Mkurugenzi: Wananchi Bukoba tulieni

*Asema ripoti ya CAG itatoa mwelekeo
*Pande zinazovutana zaandaa ‘bakora’

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba, Limbakisye Shimwela, amewaomba wakazi wa Manispaa hiyo kuwa watulivu na kusubiri majibu yatakayotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) baada ya ukaguzi maalum hivi karibuni.


Akizungumza na JAMHURI ofisini kwake mjini Bukoba mwishoni mwa wiki iliyopita, Shimwela alisema wananchi waondoe wasiwasi juu ya taarifa kuwa nyaraka zinaibwa au kuharibiwa, na akasema yeye atasimamia utekelezaji wa Ripoti ya CAG kwa mujibu wa sheria.

Madiwani wanane – Deusdedith Mutakyahwa (Nyanga), Robert Katunzi (Hamugembe), Dauda Karumuna (Ijuganyondo), Samuel Ntambala Luhangisa (Kitendaguro), Yusufu Ngaiza (Kashai), Richard Gasper (Miembeni), Alexanda Ngalinda-Naibu Meya (Buhembe) na Murungi Kichwabuta (Viti Maalum) – uongozi wa CCM Mkoa uliwafukuza uanachama, lakini Kamati Kuu ya CCM ikabatilisha uamuzi huo mwezi uliopita na kuagiza ufanyike ukaguzi maalum kwenye halmashauri kubainisha tuhuma dhidi ya Mstahiki Meya, Anatory Amani.

 

“Ni kweli kuna mgogoro kwenye halmashauri yetu ya Manispaa ya Bukoba. Kumekuwa na mazungumzo mengi na vikao vingi, hasa hasa kwenye chama, wamezungumza. Hapa mimi kama Mkurugenzi nilicho nacho ni barua ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba itakuja special audit (ukaguzi maalum).

 

“[Ukaguzi] utaangalia mambo mengi pamoja na hizo tuhuma. Waziri Mkuu ameagiza katika barua hiyo kuwa wakikagua taarifa hiyo itolewe kwenye Baraza la Madiwani na nitafanya hivyo.

“Baada ya ripoti nitaanzia hapo kufanya kazi. Mheshimiwa Waziri Mkuu ameagiza ifanyike haraka. Hizi statements (kauli) huyu atoe hivi, huyu atoe vile tunayumbisha wananchi. Ndiyo maana mimi nimeamua kukaa kimya.

 

“Tukiendelea hivi huyu anasema hivi, huyu anasema vile wananchi wanabaki wanayumba, tunadumaza maendeleo. Naamini ukaguzi wa aina yoyote utashauri kuwa hili lifanyike hivi, hili liende hivi, nasi tutatekeleza kwa mujibu wa maelekezo. Hapo ndipo pa kuanzia.

 

“Naomba watendaji waendelee kufanya kazi kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyopo. Kuna mambo ya kiutendaji ambayo hayasubiri maamuzi ya Baraza, hayo tuendelee nayo. Watendaji wasiyumbe kuingia kwenye siasa, watende kwa mujibu wa sheria na wananchi watuamini kuwa tutasimamia sheria,” amesema Shimwela.

 

Kuhusu tuhuma za nyaraka kuibwa kwa nia ya kukwepa mkono wa dola, alisema: “Meya ameondoka hapa tangu tarehe 24/8/2013. Sasa amekesha wapi? Hakuna hicho kitu cha kuharibu nyaraka. Hata uthibitisho muhimu ni Meya, kwamba yuko Dar es Salaam leo ni tarehe 10/9/2013 wakati fulani ni vizuri kuthibitisha. Hata mimi kama sehemu ya jamii, naviamini mno vyombo vya habari na navipenda. Hakuna kitu kama hicho. Wananchi wasijengewe hofu ya bure.”

 

Shimwela ameiambia JAMHURI kuwa kwa kuwa yeye ni mgeni katika Manispaa ya Bukoba na mgogoro huu ameukuta, hataki kujihusisha na upande wowote katika mgogoro huo na anasubiri baada ya ukaguzi wa CAG, utakaofanyika hivi karibuni aanze rasmi kazi ya kuijenga upya Bukoba kwani mgogoro umekwamisha maendeleo.

 

Wakati Mkurugenzi akitoa kauli hiyo, aliyekuwa Meya wa Mji wa Bukoba hadi mwaka 2010 ambaye sasa ni Diwani wa Kitendaguro, Samuel Ntambala Luhangisa, ameiambia JAMHURI kuwa watumishi wa halmashauri wanashiriki mchezo mchafu wa kuiba nyaraka. Luhangisa ametaja majina ya watumishi wanaotuhumiwa kuiba nyaraka na kuziteketeza, ila kwa sababu za kisheria kwa sasa majina hayo tunayahifadhi.

 

“Baada ya Kamati Kuu kuturudisha, nilipigiwa simu saa 8 usiku kuwa ofisi ya Manispaa ya Bukoba wapo kazini usiku. Niliamka nikaenda na nilikuta maofisa kutoka ofisi ya Ardhi, wamo ofisini hadi saa 10 usiku. Jana [Ijumaa Septemba 6], tulimpeleka mama Kahama aende kuuliza mambo ya faili lake lililopotezwa.

 

“Tulipofika tukakuta watendaji wote walikuwa wana kikao. Madereva wa Council, walikuwapo pale katika mazingira yale. Wakuu wa maidara, cashier [jina linahifadhiwa] ametafuta vitenge, amefunga general receipt (stakabadhi za malipo) na ‘mafaili’ mbele yao wote, amefunga amejitwisha amekwenda kutupa.

 

“Aliondoka na pikipiki na hakuna aliyeshituka… Watu wameniambia, Amani [Meya wa sasa] anaposema ‘nimekaguliwa na Tume tatu’, sasa ana mpango wa kuhakikisha anasafisha ofisi zile. Wanakutana mle wanafanya nini usiku?

 

“Vitabu hivyo anavitoaje hata kama kingelikuwa kimoja? Kilichosikitisha mke wangu na mama Kahama walimuona dereva (jina linahifadhiwa) anatupa mafaili ya ardhi na wametupa mafaili yote. Sijaona popote duniani mtu anatuhumiwa anabaki ofisini. Maofisa ardhi, wamo ofisini usiku, ofisini muda wote wanahaha,” alisema Luhangisa.

 

Kuhusu kufukuzwa kwao udiwani, Luhangisa kwanza anaishukuru Kamati Kuu ya CCM kwa kuwarejeshea uanachama, lakini anaeleza hali ilivyokuwa: “Bila kuitwa, bila kushirikishwa, tulipewa onyo. Kabla hatujalitumikia tukapewa barua ya kutufukuza, na kabla barua hatujazipata tukatangazwa kuwa tumefukuzwa, na kesho yake tukapata barua ndefu ya Katibu wa Mkoa [Everine Mushi], akimwandikia Mkurugenzi kuwa sisi si madiwani tena.

 

“Watu wanasema Katibu wa Mkoa ameukataa uamuzi wa Kamati Kuu, kwani hadi leo [Septemba 7] hajatuandikia barua za kuturejeshea uanachama, hata kutoa maelezo kama ameambiwa kumwandikia Mkurugenzi kuwa kwa barua yangu hii naifuta ile barua [ya kutengua kuwafukuza udiwani] angetueleza kitu chochote katika chama. Jana [Septemba 6] niliitwa katika Kamati ya Chama ya Kata, nimekwenda kumuuliza Katibu wa Chama wa Kata yangu, nikamuuliza tunakuja katika chama kwa njia gani?”

 

Hata hivyo, Jumanne ya Septemba 10 madiwani hao wanane waliokuwa wamefukuzwa uanachama walikabidhiwa rasmi barua za kurejeshewa uanachama, ingawa wanasema barua ya awali iliandikwa na Katibu wa CCM wa Mkoa, Mushi, lakini hii ya kutengua ya awali imeandikwa na Katibu wa CCM wa Wilaya, Janeth Kayanda.

 

Luhagisa, aliyekuwa mmoja wa wakuu wa mikoa tisa wa kwanza wazalendo baada ya Tanganyika kupata Uhuru, ameiambia JAMHURI: “Katika maisha yangu sitasahau. Nitaomba viongozi wa dini waniongoze, wanisaidie katika suala la kusamehe Bukoba, mimi, CCM si baba yangu, si mama yangu. Hata nikisamehewa namna gani, nataka kuelezwa Katibu wa CCM Mkoa amekataa kufuta barua baada ya kuelekezwa na makao makuu?

 

“Sasa niende kwenye chama changu? Tangu mwaka 1955 ni mwanachama wa TANU na baadaye CCM. Kadi yangu ni ya 1500 Tanzania nzima. Wanachama walionitangulia ni 1499. Ndiyo, kadi yangu niliyoipata akiwapo Mwalimu [Julius Nyerere] na Oscar Kambona, halafu huyu anatuandikia barua?

 

“Sasa ndiyo nimelala baada ya Kamati Kuu kutoa tamko la kuturejesha. Hata marafiki zangu Denmark nimepata simu zaidi ya 50. Tukianza kudhalilishwa hivi, hivi, hivi kweli! [anashika kichwa]. Ndiyo maana kama wanatutoa watutoe. Sisi tunapigania watu, ndiyo wanatutoa kweli?”

 

Diwani wa Kata ya Kahororo (CCM), Chifu Adronikus Karumuna, aliiambia JAMHURI kuwa Luhangisa bado ana hasira za kushindwa udiwani ndiyo maana anaweza kutoa tuhuma nzito kama hizo.

 

Amesema ameusikia mpango wa madiwani wanaopingana na Meya Amani, wakitamba kuwa baada ya taarifa ya CAG watamng’oa Meya Amani mara moja, ila hilo halitakaa litokee. Chifu Karumuna anasema:

 

“Leo wanazungumza CAG anakuja, mimi siogopi CAG hata chembe. Mwaka 2013 tumepewa hati safi. Katika Kanda ya Ziwa Bukoba ni ya pili kupata hati safi. CAG anakuja kufanya uchunguzi, anakuja kuangalia masuala ya fedha. Hatuna Meya Mtendaji. Meya ili asaini ni baada ya Mkurugenzi kuwa amesaini na Mwanasheria [wa Manispaa] kama kuna kosa ni kosa la manejimenti.

 

“CAG akifanya otherwise [vinginevyo], then [hapo] tutajiuliza. Si alitusifia juzi hapa Julai kwa kutupa hati safi? Tunaamini CAG haji kumkagua Meya, anakuja kuikagua halmashauri. Sijui kama Nape anatumwa na nani kusema baada ya ukaguzi taarifa itawasilishwa kwenye Council (Baraza).

 

“CAG anapomaliza kukagua anapeleka kwa Waziri Mkuu. Watu [madiwani] wanane waliokuwa wamefukuzwa bado wana hasira zao. Nape asitufanye wajinga. Kwamba CAG akikagua ripoti akaiwasilisha kwenye council na wakitaka kupiga kura wapige, nasema patachimbika. Watapiga kura pale kwa utaratibu upi?

 

“Labda wawepo polisi wengi pale nje. Tutakwenda kumsikiliza CAG, kwa kufuata utaratibu wafuate taratibu za kumwondoa Meya wakipenda. Kuna watu wamemwambia Meya wazi kuwa ‘Jamani mimi Meya nakupenda, lakini nimepewa milioni 25.’ Mwisho Hamis [Kagasheki] ametufikisha hatua mbaya. Kamati ya Siasa ya Mkoa, niliwaeleza hivi hivi na Hamis akiwapo. Kamati ya Kandoro niliwaeleza, leo CAG anakuja kufanya nini?

 

“Hamis ametamka mbele ya Rais na mbele ya Makamu Mwenyekiti kuwa hawezi kufanya kazi na Meya. Sijui kwa nini Chama kinamlinda hivyo Kagasheki? Watu wanapitisha vitu kisha wanavipinga?”

 

Wakati Chifu Karumuna akitema cheche hizo, Diwani wa Nyanga, Deusdedith Mutakyahwa, anasema Meya Amani amevuruga Halmashauri ya Bukoba. Mutakyahwa anasema tatizo si ukweli kuwa mipango hii ilipata kupitishwa na madiwani, bali utekelezaji wake.

 

Anasema yanayokubaliwa kwenye vikao, Meya na baadhi ya watendaji huyabadilisha na kuchonga kumbukumbu za vikao kwa kubandika majina ya madiwani waliohudhuria, huku wakighushi saini za madiwani.

 

“Minutes (kumbukumbu za vikao) zinaposomwa, unashangaa mliyokubaliana kwenye kikao ni tofauti na yanayoletwa kwa utekelezaji. Meya anabadilisha mlichozungumza, ukiuliza anasema ndiyo hivyo, anakopa fedha bila kushirikisha madiwani, miradi ya maana anaisitisha, anahamisha miradi kutoka eneo moja kwenda jingine – kwa kweli hali ni mbaya,” anasema Mutakyahwa.

 

Miradi inayolalamikiwa ni ya ujenzi wa soko la kisasa Bukoba, stendi ya mabasi Kyakailabwa, mradi wa maji Kagondo, ujenzi wa barabara ya lami Kagondo, Uwanja wa Mpira wa Shule ya Msingi Kiteyagwa, ubinafsishaji wa eneo la kuoshea magari (car wash), mkopo wa sh milioni 200, riba ya milioni 90, mkopo wa sh bilioni 2.9, mradi wa viwanja 5,000, ujenzi wa dampo Nyanga, umeme Nyanga, tuhuma za viongozi kusambaza rushwa, udini na mengine mingi ambayo yote imezungumziwa kwa kina.

 

Makala haya yamewezeshwa na Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF) unaolenga kuimarisha weledi katika sekta ya habari nchini.

 

Wiki ijayo, tutakuletea sehemu ya pili ya makala haya, itakayokuwa na mahojiano kati ya madiwani sita, mameneja wa miradi inayolalamikiwa, viongozi wa CCM ngazi mbalimbali na madiwani wa pande zote wanaopingana.

 

Hata hivyo, hadi naandika makala haya nilikuwa sijafanikiwa kuzungumza na Mbunge wa Bukoba Mjini, Khamis Kagasheki, ambaye amenieleza kuwa ametingwa na kazi na akaahidi kuwa tungezungumza akiwa Dar es Salaam, lakini pia Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba, Dk. Anatory Amani, nilikuwa sijazungumza naye pia. Dk. Amani aliahidi kuzungumza na JAMHURI baada ya Jumamosi. Wakati mwandishi yuko Bukoba, kumbe Dk. Amani alikuwa Dar es Salaam na mwandishi aliporejea Dar es Salaam, Dk. Amani akamwambia kuwa amesafiri kwenda Bukoba.

 

Kutokana na hali hiyo, ikiwa Kagasheki na Amani hawatapatikana, makala yajayo yatawasilisha yaliyozungumzwa na watu mbalimbali wasiopungua 26 waliohojiwa kwa nyakati tofauti. Zipo tuhuma kwa pande zote mbili, hivyo ingependeza viongozi hawa wakapatikana kuzungumzia tuhuma dhidi yao. Juhudi za kuwatafuta viongozi hawa zinaendelea.