Mkutano Mkuu wa Wekundu wa Msimbazi, Simba Sports Club ya Dar es Salaam unaotarajiwa kufanyika Julai 15, mwaka huu, jijini ndiyo utakaoamua iwapo Mwenyekiti wa timu hiyo, Ismael Aden Rage, ataendelea kushika wadhifa huo au la.

Chanzo cha habari cha kuaminika kutoka katika kwa Wekundu hao wa Msimbazi kimeiambia  JAMHURI kuwa wanachama klabu hiyo, wamepania kumuondoa madarakani Rage kutokana na kushindwa kufanya vizuri katika michuano iliyopita.

 

“Tanamsubiri Rage katika Mkutano Mkuu wa atujibu maswali yetu ya msingi  kuhusu timu yetu, akishindwa aondoke; hatuwezi kuwa na mwenyekiti ambaye hakai na timu  na muda wote yuko kwenye siasa, sasa tunamtaka achague moja kuendelea na siasa au mpira.

 

“Tumekosa Kombe na tumeshindwa kujenga uwanja kwa sababu yake hili hatukubali, mapinduzi yaliyopita yalishindikana sasa hapa lazima katika mkutano huu atueleze anabaki na soka au siasa, kuna watu wanaweza kuiongoza Simba kama akina Hans Hope… awaachie waongoze timu kuliko kuin’gang’ania wakati anaharibu”.

 

Chanzo hicho pia kimesema kuwa wanachama hao wamejipanga vizuri kuhakikisha kuwa wanautumia vizuri mkutano huo kwa maslahi na manufaa ya Simba.

 

Katika mkutano huo, wanachama hao wamepanga kuhoji kuhusu fedha  walizochanga ili kununua kiwanja cha kujenga uwanja eneo la Bunju nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

 

“Wanachama walichanga, Sh 20,000 kwa  ajili ya ununuzi wa uwanja katika eneo la Bunju, wameuliza maswali kuhusu hati ya uwanja huo, lakini hakuna majibu wala mtu aliyepata kuiona hati hiyo, wanachama wana hasira na hiyo hati wanataka kujua hatima ya fedha zao,” kilisema chanzo hicho.

 

Pia wanataka kujua hatima ya fedha za Emmanuel Okwi, nyota na mtupia mabao wa Simba aliyeuzwa kwa timu ya Etoile du Sahel ya Tunisia, kwani hawakubaliani na majibu yanayotolewa na uongozi huo.

 

“Tutauliza kuwa hivi Rage na wenzake wakati wanamuuza Okwi hakujua kuwa timu hiyo haina fedha? Leo tunasoma katika magazeti kuwa tutapata fedha hizo mwezi wa tisa; hizi ni danadana; atatueleza fedha hizo ziko ziliko,” kimesema.

 

Chanzo hicho kilisema moja ya mambo mengine ni kuhusu usajili wa mchezaji Mrisho Ngassa. Wanachama hao wanahoji iweje leo uongozi huo umsajili Ngassa wakati wakijua ana mapenzi makubwa na watani wao Yanga.

 

Hata hivyo, Rage hakupatika kuzungumzia suala hiyo kwa kuwa simu yake ya mkononi ilipopigwa iliita bila kupokewa.

By Jamhuri