Majuma mawili yalilopita nilishiriki hafla ya kuchangisha pesa za hisani iliyofanyika Ojai, kwenye Jimbo la California nchini Marekani. Ni hafla inayoandaliwa kila mwaka na Global Resource Alliance, shirika lisilo la kiserikali linalosimamia utekelezaji wa miradi ya kusaidia jamii mkoani Mara.

Ojai ni mbali. Nimeanza safari Alhamisi na kufika Jumamosi. Kwa ndege, siyo kwa basi la Zuberi. Siyo rahisi kusafiri zaidi ya kilomita 19,000 na kwa zaidi ya siku mbili usitafakari umbali wa safari yako.

Siku ilipowadia nikasimama mbele ya hadhira ya watu wasiozidi 50 na nikazungumzia kazi ambayo ya michango ya pesa, pamoja na ya wengine ambao hawakuhudhuria pale, inavyosaidia kuendesha miradi kadhaa kwenye mkoa wa Mara.

Miradi hiyo ni pamoja na kutoa msaada wa elimu, huduma ya afya, na mahitaji muhimu kwa yatima zaidi ya mia moja katika ngazi mbalimbali za elimu.

Wenye kutoa pesa waliuliza maswali mengi na uendeshaji wa miradi hiyo, na maswali yalijibiwa kwa ukamilifu.

Mimi pia nilikuwa na maswali, lakini nilikosa wa kumuuliza kwa sababu majibu niliyaacha Tanzania. Kwanini nalazimika kusafiri umbali wote huu kuomba Wamarekani msaada wa kusaidia jamii ya Watanzania?  Watanzania wako wapi? Pesa yao wanachangia nini?

Sababu moja ya kwenda Ojai inaweza kuwa Wamarekani wanashika nafasi ya pili kama watu wenye kuongoza katika kutoa misaada kwa wenzao. Mtu anayehesabika hutoa misaada ni yule anayesadia mtu mwenye shida ambaye mtoa msaada hamfahamu, anayechangia pesa za hisani, au anayejitolea kufanya kazi bila malipo. Nafasi ya kwanza ulimwenguni inashikwa na raia wa Myanmar.

Kwenye orodha niliyoipitia, ambayo ni matokeo ya utafiti ya kampuni ya Gallup, Kenya inashika nafasi ya 12, Uganda ya 26, na Tanzania inashika nafasi ya 57 kwa matokeo ya utafiti wa mwaka 2016.

Ni rahisi kusema kuwa Wamarekani wana uwezo mkubwa wa fedha kuliko Watanzania, kwa hiyo ukweli kwamba pesa za hisani zipo nyingi zaidi nchini Marekani si suala la kushangaza.

Lakini hoja ya aina hiyo inapuuzia ukweli kwamba moyo wa kutoa au wa kujitolea hauna uhusiano wowote na utajiri. Moyo wa kujitolea ni uamuzi unaoongozwa na jinsi gani mtu mmoja amepima tatizo lililopo mbele yake na kuamua kuchukua hatua kupunguza tatizo hilo kwake au kwa jamii inayomzunguka.

Kila mara tunafikiwa na maombi ya kuwa miongoni mwa wale wanaochangia kumaliza matatizo kadha wa kadha. Na, hali inaporuhusu, kila mara tunafanya uamuzi wa kusaidia au kutosaidia.

Mara kwa mara napokea kadi ya kuchangia sherehe ya aina moja au nyingine, na tabia iliyojengeka miongoni mwetu ni kuwa asiyechangia sherehe hizo anajipambanua kama mtu ambaye hapendi kushirikiana na wanajamii wenzake.

Kwa hiyo baadhi ya Watanzania tunachangishana mamilioni ya pesa kwa madhumuni ya kuandaa sherehe kubwa na karamu za vyakula, vinywaji, na muziki kwa siku moja. Na kwa siku zilizosalia ndani ya mwaka tunaitisha vikao kujadili matatizo mbalimbali ambayo yanatukabili ndani ya jamii zetu.

Kwenye sensa ijayo ingefaa kuwauliza Watanzania wanachangia kiasi gani cha pesa kwenye sherehe kila mwaka ili tukae kutafakari kama hayo mabilioni ya pesa yasingeweza kuleta manufaa makubwa zaidi kama yangeelekezwa kwenye kuboresha elimu, au afya zetu, au kwenye miradi ya kutunza na kuhifadhi mazingira.

Wapo watakaosema kuwa ni serikali ndiyo inayopaswa kuhakikisha kuwa raia wake wanapata huduma zote za jamii. Kinadharia utaratibu ni huo, lakini ukichunguza hali halisi utabaini kuwa hata kwenye nchi tajiri serikali inahitaji mashirika yasiyo ya kiserikali kushirikina nayo kuziba mapengo ya huduma mbalimbali za jamii.

Watu wazima ndiyo wenye uwezo wa kubadilisha mitazamo juu ya masuala mbalimbali. Kama sisi hatubadiliki, basi tunarithisha mitazamo na matatizo yetu kwa vizazi vijavyo.

Si chini ya mara sita kwa mwaka kijijini Butiama nasikia sherehe ya harusi ikifululiza kwa siku mbili au tatu. Kupata usingizi si rahisi kwa sababu muziki wa sherehe ni wa sauti ya juu kabisa. Mtoto anayeshuhudia sherehe za aina hii naye anajifunza kufuata desturi hiyo hiyo ya kuchangisha pesa za sherehe na kuziteketeza kwenye sherehe.

Watu wazima tukianza kuchangisha pesa na kuzielekeza katika masuala yenye manufaa mapana kwa jamii, tutalea vizazi vinavyowajibika kukabiliana na matatizo ya jamii zaidi ya matatizo binafsi.

Siamini kuwa Watanzania hawana moyo wa kutoa. Nadhani tatizo ni tumepitia kipindi kirefu ambacho msisitizo uliwekwa kwenye serikali au wahisani kutatua matatizo yetu yote na sisi kujiona tuna wajibu wa kugharimia sherehe tu.

Mabadiliko yakitokea hizi harambee za Ojai zitaandaliwa Butiama, zitaandaliwa Muleba, zitaandaliwa Mwanza, na zitaandaliwa kwingineko kote nchini.

.tamati…

2824 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!