanza (Juma Mokili) hakikisha unapata mikataba yote ya watu waliopanga humu.
“Fedha hizo uangalie, wanamlipa nani na shilingi ngapi. Mikataba hiyo haitakiwi mtu mwingine tena. Lazima muangalie jengo lenyewe na sisi kama Serikali tutafuatilia,” amesema.
Kwa upande wake, Mokili, amesema mali hizo ni miongoni mwa mali zilizotakiwa kurejeshwa tangu Aprili, mwaka jana.
Amesema watu saba wengine walishakubali kurejesha mali walizojitwalia, wakiwamo baadhi ya viongozi wa wakati huo.
Miongoni mwao ni aliyekuwa Mwenyekiti wa Nyanza, Jacob Shibiliti, ambaye baada ya kufikishwa mahakamani kesi yake ilifutwa.
“Aliyekuwa amebaki ni huyu mmiliki wa KAUMA wakati huo (Anthonia Zakaria). Kwa hiyo kukubali kwake leo, maana yake ni kwamba tutakuwa tumekamilisha mali 10 ambazo zilikuwa zimechukuliwa kwa njia zisizo halali,” amesema Mokili.
Mume wa Anthonia, Peter Zakaria (59), anayemiliki Kampuni ya mabasi ya Zakaria bado yupo rumande akikabiliwa na kesi mbili za kujaribu kuua maofisa wa Usalama wa Taifa; na uhujumu uchumi.
Inadaiwa kuwa Juni 29, mwaka jana katika Mtaa wa Anglikana mjini Tarime, Mara, Zakaria aliwapiga risasi maofisa usalama hao.
Katika kesi hiyo Na. 3 ya 2018 iliyosikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mara, mfanyabiashara huyo anatetewa na mawakili wawili; Onyango Otieno na Kassim Gilla. Upande wa mashtaka yupo Wakili Lukelo Samwel.
Msemaji wa familia ya Zakaria, Samuel Chomete (66), amezungumza na JAMHURI na kusema asingependa kulizungumzia suala hilo.
“Yamekwisha. Kama unataka mambo zaidi nenda pale mahakamani watakueleza,” amesema.

2554 Total Views 1 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!