*Asema Chadema ina baraka za Mwalimu Nyerere

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetamba kwamba nguvu yake haitamalizwa na ziara za viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mikoani, katika kipindi hiki ambacho Watanzania wengi wanahitaji mabadiliko.

Kwamba wakati viongozi wa CCM wamezinduka sasa kufanya ziara mikoani, chenyewe (Chadema) viongozi wake wanaendelea kuongeza kasi ya kutumia operesheni zake kueneza sera mbadala kwa matumaini mapya ya Watanzania.

 

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika, ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo katika mazungumzo na JAMHURI jijini Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki.

 

Mnyika alikuwa akijibu swali la mwandishi wa habari hizi aliyetaka kujua Chadema kimejipangaje kukabili nguvu ya kisiasa ya Sekretarieti ya CCM inayozuru mikoa mbalimbali kutangaza maazimio ya mkutano wake mkuu uliomalizika hivi karibuni mjini Dodoma na kuhamasisha uhai wa chama hicho tawala kwa wananchi.

 

“Hii si mara ya kwanza kwa Sekretarieti ya CCM kudai kuwa ziara zao zitaimaliza Chadema… walijaribu wakashindwa na kuishia njiani, wakajaribu kujivua gamba nako wakashindwa, hii ya Kinana (Abdulrahman – Katibu Mkuu wa CCM) nayo itashindwa.

 

“Chadema iko kwenye nyoyo za wananchi, haiwezi kuondoka kwa propaganda na kauli hewa za CCM, Chadema inalindwa na kuendelezwa na Watanzania kwa falsafa yake ya nguvu ya umma.

 

“CCM imeshindwa kushughulikia ufisadi na kero nyingine za wananchi, hivyo badala ya maisha bora bei za bidhaa na ugumu wa maisha unaongezeka. CCM iliyoshindwa kushughulikia matatizo ya Taifa haiwezi kuimaliza Chadema.

 

“Nguvu ya Chadema kumalizwa na CCM ni sawa na umma wa wapenda mabadiliko kumalizika, suala ambalo haliwezekani. Chadema inaendelea kuongeza nguvu kwa operesheni zake za kuleta uongozi bora, sera sahihi, mikakati makini na oganizesheni thabiti kwa maendeleo endelevu ya Taifa.

 

“Tutaendelea (Chadema) kwenda mijini na vijijini, wakati huo huo, tukieneza sera mbadala kwa matumaini mapya ya Watanzania,” amesema Mnyika na kuongeza:

 

“CCM ya kuwajali wanyonge, wakulima, wafanyakazi na watu maskini iliondoka na Mwalimu Nyerere, CCM ya leo haina uwezo wa kutekeleza kwa usahihi na kwa ukamilifu sera za Chadema ambazo tangu kuanzishwa kwake ilipongezwa na Nyerere kwa kuwa na sera bora, na tunaendelea kuziboresha kila wakati…”

 

Hata hivyo, Makamu Mwenyekiti wa Taifa wa CCM (Bara), Philip Mangula, amesema chama hicho tawala hakihitaji kudhoofisha nguvu ya Chadema, kauli inayodhihirisha kuwa CCM sasa kinafyata kwa Chadema katika kipindi hiki cha vyama vya siasa kujinyooshea mapito ya Uchaguzi Mkuu utaofanyika mwaka 2015.

 

“Tumetoka Mkutano Mkuu wa CCM, kuna maamuzi makubwa na mazito yaliyopitishwa, lazima yafikishwe kwa wanachama mikoani wayajue, sisi tuna wanachama milioni sita, hawajapungua, sanasana wanaongezeka, hao tunataka wajue kuna kazi imefanywa na wawakilishi wao kwenye Mkutano Mkuu (huo wa CCM wenye wajumbe zaidi ya 2,000).

 

“Hiyo ni hatua moja kubwa tu, wala hatuhitaji kudhoofisha nguvu ya yeyote, sisi tuna nia ya kuwaimarisha na kuwafanya wanachama wetu wajue yaliyojiri katika mkutano ule, hatuwezi kuwasema Chadema, wala upinzani, wala nani,” amesema Mangula.

 

Alipoulizwa msimamo wake kuhusu mvuto wa Chadema unaodhihirishwa na wananchi wengi kuhuduria mikutano ya chama hicho kikuu cha upinzani nchini ilikilinganishwa na wachache wanaohudhuria mikutano ya CCM, hususan katika kanda za Ziwa na Kaskazini mwa Tanzania, Mangula amesema:

 

“Mikutano siyo kigezo sahihi cha kukubalika (kwa chama cha siasa), matokeo ya uchaguzi ndiyo kigezo cha kujua heshima (ya chama) imepotea au haijapotea.”

 

Akizungumzia kashfa ya vitendo vya rushwa kuendekezwa katika uchaguzi wa viongozi wa CCM, Mangula amesema tatizo hilo sasa linashughulikiwa kwa nguvu kubwa, ikiwa ni pamoja na kuwavua madaraka watakaothibitika walitoa rushwa, kama ambavyo imekuwa ikisisitizwa na Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Rais Jakaya Kikwete.

 

 

 

1044 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!