Serikali imewasha moto wa aina yake katika Mji wa Tunduma baada ya kuwapa wiki moja wananchi waliojenga katika eneo la mpaka (no man’s land) kuhamisha mali na kuvunja nyumba zao kwa hiyari, JAMHURI linathibitisha.

Uamuzi wa Serikali umekuja wiki moja baada ya Gazeti la JAMHURI kuchapisha habari za kiuchunguzi kuonyesha kuwa kuna mapato zaidi ya Sh bilioni 100 zinapotea kwa mwaka katika mpaka wa Tunduma kwa njia ya magendo.

Gazeti la JAMHURI limefanya uchunguzi wa kina na kubaini kuwa sigara zinaingia nchini kutokea Zambia na bidhaa nyingine kama sukari, vipodozi na vinywaji vikali vinaingia nchini bila kulipiwa ushuru kupitia mpaka huu wa Tunduma.

Baada ya habari hizo kuchapishwa kwa vielelezo, ambapo mwandishi alinunua hadi sigara nchini Zambia kwa wastani wa Sh 14,000 kwa paketi 10, ikilinganishwa na Sh 23,500 kwa paketi 10 kwa bei inayouzwa hapa nchini, Serikali imezinduka.

Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Luteni Chiku Galawa wiki iliyopita ameamua kwenda Tunduma na kufurusha wafanyabiashara kutoka Zambia waliodai wanamiliki kihalali maeneo ndani ya Tanzania, huku akiwataka Watanzania waliojenga mpakani kuvunja nyumba zao mara moja na kufanyia biashara katika maeneo yaliyotengwa.

Joel Siame, Mfanyabiashara na Mzambia amefanya ubishi mkubwa akimweleza Mkuu wa Mkoa Galawa kuwa yeye ni mmiliki halali wa eneo lililopo Tanzania na amekuwa na mikutano kadhaa na viongozi wa mkoani hapo huku akisema anasubiri barua ya kuhalalisha umiliki wake.

“Sasa nasema hivi, wiki moja haya magari yote yaondolewe,” amesema RC Galawa wakati akimtaka mfanyabishara huyo kutoka Zambia kuondoa magari yake eneo la mpakani lisilostahili kuwa na raia mkaazi yeyote ndani ya mita 50 kila upande kutoka kwenye vigingi vya mpaka kwa mujibu wa sheria za kimataifa.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Songwe, Mathias Nyange amelazimika kutumia nguvu za dola kumwondoa mkutanoni Siame baada ya kuonekana kuwa yeye alikuwa akifanya ubishi bila kujali uhalisia kuwa sheria za kimataifa hazimruhusu yeyote kufanya biashara katika eneo la mpaka ndani ya mita 50 kila upande wa nchi.

“Hapa sio mahali pa kufanyia biasara. Lazima tuwambie na hili ndugu zangu halina mjadala. Ni wewe tu kujadiliana na akili yako harakaharaka na wewe mwenyewe, wala usijadiliane na mtu. Tambueni tu kwamba hapa tunachokifanya hatukosei. Tambueni viongozi wenu, ninyi hapa na wale kule ili wakawaonyeshe eneo mnalokwenda kufanyia biashara,” Galawa amewambia wananchi waliofurika katika mpaka wa Zambia na Tanzania kumsikiliza.

Awali Galawa aliliambia JAMHURI kuwa nyumba zipatazo 3,000 au zaidi zitavunjwa eneo la Tunduma kwa nia ya kusafisha mpaka na kuweka eneo la wazi ambalo ni mita 50 kila upande wa nchi kutoka eneo la kigingi kinachotenga mpaka.

Baadhi ya wananchi wameonyesha wasiwasi kuwa huenda uhamishaji huu unafanywa kisiasa, licha ya ukweli kubainika kwamba bidhaa nyingi za magendo zinavuka kutoka upande wa Zambia kuja Tanzania.

Stanley Jonas, Mkazi wa Tunduma amesema suala la mpaka wa Zambia na Tanzania halipaswi kuzisumbua mamlaka kwani Wazambia na Watanzania wamekuwa marafiki wa muda mrefu na kama ni suala la mpaka linafahamika hivyo hakutakuwapo usumbufu wowote waache hali iendelee kama ilivyo.

Raia wa Zambia Michael Siwiti, yeye amesema suala la uhusiano wa Tanzania na Zambia ni la muda mrefu na viongozi wa kiserikali wanapaswa kujiepusha na siasa kwani zinaweza kuathiri uhusiano wa nchi hizi mbili.

Akizungumza na JAMHURI, mwishoni mwa wiki Mkuu wa Mkoa Galawa, amelishukuru gazeti hili na kusema limeifumbua macho Serikali na akalipongeza kwa kazi ya uchunguzi liliyofanya kubaini biashara ya magendo katika mji wa Tunduma.

“Baadhi ya wafanyabiashara wanataka kugeuza suala hili kulifanya ni mapambano kati ya nchi na nchi na si yeye. Nimi naendelea kusisitiza kuwa tutaendelea kuwa ndugu, lakini watu lazima wafuate sheria na taratibu. Na undugu wetu utaendelea kubaki pale pale,” amesema RC Galawa.

Amesema mkoa wake umemwandikia barua Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene kumwomba aitishe mkutano wa pamoja kati ya Wizara ya Fedha na Mipango, Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Viwanda na Biashara na Mambo ya Ndani wakutane kujadili mpango mkakati bora wa kusafisha mpaka wa Tunduma, ambapo anaamini ndani ya mwezi huu watapata sehemu ya ufumbuzi.

Ameongeza kuwa ramani ya Mipango Miji inaelekea kukamilika na hivyo suala hili pamoja na ugumu wake ni lazima likamilishwe sasa kuepusha nchi kuendelea kuwa na mpaka unaoruhusu magendo na kuikosesha nchi mpato.

Waziri Simbachawene ameliambia JAMHURI kuwa anaunga mkono juhudi zinazofanywa na Mkuu wa Mkoa Galawa na akasema atakuwa tayari kuratibu kikao cha pamoja kwa nia ya kuhakikisha watu wote walioko kwenye mpaka kati ya Tunduma na Tanzania wanaondolewa kuacha wazi eneo la mita 50 kila upande.

Wiki mbili zilizopita, Gazeti la JAMHUR limeripoti taarifa za upotevu wa mabilioni kwa mapato ya serikali katika mpaka wa Tunduma kutokana na biashara ya magendo katika sigara, sukari, vinywaji na vipodozi, hali iliyoiamsha Serikali na kuchukua hatuzi hizo.

By Jamhuri