*Aeleza sababu za kusaini kumng’oa Waziri Mkuu
*Asukumwa na wizi uliofanywa mgodini Buhemba

Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono (CCM), ameamua kueleza sababu zilizomfanya asaini fomu ya majina ya wabunge katika kusudio la kumpigia kura Waziri Mkuu Mizengo Pinda ya kutokuwa na imani naye.
Mkono, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ameiambia JAMHURI kuwa uamuzi wake unatokana na kuguswa na hoja iliyowasilishwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema).

Amesema alichofanya hakina tofauti na kilichowahi kufanywa na Rais Jakaya Kikwete wakati wa mchakato wa kuandikwa kwa sheria ya kuundwa kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Kama kuna jambo zuri ni vizuri tukaliunga mkono bila kujali kama limetolewa na CCM au Chadema.

“Kwenye sheria ya kuunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba waheshimiwa wabunge tulipitisha ile sheria, lakini baadaye Chadema wakamfuata Mheshimiwa Rais Kikwete – na wengine pia walifanya hivyo – wakaeleza hoja zao na Mheshimiwa Kikwete zikamgusa, akaona zina mantiki, akaamua Serikali yake iandae amendments na kuzifikisha bungeni.

“Kwa hiyo alichofanya Mheshimiwa Rais ni kukubaliana na hoja bila kujali anayezitoa ni mpinzani au ni mwana-CCM. Hapa ni suala la kuona masilahi mapana ya Watanzania.

“Hata mimi nilipoona hoja ya Mheshimiwa Zitto ya kutaka tupige vita ufisadi nikaona hii ni hoja ya msingi, na kwa kweli wapigakura wa Musoma Vijijini wasingenielewa kama wangebaini kuwa siungi mkono suala la kutaka kudhibiti upotevu wa fedha za umma.

“Nilichokifanya nasema hakina tofauti na alichokifanya Mwenyekiti wangu Mheshimiwa Kikwete…kama wapinzani wana hoja nzuri ni vema tukawaunga mkono,” amesema.

Alipoulizwa kilichomsukuma zaidi kutekeleza azma hiyo Mkono akajibu; “Ukifika pale Buhemba ukaona namna mgodi ulivyoporwa vifaa kuanzia nyumba hadi mitambo, huwezi kunyamazia hali hiyo.

“Pale Buhemba pamebaki mashimo na magofu wakati wale Wazungu walipoondoka waliacha mitambo, magari, nyumba na kila kitu. Tulitarajia kuwa baada ya kuwa hawakuacha chochote kama huduma za afya na elimu, basi wananchi wangeambulia hivyo walivyoacha.

“Jambo la kusikitisha ni kuona polisi waliopewa jukumu la kulinda mali hizo, ndiyo hao hao waliogeuka na kuwa wezi na kuwasaidia wezi wengine kupora mali zote. Hata ungekuwa wewe ukiona ile hali ya Buhemba na kisha ukaambiwa usaini fomu ya kutaka mawaziri wajiuzulu, ni lazima ungesaini.

“Mimi nawakilisha wananchi wapigakura wa Musoma Vijijini, wao ndiyo walionichagua, nina wajibu wa kuwatumikia na kuhakikisha wanasaidiwa na Serikali yao ikiwa ni pamoja na kulinda rasilimali za nchi.”

Kuwa Mbunge wa Maisha

Katika hatua nyingine, Mkono amesema kwamba wale wanaonyemelea kuwa wabunge wa Musoma Vijijini, hawapaswi kumwandama kutokana na ukweli kwamba mara kadhaa wananchi wamemtaka awe mbunge kwa muda atakaopenda.

Amesema si yeye aliyeibua hoja ya kuwa ‘mbunge wa maisha’ katika jimbo hilo, bali ni wananchi wanaofurahishwa na uwajibikaji wake katika kushirikiana nao kujiletea maendeleo.

“Wananchi wenyewe wamekuwa wakisema ‘Mkono uwe mbunge wa maisha’, sasa unatarajia mimi nitasemaje? Kama wanaona ninafaa hayo ni mawazo yao.

“Lakini hata kama nikisema sina mpango wa kung’atuka kuna kosa gani? Ubunge hauna ukomo. Katiba yetu ya sasa haisemi kuna ukomo kwenye ubunge isipokuwa kwenye urais. Kwa hiyo hata kama nikisema nitakuwa kama Mugabe (Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe), hakuna kosa kikatiba kwa sababu ubunge hauna ukomo,” amesema.

Mkono anasifika kwa kupeleka maendeleo makubwa jimboni mwake, kiasi cha kutajwa kuwa hakuna mbunge yeyote katika historia ya Tanzania aliyeweza kufanya mambo makubwa ya kimaendeleo jimboni kama yeye.

Amejenga shule nyingi za sekondari zenye hadhi ya kipekee, amejenga shule za sekondari za kata, amejenga shule za msingi nyingi, ameshiriki ujenzi wa barabara katika jimbo lote la Musoma Vijijini, ameshiriki ujenzi wa zahanati na vituo vya afya, amechimba visima na kuweka miradi mbalimbali ya kijamii.

Si hayo tu bali pia amesambaza kompyuta, madawati, vitabu na vifaa vya masomo katika shule mbalimbali ndani na nje ya jimbo hilo. Hatua hiyo imemfanya awe na maadui wengi hasa kutokana na msimamo wake wa kusimamia miradi yeye mwenyewe badala ya kutumia Halmashauri ya Musoma, ambayo ni miongoni mwa halmashauri zinazotuhumiwa kuwa na ‘mchwa’ unaotafuna fedha za umma.

Kwa sasa amejielekeza kwenye ujenzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Mwalimu Julius Nyerere kijijini Butiama. Anaendesha juhudi hizo kwa kushirikiana na Serikali na wafadhili mbalimbali wa ndani na nje ya nchi.

1177 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!