Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania (TRCS), kinakabiliwa na tuhuma za kulindana, kupeana na kupandishana vyeo kiholela, upendeleo, wafanyakazi hewa, kutolipa kodi kwa muda na kuajiri wataalamu wasio na sifa. 

Kuna mkanganyiko wa muda mrefu wa nani hasa mwangalizi wa Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania, hali inayokifanya kionekane kuwa ni ‘shamba la bibi’. 

Miongoni mwa mambo yanayojadiliwa sasa ni kuajiriwa kwa mwanafunzi anayedaiwa kuwa ni ndugu wa mmoja wa vigogo kwenye chama hicho. 

“Ajira za aina hii ndani ya TRCS ni za kawaida, madudu ni mengi, ikiwemo pia ubadhirifu wa fedha na rushwa. Kwa kifupi pale ni kijiwe cha upigaji [ulaji fedha],” kinasema chanzo chetu na kuongeza:

“Inasikitisha kuona hakuna hatua zinazochukuliwa huku ukiukwaji wa taratibu ukiendelea kama kawaida. Mfano mzuri wa hili ni kuajiriwa kwa mtu ambaye bado yuko chuo.”

Mwanafunzi huyo wa mwaka wa kwanza katika Chuo cha Ufundi Arusha, anadaiwa kuwa ni ndugu wa mmoja wa vigogo wa TRCS. Kwa sababu za kitaaluma, tunahifadhi jina lake kwa sasa. Anasoma uhandisi wa ujenzi na umwagiliaji. Aliajiriwa Desemba mosi, mwaka jana.





Wafanyakazi wa Chama cha Msalaba Mwekundu nchini wakiangalia hali ya mafuriko katika Mto Msimbazi eneo la Kigogo jijini Dar es Salaam.

Barua yake ya ajira iliandikwa Novemba 30, mwaka jana na kusainiwa na Katibu Mkuu wa TRCS, Julius Kejo. Ameajiriwa kwa nafasi ya Ofisa Uhamasishaji wa Jamii wa Mradi wa Wash ulioko Simanjiro, mkoani Manyara; na pia kaimu mratibu wa TRCS mkoani humo.

Kiwango cha mshahara anacholipwa ni Sh 2,625,000 kwa mwezi. Licha ya kuajiriwa, amekuwa haonekani mara kwa mara katika kituo chake cha kazi, kwa kile kinachoelezwa kuwa ni kutingwa na masomo. 

“Ameshapokea mishahara miwili ya Desemba, 2019 na Januari, mwaka huu bila kufanya kazi yoyote. Hatushangai kuona huyu jamaa bado anaendelea kuwapo, na kuna ndugu yake mwingine naye ajira yake ina utata vilevile,” kinasema chanzo chetu.

Kejo, amezungumza na JAMHURI na amekiri kuifahamu ajira ya mwanafunzi huyo, na kwamba suala hilo linafanyiwa kazi. Hakueleza aina ya hiyo ‘kazi’ inayofanywa, ingawa amesisitiza kuwa hatalipwa mshahara wa Februari. 

“Tatizo la huyo mfanyakazi tumelibaini na linafanyiwa kazi, lakini sijui kabisa kama ana undugu na kiongozi yeyote wa Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania. Suala lake halimaanishi kuwa taasisi yetu ina matatizo makubwa kwenye uendeshaji wake kama inavyodaiwa. 

“Sisi kama taasisi hatuwezi kukosa kasoro, lakini hali si mbaya kama watu wachache wanavyojaribu kuonyesha. Kosa la [mwanafunzi mwajiriwa] lilifahamika ilipogundulika kuwa hafiki kazini kama inavyopaswa na suala lake linashughulikiwa na litakamilika hivi karibuni,” anasema.

TRCS inatuhumiwa pia kwa kutowasilisha mamilioni ya shilingi za kodi zinazotokana na mshahara au mapato ya mfanyakazi (PAYE); licha ya wafanyakazi kukatwa fedha kwenye mishahara yao.

Mawasilisho ya kodi hiyo yaliyokuwa hayajafanywa hadi mwishoni mwa mwaka jana yalikuwa zaidi ya Sh milioni 700. Fedha hizo ni pamoja na kodi zilizopaswa kulipwa kuanzia mwaka 2012 hadi 2016; na malimbikizo ya Mei, 2017 hadi Desemba, mwaka jana. 

Kejo anajitetea kwa kusema: “Sisi tunalipa hii kodi kila mwezi kwa zaidi ya asilimia 90 kwa watu wote wa miradi na taasisi yote kwa ujumla ambayo ina wafanyakazi zaidi ya 600. Ni watu wachache tu zinachelewa, lakini taarifa zinakuwepo kuwa tutalipa.”

Kumekuwapo malalamiko ya kuanzishwa kwa cheo cha ‘Naibu Katibu Mkuu wa TRCS’ kinyume cha katiba ya chama hicho kwa lengo la kumlinda John Busungu, ambaye inadaiwa awali aliajiriwa kama Meneja Mkaguzi wa Hesabu wa Ndani bila kuwa na sifa za nafasi hiyo.

Nyaraka kuhusu ajira yake na mawasiliano ya ndani vinaonyesha kuwa Busungu anatuhumiwa pia kwa kuwa Mkaguzi wa Ndani bila kuwa na usajili kwenye Bodi ya Taifa ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu (NBAA) na CPA kama sheria inavyoelekeza.

Kejo anasema nafasi ya awali ya Busungu haikuwa tu ya ukaguzi wa ndani kama inavyodaiwa, bali pia alijihusisha na masuala ya kukidhi vigezo kwenye shughuli za taasisi na kudhibiti vihatarishi (internal audit, compliance & risk management).

 “Tulipotangaza nafasi hii tulibainisha haya yote na kigezo hakikuwa tu cha ukaguzi wa ndani na upungufu uliojitokeza sababu yake kubwa ni kutokana na kwamba ndiyo ilikuwa mara ya kwanza kuwa na kitengo hiki. Hata hivyo, hivi sasa nafasi hiyo inashikiliwa na mtu mwenye CPA na mwenye usajili wa NBAA,” anasema Kejo. 

Vyanzo vyetu vinasema nafasi ya Naibu Katibu Mkuu iliondolewa na Mkutano wa Halmashauri Kuu ya TRCS Novemba, mwaka juzi lakini ilirejeshwa Oktoba, mwaka jana mahususi kwa ajili ya Busungu, baada ya kuwapo shinikizo la yeye kutokuwa na sifa za kumwezesha kuwa Meneja Mkaguzi wa Hesabu wa Ndani.

Kuna malalamiko kuwa nafasi hiyo ilirejeshwa bila kufuata utaratibu au kuzingatia katiba ya chama hicho, kifungu cha 42 (ii) kinachotaka mabadiliko yoyote yanayofanyika yawasilishwe kwenye Kamati Kuu ya pamoja ya Shirikisho la Vyama vya Msalaba Mwekundu na Mwezi Mwekundu (IFRC); na kwenye Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC). 

Kejo anasema marekebisho ya katiba yaliyofanywa yalipata baraka zote. Kejo anasema baadhi ya mambo kwenye uendeshaji wa chama hicho kama yale ya kimuundo hayahitaji mabadiliko ya katiba au idhini ya IFRC na ICRC; akisisitiza kuwa uendeshaji wa vyama vya msalaba mwekundu huzingatia pia mazingira husika.

By Jamhuri