Jose+Mourinho+Real+Sociedad+v+Real+Madrid+NbI6HcXwrYCx copy copy

Licha ya kubezwa, hasa kwa kuondolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, Chelsea imeamua kuhamishia hasira zake kwenye Ligi Kuu England (EPL) ambako inaongoza kwenye msimamo.
  Kocha Mkuu wa timu hiyo, Jose Mourinho, amesema katu sasa hawatang'oka katika nafasi hiyo ya kinara katika msimamo na malengo sasa ni kushinda taji.
  Chelsea maarufu kama The Blues wametupwa nje katika michuano ya Ulaya na Paris St Germain (PSG) katika mchezo uliofanyika katikati ya wiki iliyopita. Inaongoza Ligi ya England kwa tofauti ya pointi tano na Manchester City inayofuatia.
“Sawa, tumetolewa Ulaya. Timu yangu bado ni nzuri na ndiyo ileile inayoendelea kuongoza Ligi ya England tangu siku ya kwanza. Ni wachezaji walewale walioshinda Kombe la Ligi na ndiyo hao hao mabingwa wa EPL,” anasema Mourinho, akibeza kauli za mshambuliaji wa PSG, Zlatan Ibrahimovic.
  Raia huyo wa Sweden alitolewa baada ya kumchezea visivyo kiungo wa kati wa Chelsea, Oscar, na akasema, “Ni ngumu kwa timu hii ya kitoto kushinda hata taji la England.”
  Ibra alitolewa nje ya uwanja dakika ya 31 baada ya kupewa kadi nyekundu kwa kumfanyia madhambi Oscar.

By Jamhuri