*Yajipanua hadi mataifa ya Zambia, Uganda

*Watoto wa wafanyakazi wasomeshwa bure

*Watumishi wapewa vifaa ujenzi wa nyumba

*Ni mali ya Watanzania kwa asilimia mia moja

Oktoba 10, mwaka huu, wahariri kutoka vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini, walizuru viwanda vinavyomilikiwa na Kampuni ya Motisun Holdings Limited vilivyopo jijini Dar es Salaam.

Katika ziara hiyo, wahariri walijionea kazi nyingi, kubwa na za kujivunia kutoka katika viwanda vya kampuni hiyo vinavyomilikiwa kwa asilimia 100 na Watanzania wenyewe.

 

Si wananchi wengi wanaotambua mchango wa kampuni hiyo katika uchumi wa Taifa letu. Ni kwa sababu hiyo, JAMHURI imeona ni vema ikawaletea wasomaji historia ya kampuni pamoja na dhima yake kwa uchumi wa Taifa letu.

HISTORIA FUPI

Kampuni ya Motisun Holdings Limited ilianzishwa mwaka 1992 ikiwa ni kampuni mama inayomiliki kampuni mbalimbali hapa nchini na nje ya nchi zinazojihusisha na uzalishaji wa vifaa vya ujenzi, vinywaji baridi, hoteli, kampuni za ujenzi, uchimbaji madini, na kadhalika.

Ni kampuni inayomilikiwa kwa asilimia 100 na Watanzania ikiwa chini ya Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji, Subhash Patel.


Kwa upande wa Tanzania, kuna viwanda vya M. M. Integrated Steel Mills Limited, Motisun Industries Ltd, PNP Industries Ltd, Kiboko Precoated Sheets Ltd, Kiboko Cold Rolling Ltd, Kiboko Continuous  Galvanising Plant, Kiboko Paints, Kiboko Tanks, na Sayona Drinks. Taratibu za ujenzi wa viwanda vya saruji na juisi za matunda unaendelea Bagamoyo mkoani Pwani.


Kwa upande wa hoteli,  kampuni inamiliki White Sands Hotel Ltd, Sea Cliff Hotel Zanzibar, Sea Cliff Court Ltd na Best Bite. Mchakato unaendelea wa kufungua hoteli nyingine katika mbuga za wanyamapori Ngorongoro na Makinde Ruaha.

SEKTA YA VIWANDA

Kampuni ya MM Integrated Steel Mills Limited ni ya mwanzo kabisa kupewa kibali na Kituo cha Uwekezaji wakati huo kikijulikana kama Investment Promotion Centre (IPC); na sasa kinaitwa Tanzania Investment Centre (TIC). Kilipewa kibali cha ujenzi wa kiwanda cha chuma mwaka 1992. Kiwanda hiki cha MM Integrated Steel Mills Limited kinamilikiwa asilimia 100 na Watanzania.

Kilianza uzalishaji Mei 1995 kikiwa ni kiwanda binafsi cha kwanza chenye uwezo wa kuyeyusha chuma chakavu na kutengeneza chuma (billet) na kutumia billet kutengeneza bidhaa za chuma kama vile nondo, angle iron, flat bars; na kadhalika. Uwezo wa uzalishaji wa kiwanda wakati huo ulikuwa tani 10,000 za bidhaa za chuma kwa mwaka.

 

Katika kipindi cha takribani miaka 17 tangu kuanza, kumefanyika upanuzi wa shughuli za uzalishaji kama ifuatavyo: Kuongeza uwezo wa kuyeyusha chuma chakavu (melting capacity) na utengenezaji wa bidhaa ya chuma (rolling capacity); kupanua wigo (diversity) wa uzalishaji wa bidhaa itokanayo na chuma kama vile mabomba, waya, tubu, mabati, na kadhalika; uwezo wa kuongeza thamani katika malighafi na bidhaa (galvanization plant, picking cold rolling plant).

KAMPUNI YAWEKEZA UGHAIBUNI

Licha uwekezaji wa ndani ya nchi katika sekta hiyo ya viwanda iliyoonesha mafanikio, kampuni imeweza kuvuka mipaka ya Tanzania na kwenda kuwekeza nje.

M.M. Integrated Steel Mills (Zambia) Limited:

Soko la bidhaa za Motisun limeongezeka katika nchi jirani kutokana na ubora wa bidhaa unaokidhi viwango vya kimataifa. Kampuni iliamua kujenga kiwanda nchini Zambia na kufunguliwa Juni 7, 2011 na aliyekuwa Rais wa Zambia kwa wakati huo, Rupiah Banda. Kiwanda kina Cold Rolling Mill na Continuous Galvanizing line na colour coating. Upanuzi wa kiwanda hicho unaendelea.


Aidha, kampuni ya M. M. I. S. M pia imewekeza nchini Uganda – M.M. Integrated Steel Mills (Uganda) Limited. Ujenzi wa kiwanda hicho unaendelea.


“Tunatarajia kitafunguliwa rasmi kwa ajili ya kuanza uzalishaji baadaye mwaka huu (2012). Kiwanda hiki kitakuwa na Cold Rolling Plant Continuous Galvanizing line Colour Coating line pamoja na Tube Mill. Kutokana na uwekezaji huo tumeweza kuongeza ajira na pato kwa Taifa,” amesema Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa Motisun Holdings Limited, Aboubakary Mlawa.


Anasema ongezeko la ajira limekuwa la kutia moyo, kwani mwaka 1995 wafanyakazi walioajiriwa walikuwa 480, lakini idadi hiyo imeongezeka hadi kufikia wafanyakazi 800 mwaka huu; na wengine wakiwa ni wa  ajira ya kila siku. Kadhalika, kumekuwapo ongezeko la Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na kodi mbalimbali.

CHANGAMOTO

Tatizo la kupungua kwa chuma chakavu nchini. Hadi kufikia mwaka 2012 vipo viwanda vya chuma 21 nchini vyenye uwezo wa kuzalisha tani zaidi ya 200,000 za chuma kwa mwaka. Baadhi ya viwanda hivyo vinaongeza uwezo wao wa kuzalisha ili ufike tani 100,000 za chuma kwa mwaka. Hivyo, kati ya mwaka 2007 hadi 2012 mahitaji ya viwanda vya chuma ni tani kati ya 600,000 hadi 700,000 za billet (malighafi inayotumika kuzalisha bidhaa za chuma).


“Hii ni sawa na kuyeyusha tani 750,000 hadi 910,000 za chuma chakavu kwa mwaka. Chuma chakavu kilichopo nchini hakitatosha uwezo huo wa viwanda wa kuyeyusha chuma chakavu, kwani uwezo wa kuyeyusha nchini ni mdogo sana.


“Hali hiyo ya upungufu wa chuma chakavu, ndiyo iliyotoa msukumo kwa Serikali kuona sasa ni wakati mwafaka wa utekelezaji wa mradi wa Kasi Mpya huko wilayani Ludewa kwa ajili ya kuzalisha chuma ghafi,” anasema Mlawa.

MRADI WA KASI MPYA

Mradi wa kutengeneza chuma (sponge iron) kutokana na mawe ya chuma cha Liganga na makaa ya mawe Katewaka, utakuwa mbadala wa matumizi ya chuma chakavu nchini. Mradi huo unatekelezwa na kampuni ya Motisun kwa kushirikiana na Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC).

Vipengele vya mradi – awamu ya kwanza

Mradi huu utahusisha kuanzishwa kwa mitambo ya kuzalisha chuma ghafi kwa kiwango cha tani 330,000 kwa mwaka, zitakazowezesha uzalishaji wa tani 250,000 kwa mwaka za chuma (steel billets), kuanzishwa kwa Mgodi wa Chuma Maganga Matitu; Mgodi wa Makaa ya Mawe Katewaka; na mitambo ya kuzalisha umeme kwa kutumia gesi joto inayotoka kwenye mitambo ya kuzalisha chuma ghafi kwa kiwango megawatt 48.

Maendeleo ya mradi

“Mosi, Uchorongaji (Diamond Core Drilling):

Eneo la chuma, mashimo 70 yenye jumla ya mita 18,000 (kilomita 18) yamechorongwa. Eneo la makaa (Katewaka) mashimo 30 yenye jumla ya mita 4,547 (kilomita 4.5) yamechorongwa.

“Pili, Miundombinu: Kilometa 180 za barabara katika maeneo ya chuma Liganga-Mundindi na Katewaka-Amani ambako kiwanda cha chuma kitajegwa zimeshachongwa. Barabara hizo zimewezesha wananchi kufika sehemu ambazo hazikufikika na hivyo kuongeza shughuli za maendeleo.


“Tatu, wingi na ubora wa madini (chuma na makaa):

Kazi ya kutathmini wingi na ubora wa madini kwa kutumia wataalamu wa Kitanzania na shughuli hizo kuhakikiwa na wataalamu wa kampuni ya kimataifa ya PB Uingereza. Maabara zinazotambuliwa duniani za Uingereza na Afrika Kusini zimeshatoa ripoti ya ubora wa madini hayo.


“Nne, tathmini ya mali za wananchi katika maeneo ya madini chuma na mkaa, inakaribia kumalizika kwa ajili ya kulipa fidia.

 

“Tano, mpango wa awali wa uhamasishaji na uwezeshaji wa wananchi hasa wa Wilaya ya Ludewa, kutambua fursa na changamoto zitakazotokea kwa kuwapo kwa mradi huo Ludewa zinaendelea,” anasema Mlawa.

FAIDA ZA MRADI HUU

Mlawa anataja baadhi ya faida za mradi huo kuwa ni pamoja na kuongeza uwezo wa nchi kuzalisha malighafi inayotumiwa na viwanda vingine. Aina ya chuma cha sponge – kitakachozalishwa kitatumiwa na viwanda vingine vya chuma kama malighafi ya kutengeneza bidhaa nyingine za chuma.


Kuongeza uwezo wa nchi kuzalisha aina nyingi ya bidhaa ya chuma ambazo kwa sasa zinatoka nchi za nje. Hizi ni pamoja na Hot-Roll Coils, Cold Coils, Flat bars, na aina nyingine nyingi za chuma.


Kuongeza uwezo wa nchi kushiriki kikamilifu katika ushindani wa soko hasa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), na kadhalika.

 

Kuongeza pato la Taifa kutokana na kulipa kodi, kuuza nje ya nchi baadhi ya bidhaa zitakazozalishwa na mradi kama vile sponge iron na bidhaa nyingine za chuma, hivyo kuongeza fedha za kigeni kwa Taifa. Kuongeza kasi ya maendeleo katika vijiji, kata na wilaya ya Ludewa kwa ujumla.


Kupunguza umaskini kwani: Kutakuwa na nafasi 3,000 za ajira za moja kwa moja katika mradi huu. Nafasi zaidi ya 4,000 za ajira zitakazotokana na shughuli mbalimbali za mradi huo.

AFYA NA MAZINGIRA

Mlawa anasema katika kuboresha mazingira ya afya na usalama wa wafanyakazi na bidhaa za kampuni ya Motisun, mwaka 2007 kampuni ilianza mchakato wa mfumo wa mazingira, afya na usalama kwa kufuata taratibu za Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC) pamoja na taasisi ya kitaifa ya afya na usalama, yaani OSHA.


“Mwaka 2008 tulipiga hatua zaidi kwa kuanza mfumo wa mazingira, afya na usalama kwa kufuata viwango vya kimataifa, yaani ISO 14001:2004 na OHSAS 18001:2007.


“Februari 2011 jopo la wakaguzi wa kimataifa, baada ya ukaguzi wa kina, waliridhika kuwa kampuni zetu zote yaani viwanda na hoteli zimekidhi kwa kila hali vipengele vyote vya viwango hivyo vya kimataifa, na hivyo kuwa certified,” anasema.

HUDUMA KWA WAFANYAKAZI

“Kampuni zetu zimekuwa zikitoa huduma zifuatazo kwa wafanyakazi; chai na chakula wakati wa kazi; matibabu katika zahanati zilizopo ndani ya kiwanda, matibabu katika Hospitali ya Hindu Mandal na Hospitali ya Sino; kuchangia shughuli mbalimbali kwa vyama vyao (wafanyakazi) mfano, vyama vya kufa na kuzikana na vyama vya akiba na mikopo (SACCOS); bima ya wafanyakazi; vitendea kazi; usafiri – ambako hutoa nauli kwa wafanyakazi na wengine hutumia staff bus.


“Kuwalipia ada watoto wao wanaofaulu kuingia sekondari hadi elimu ya juu ambako wastani wa Sh milioni 200 hutumika kila mwaka; na motisha mbalimbali kama kuwapa wafanyakazi vifaa vya ujenzi na kadhalika,” anasema Mlawa.

HUDUMA ZA JAMII

Mlawa anasema Kampuni ya Motisun imekuwa ikichangia shughuli mbalimbali za maendeleo zikiwamo za ujenzi wa shule, zahanati, barabara na miradi mingine kwa nchi nzima. Wastani wa Sh bilioni moja hutumika kila mwaka kwa shughuli hizo.

 

“Pia tunachangia shughuli za kiserikali na kitaifa, tumetoa mafunzo ya elimu ya kupambana na majanga ya moto kwa shule zote za sekondari wilayani Bagamoyo pamoja na kutoa vifaa vya kuzima moto. Mpango kama huo pia utatekelezwa katika baadhi ya shule za Wilaya ya Kinondoni mwaka huu. Na pia huduma ya kupambana na kuzuia moto hutolewa kwa majirani zetu kupitia kikosi chetu cha zimamoto chenye vifaa vya kisasa na askari waliopata mafunzo,” anasema Mlawa.


By Jamhuri