Serikali za Marekani na Uingereza zimetaka maelezo kutoka Serikali ya Tanzania juu ya madai kwamba

Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono (CCM) amelishwa sumu wakati akiwa kwenye safari ya kikazi jijini London, Uingereza.

Mmoja wa maofisa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, amethibitisha kuwa ni kweli mataifa hayo yametaka maelezo.

Nchi wafadhili, zikiwamo Marekani na Marekani zimezuia mabilioni ya fedha za misaada kwa Tanzania zikitaka kwanza zilidhishwe na juhudi za Serikali katika kuwakabili waliohusika kwenye ukwapuaji fedha katika akaunti ya Escrow.

“Hatujui tutatoa maelezo gani, lakini Uingereza inataka maelezo kwa sababu kama Mkono angefika London, ingekuwa kashifa; lakini pia kwa Marekani, Mkono amekuwa na uhusiano wa kikazi na kampuni na Serikali ya nchi hiyo,” amesema ofisa huyo.

Mkono ambaye kitaaluma ni mwanasheria, aliugua ghafla alipokuwa jijini London, akiwa mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala. Kamati hiyo ilikuwa na ziara ya mafunzo katika Bunge la Makabwela (House of Commons) la Uingereza.

Madaktari wake walisema alilishwa sumu iliyokuwa imekusudiwa kuharibu figo zake ndani ya saa 72.

Mkono amekunuliwa alisema: “Ilikuwa siku mbili tangu niwasili London, nilianguka wakati nikiwa ofisi za Bunge.

“Nilijisikia vibaya na kupoteza kumbukumbu kwa takriban saa sita. Ninachokumbuka ni kutokwa jasho jingi ghafla kabla sijaanguka na kupoteza fahamu.”

Akizungumza na JAMHURI nyumbani kwake Oysterbay, Mkono amesema alikuwa ameonywa mapema kuwa muda mfupi kabla hajasafiri kwenda London anapaswa awe mwangalifu, pia asifikie kwenye hoteli zilizokuwa zimeandaliwa kwa ajili ya kundi kutoka Tanzania.

“Nilionywa mapema na watu wa karibu yangu. Kuna rafiki yangu waziri alimtuma kijana akaniletea taarifa. Hata nikiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, niliendelea kupata taarifa; hivyo niliona nikifika London nifikie kwenye hoteli ambayo nimeizoea. Sikwenda kule tulikopangiwa,” amesema na kuongeza:

“Nilipokea meseji mbili kutoka kwa baadhi ya marafiki zangu wakinionya kuwa mwangalifu wakati wote. Nilikuwa nimeongozana na baadhi ya wabunge katika safari hiyo.”

Aidha, habari zinasema kuwa maofisa usalama wa Kikosi cha Upelelezi nchini Uingereza wameanza kulichunguza tukio hilo.

 

Mkono na sakata la Escrow

Miongoni mwa ujumbe aliotumiwa Mkono unamuonya juu ya kile kinachodaiwa kuwa ni mkakati wake wa ‘kuiangusha Serikali’ kutokana na kashfa inayovuma sasa ya wizi wa Sh bilioni zaidi ya 300 kutoka katika Akaunti ya Escrow. Mkoano anatajwa kama mmoja wa watu wanaolijua vema sakata hilo.

 

Alikuwa Mshauri Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Serikali dhidi ya Kampuni ya Kufua Umeme ya Independent Powere Tanzania Limited (IPTL). Amewahi kuziwakilisha kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Utatuzi wa Migogoro ya Kibiashara (ICSID) kabla ya mkataba wake kumalizika mwanzoni mwa mwaka huu, na TANESCO walikataa kusaini upya mkataba na Mkono.

Anatajwa kuwa nyuma ya kuvuja kwa kashfa ya Escrow kutokana na ukweli kwamba sakata lote tangu mwaka 2000 limekuwa mikononi mwake.

Julai mwaka huu, Waziri wa Nishati na Madini, Sospeter Muhongo alimtuhumu Mkono kutumia kashfa ya Escrow kumchafua, tuhuma ambazo Mkono anazikana.

Wiki chache baadaye, Spika alimtaka Mkono kueleza namna ambavyo aliishughulikia kesi ya IPTL na Standard Chartered Bank Hong Kong iliyokuwa imefunguliwa dhidi ya Tanesco na Serikali.

Mkono aliwasilisha taarifa kuhusu kuchotwa kwa Sh bilioni 207 kwenye akaunti ya Escrow ilhali kukiwa na kesi nyingine ikiendelea katika Mahakama ya Kimataifa.

1029 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!