Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isaac Kamwelwe amesema mafunzo yanayotolewa sasa na Chuo cha Bandari yalenge kutatua matatizo yaliyomo katika sekta ya huduma za meli, biashara za bandari na shughuli za bandari.

Mhandisi Kamwele ametoa kauli hiyo katika mahafali ya 17 ya Chuo cha Bandari yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki. Pia Waziri alielekeza wahitimu wote 196 kupatiwa ajira Bandari.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TPA,  Prof. Ignatus Rubaratuka yeye amesema Bodi ya Wakurugenzi wataendelea kukiboresha chuo hicho kuwa cha kisasa zaidi katika miundombinu na vifaa vya kufundishia, huku wakiwawezesha watumishi wawe na viwango vya elimu stahiki. Kwa kuanzia, Bodi hiyo ilielekeza kununuliwa kwa mtambo wa kufundishia.

Mwenyekiti wa Bodi ya Magavana ya Chuo cha Bandari, Mhandisi Deusdedit Kakoko amesema kutatua changamoto ya vifaa vya kufundishia chuoni hapo, TPA tayari imeingia mkataba wa kununua mtambo mkubwa wa kufundishia uendeshaji wa vyombo vyote vya kupakia na kupakua mizigo bandarini. Mtambo huo utakaogharimu takribani Sh bilioni 1.5 utakuwa umefungwa ndani ya miezi sita kuanzia sasa.

Mkuu wa Chuo cha Bandari, Dk. Joseph Kakeneno amesema chuo kinakusudia kutoa stashahada za juu na shahada ya kwanza ya kuongeza ujuzi wa utendaji kazi katika taaluma zinazohusiana na huduma za meli kwa ajili ya usafirishaji kwa njia ya maji na menejimenti ya shughuli za Bandari.

Please follow and like us:
Pin Share