Misitu ya Asili na Maendeleo ya Jamii Tanzania (4)

Toleo lililopita, Dk. Kilahama alieleza umuhimu wa viongozi wa vijiji na jamii kuhakikisha wanapata manufaa kutokana na misitu, hasa ya asili. Akasisitiza umuhimu wa uongozi bora na imara katika vijiji na vikundi vya kijamii. Endelea.

Uzoefu nilionao unaonesha kuwa vijiji vyenye uongozi usiokuwa makini na unaolegalega maendeleo yake ni hafifu sana, ilhali vikiwa na fursa za kutosha ikiwamo ardhi yenye rutuba na misitu ya asili.

 

Haifai kuendelea kuona rasilimali za asili katika vijiji zinanufaisha watu kutoka nje wakati wakazi wa sehemu husika wanazubaa tu na viongozi wao yaani Mwenyekiti na Halmashauri ya Kijiji wakiwapo. Mathalani, Wilaya ya Handeni mkoani Tanga imejaaliwa kuwa na hazina kubwa ya misitu aina ya miombo (miombo woodland).

 

Unakuta sehemu kubwa ya kijiji imefunikwa na misitu, tena yenye aina za miti ya thamani sana kama mikarambati, mihuhu, mipangapanga, na mingineyo, lakini wananchi ni masikini.

 

Wanatokea wapuuzi wachache wanaenda kijijini na kuonana na uongozi wa kijiji na kwa lugha laini ya kuwekeza katika kilimo, tena kwa kutumia maneno kama kuendeleza taifa letu kupitia sera ya Kilimo Kwanza; na kwa kuwa vijiji vina ardhi kubwa na kupitia Sheria ya Ardhi ya Kijiji ya mwaka 1999 inayoruhusu kijiji kumpatia mkulima ardhi isiyozidi ekari 50, uongozi unakubali kutoa sehemu ya ardhi ya kijiji kwa wanaohitaji bila ya kujali juu ya ardhi hiyo kuna kitu gani.

 

Hivyo, kama ni watu 10 wanapewa ekari 500 au hekta 200 na wengine wanapewa kwa makubaliano kuwa wataboresha huduma za kijamii katika kijiji husika kwa mfano kujenga shule, kuboresha shughuli za afya au upatikanaji wa maji au kuimarisha miundombinu kama barabara.

 

Eneo la eka 500 (hekta 200) na kwa mtazamo wa kawaida na kwa eneo kama hilo kulitoa kwa watu 10 linaonekana si kubwa sana, lakini kama limesheni miti ya asili kwa wale wanaopewa wanafahamu fika kuwa hapo (wao wanaopewa eneo) wamelala maskini na kuamka matajiri, maana wanapata mali bila ya kuitolea jasho.

 

Hivyo wanachekelea mioyoni mwao na pengine kusema kimyakimya “wajinga ndiyo waliwao”. Nimeshuhudia kwamba wanapopewa kimaandishi wanachokifanya cha kwanza ni kuingiza mashine za moto (power saws) na misumeno na kuanza kukata miti tena ile yenye thamani ya mbao au nguzo na kuichakata mbao na kuuza na kujipatia fedha za harakaharaka hata bila kulipa ushuru wowote kijijini, Halmashauri ya Wilaya na kwa Serikali Kuu.

 

Wakiulizwa mbona mnakata miti bila kuwa na kibali kulingana na Sharia ya Misitu na Kanuni zake, jibu likawa sisi hapa “tunasafisha sehemu ya shamba letu au kwa maneno mengine tunaandaa sehemu ya kulima msimu ujao”. Wanapoulizwa nani amewaruhusu wafanye hivyo? Jibu linakuwa, “tumepewa eneo hili na Serikali ya Kijiji”. Tena wanakuwa na uthibitisho wa makaratasi ya makubaliano ya kuanzisha kilimo katika sehemu husika.

 

Kwa upande mwingine, unapohoji uongozi wa kijiji (mwenyekiti na timu yake) je, mlipotoa eneo hilo kwa wageni ili waanzishe mashamba ninyi hamkuona kuwa eneo hilo limesheheni miti ambayo ni rasilimali muhimu kwa maendeleo ya kijiji chenu? Kwa nini hamkuivuna kwanza ninyi wenyewe kama kijiji mkaitumia rasilimali hiyo kwa faida ya kijiji halafu ndipo mgawe maeneo kwa wanaotaka kulima?

 

Hakuna wanachojibu kinachoashiria kwamba wanafahamu fika nini faida ya uamuzi wao kwa maendeleo ya kijiji chao, isipokuwa wanabaki wamekuangalia tu! Kinachosikitisha zaidi ni kuona wale walioomba kupewa eneo la kulima wanapokata miti wakapata mbao na miti mingine wakaitumia kutengeneza mkaa, bidhaa ambazo wakiziuza wanapata fedha na hatimaye kuondoka bila ya kulima wakiacha wakijiji wakiwa wameduwaa.

 

Katika sehemu nyingine nchini, kwa mfano, katika Wilaya ya Kilwa, wawekezaji kutoka nje ya nchi walipewa ardhi kwa madhumuni ya kuotesha mibono (jatropha carcus) kwa ajili ya kuzalisha nishati inayotokana na mimea (biofuels), ili kuwezesha magari na mitambo kutumia nishati hiyo kama njia mojawapo ya kupunguza uzalishaji wa gesiukaa (CO2) ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa katika mabadiliko ya tabianchi.

 

Vilevile wanapotafuta ardhi ya kuwekeza wanatumia lugha nzuri ya kuvutia kwamba licha ya kuwekeza, wataboresha upatikanaji wa huduma za kijamii hivyo kuvifanya vijiji kuhamasika na kutoa sehemu ya ardhi yao kwa wawekezaji kwa kuelewa kuwa watanufaika na kuondokana na umaskini.

 

Baada ya kupata hekta 80,000 kutoka vijiji husika, kampuni ilishaona kuwa ardhi wanayopewa imefunikwa na misitu yenye miti ya thamani. Hivyo walichofanya cha kwanza baada ya kupewa na kuwa na haki ya kutumia ardhi hiyo, ni kuingiza mashine za kuchakata magogo kupata mbao. Hivyo wakaanzisha kiwanda cha mbao (sawmill) tena kwa kutohusisha Wizara ya Maliasili na Utalii na kuanza biashara ya mbao.

 

Wizara ilikuja kupata habari na kuchukua hatua za kuzuia kuendelea kukata miti bila ya kulipa ushuru wa Serikali wakati kampuni husika imeishanufaika vya kutosha. Sehemu nyingine nchini kampuni za nje zinaomba kupewa ardhi kwa nia ya kupanda miti ili itumike kunyonya gesiukaa kutoka angani (carbon sequestration) na kuihifadhi kama sehemu ya mti.

Kampuni huweza kufanya biashara ya gesiukaa (carbon trading) kadri miti inavyozidi kukua na kuviacha vijiji vikiambulia sehemu ndogo tu ya mapato husika. Vijiji na pengine watu binafsi katika sehemu mbalimbali nchini wanatoa kirahisi ardhi yao kwa wawekezaji kutokana na sababu kubwa mbili:

(i)  Kwanza, kutokuwa na uelewa na upeo mzuri wa kuiona ardhi na rasilimali misitu iliyo juu yake, kama ni nguzo muhimu na hatimaye kuweza kutumia rasilimali hizo za asili kujiletea maendeleo endelevu. Kwa bahati mbaya ardhi na misitu ya asili vinaonekana kuwa ni vitu vipo-vipo tu na watu wako tayari kutumia wapendavyo. Ukosefu wa elimu ya kutosha unawafanya Watanzania vijijini kutothamini sana ardhi na misitu ya asili, wakati ni rasilimali muhimu kwa maendeleo yao iwapo wataitumia kwa umakini sana. Vilevile, wataalamu hatujaweza kufanya kazi yetu ipasavyo ikiwa ni pamoja na kuwaelimisha juu ya umuhimu wa kuwapo rasilimali hizo na faida zake katika maisha yetu ya kila siku na isitoshe kuweza kuchukua hatua sahihi kuthamini na kutumia ardhi na misitu kwa faida yao;

(ii)   Wawekezaji kutoka nje wakijua kuwa rasilimali zilizo muhimu kwa maendeleo ya vijiji ni pamoja na ardhi na misitu ya asili, na kwa kutambua kuwa wengi vijijini ni maskini na wenye uelewa mdogo; wanatumia mwanya huo kupata faida ya haraka kwa kutumia rasilimali zilizo vijijini badala ya kuwasaidia wanavijiji na jamii kwa jumla na kuwajengea uwezo imara na hivyo kuwawezesha kutumia rasilimali hizo kuleta maendeleo endelevu vijiji. Kama wangelifanya hivyo, wawekezaji vijijini wangekuwa wamechangia kwa kiasi fulani kupunguza changamoto zilizopo na kiwango cha umasikini vijijini.

 

Itaendelea

Mwandishi wa makala haya, Dk. Felician Kilahama, ni Mwenyekiti wa Kamati ya Misitu ya Dunia, yaani Committee on Forestry-COFO iliyo chini ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kilimo na Chakula (FAO). Ni Mkurugenzi Mstaafu wa Idara ya Misitu na Nyuki katika Wizara ya Maliasili na Utalii. Alistaafu Desemba 2012. Anapatikana kwa simu na. HYPERLINK “tel:0756%20007%20400”0756 007 400.

 

By Jamhuri