Waziri mstaafu aliyeanzisha kanisa

Aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha wakati wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Dk. Kilontsi Mporogomyi, ameanzisha kanisa. Kanisa hilo lenye Makao Makuu Makongo, linatambulika kwa Jina la Kanisa la Miujiza, Uponyaji, Kufunguliwa na Mafanikio.

Akizungumza na JAMHURI ofisini kwake wiki iliyopita, Mporogomyi ambaye sasa ni Askofu Mkuu wa kanisa hilo, amesema kwamba kumtumikia Mungu lilikuwa ni jambo la kwanza katika maisha yake.

 

“Najua mtaniuliza kwanini nimeanzisha kanisa. Mimi sikuanzisha kanisa, inawezekana kabisa mimi niliitwa kufanya kazi ya Mungu, inawezekana kuwa Mungu alikuwa ananiita tangu siku za nyuma kumtumikia, kama mnavyojua kuwa mimi nilikuwa mwakilishi wa Tanzania Jumuiya za Ulaya, nafasi hii ilinipa fursa ya kutembea nchi nyingi.

 

“Inawezekana kabisa mimi nilikuwa na wito ambao sikujua kuna watu na wito wa kumtumikia Mungu. Tangu zamani kumtumikia Mungu lilikuwa ni jambo la kwanza, haya ya siasa yalikuja baadaye.

 

“Mwaka 2006 nikiwa hotelini mjini Barbados, mji mkuu wake unaitwa Bridgetown, nilipooza viungo vyote nikapofuka lakini wakati huohuo nilipata nafasi ya kuongea na Mungu.

 

“Nikamwambia Mungu nafikiri ulichonifanyia si sahihi mie nimefika  hapa kwa ajili ya mkutano lakini sijafanya kazi yoyote, hivyo nikamwambia Mungu nataka  kesho niende niifanye mikutano yangu yote.

 

“Ilikuwa saa nane usiku nikalala asubuhi niliamka salama nikaongoza mkutano wangu wa kwanza vizuri hadi watu wakashangaa.  Huu ulikuwa ni mkutano wa kwanza, nikaingia katika mkutano wa pili wakati huu nilikuwa nawasilisha andiko, katika mkutano na vivyo hivyo nilifanya vizuri mno. Nilikuwa na rafiki mbunge kutoka Sweden akaniomba niwasilishe paper yake iliyokuwa inasema kuhusu hali ya umaskini wa Afrika nikashangliwa”.

 

Mporogomyi  amesema kwamba baada ya kumaliza kikoa hicho, alitakiwa kwenda Ujerumani lakini hakufanya hivyo.

 

“Nilimwambia mwenzangu yeye aende Ujerumani, akaniuliza kwanini, nikamwambia kuwa mie naumwa hivyo unavyoniona kwa macho ni kama mzima lakini mie naumwa wewe nenda,” amesema.

 

Alisema alirudi nyumbani Tanzania kwa ajili ya matibabu na kupelekwa nchini India ambako alikaa kwa miaka mitatu.   Akiwa katika Hosptali ya Apollo matibau yake yalikuwa ni kama miujiza  kwa kuwa alifanyiwa upasuaji wa macho, mikono na miguu.

 

Mporogomyi  aliyepata kuwa Mbunge wa Kasulu kwa miaka 15, amesema baada ya kupata nafuu alianza kutoa huduma ya uponyaji katika hospitali hiyo.

 

“Nami nilianza kutoa huduma ya uponyaji, niliwaponya watu wengi waliofika kutibiwa pale nao wakapona na kurudi nyumbani.  Haya mambo ni kama miujiza tu nilipokuwa India niliambiwa na Mungu unakwenda kuanzisha kanisa, kweli niporudi nyumbani nilikuta watu wamefanya kila kitu kuhusu kuanzishwa kwa kanisa.

 

“Nilifika na kuambiwa kuwa wanataka niwe kiongozi wao, kila mtu alitaka niwe kiongozi hata wale walioanzisha nao pia  walitaka hivyo, lakini  baada ya kushika cheo siwaoni walikokimbilia,” amesema.

 

Amesema baada mwaka mmoja baadaye alianza harakati ya kulisambaza kanisa hilo katika mikoa mingine hivyo alianza na Mkoa wa Mara.  Katika mkoa huo, kanisa lake limepata waumini wengi na sasa yuko mbioni kupeleka  ujumbe wa Mungu katika mikoa ya Kagera na Mwanza.

 

Siasa ya Tanzania

Akizungumzia sasa za Tanzania, Askofu Mkuu Mporogomyi anasema kuwa kama siasa inahitaji kufanikiwa, inatakiwa kujishughulisha na umaskini wa watu.

 

“Tumetumia njia nyingi ili kuhakikisha maendeleo yanaonekana, lakini kuonekana kunatakiwa kule watu wanapoishi ni lazima kuwa na basic needs wawe na maji, wawe na hospitali na barabara ili kile kidogo wanachozalisha waweze kukisafirisha.

 

Lakini haya yote hayajatendeka, ukienda kule kijijini utakuta kuna majengo ya hospitali lakini hakuna dawa, watu wengi wanatembea umbali mrefu kwa ajili ya kufuata maji, bado kuna changamoto kubwa inayoikabili Serikali,” amesema.

 

Amesema ili iweze kufanikiwa viongozi wanatakiwa kuwa jirani na watu. Amesema kuwa pia viongozi hao wawekewe malengo na kuyafakia. Hivi sasa viongozi hawaendi kwa wananchi ili kujua matatizo yao.

 

“Mimi niliwahi kufanya utafiti kwa kushirikiana na chuo kimoja cha Marekani, nikakuta watu wanaharibu udongo kwa kushindwa kutumia mbolea vizuri, sasa haya walitakiwa kuwaambia na viongozi.

 

“Nikagundua tatizo kubwa nililoliona ni kuwa na elimu ndogo ya kutumia mbolea.   Wakulima wengi wamekuwa wanatumia vibaya mbolea na kuharibu udongo kutokana na elimu ndogo waliyonayo kuhusu kilimo.

 

Kuhusu maadili ya viongozi, amesema imefika wakati sasa Watanzania kuchagua viongozi wanaokerwa na matatizo ya viongozi na si kuchagua kwa kuangalia sura ya mtu.

 

Uwekezaji

Askofu Mkuu Mporogomyi amesema umefika wakati sasa Serikali kuwapa fursa wachimbaji wadogo wadogo ili washiriki katika uchimbaji wa madini.

 

“Sasa natoa mfano, unaweza kuja na mpango wa kuwezesha watu wetu kushiriki katika kukuza uchumi wao na wananchi – wawe na mgodi wao lakini sasa tutakuta kuna mtu anasema hapana.

 

“Sasa tunataka watu wetu washiriki katika uchimbaji wa madini, lakini kuna kiongozi nakuja nasema hawa watu wasishiriki, tunasahu kuwa hawa wachimbaji wakubwa hawalipi kodi, lazima tuwe na aina ya wawekezaji wanaotakiwa Tanzania, si kila mtu anayetaka kuja kuwekeza Tanzania anaruhusiwa, hii si sahihi,” amesema.

 

Ametoa mfano wa Afrika Kusini ambayo asilimia kubwa ya wamiliki wa migodi  hiyo ni wananchi wa nchi hiyo.  Afrika Kusini wana mgodi wao mkubwa unaomilikiwa na wanachi wa nchi hiyo, na unafadhiliwa na Serikali na hapa tunataka wachimbaji wadogo wadogo nao washiriki katika uchimbaji wa madini. Inashangaza kuona kuwa inawashikilia wachimbaji wakubwa na kuwasahau wadogo, lakini ikumbukwe kuwa hawa wakubwa ndiyo wanaokwepa kulipa kodi.

 

Ushirikiano wa Wizara

Askofu Mkuu Mporogomyi amesema nchi haitaendelea iwapo wizara zake hazitakuwa na ushirikiano katika utendaji wa kazi wa kila siku.

 

“Haiwezekani  nchi kama hii wizara hazishirikiani, kila wizara inafanya kazi kivyake, hakuna inayoshirikisha nyingine, kama zikiunganisha nguvu na kushirikiana zinaweza kufanya kitu kingine.

 

“Lazima mipango yetu iwe shirikishi ili kuleta maendeleo. Mfano, Wizara ya Kilimo ikisema inapeleka mradi wa kilimo, Wizara ya Maji nayo inasaidia kupeleka maji inafanya kazi kivyake, lazima zishirikiane, zikishirikiana lazima zitaibuka na kitu kingine,” amesema.

 

Unaweza kuchagua mkoa mmoja maskini kama Mtwara, unapeleka mradi mkubwa kule kwa ajili ya kusaidia watu wa kule.

 

Ulafi wa viongozi

Askofu Mkuu Mporogomyi amesema kuwa Tanzania ya sasa si ile ya zamani, amani inatoweka kila siku kutokana na dhuluma inayofanywa na walio madarakani.

 

“Kuna jambo nataka kuzungumza hapa, nikiwa kama Mtanzania kwanza ninampenda sana Mungu, hivi ni kwanini kila Mtanzania anayeingia madarakani lazima ajilimbikizie mal?.

 

“Watu wamejaa ubinafsi na hii inasababisha watu kutokuwa na imani na viongozi, wanazua manung’uniko na kuzua migawanyiko mikubwa na baadaye amani inatoweka, hii ni kwa sababu ya watu kuwa na ubinafsi na kusahau wengine,” amesema.

 

Amesema tatizo jingine linaloitesa Serikali ni majungu kushamiri katika ofisi mbalimbali za Serikali. Viongozi wanaofanya kazi vizuri ndani ya Serikali huonekana maadui, hivyo kufanyiwa majungu na kufukuzwa kazi au kuumizwa.

 

“Kila kiongozi mzuri ndani ya nchi hii hufanyiwa majungu hadi aondolewe katika nafasi yake, sasa watu wanaogopa kufanya kazi,” amesema.

 

Amemaliza kwa kusema kwamba  viongozi wengi sasa hawana maadili mazuri kutokana na kujilimbikizia mali na kusababisha kuwapo kwa pengo kubwa kwa walionacho na wasionacho.

1396 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!