Vitambulisho vya wajasiriamali vilivyotolewa na Rais Dk. John Magufuli mwaka jana vimeyageuza maeneo mengi katikati ya Jiji la Dar es Salaam kuwa masoko yasiyo rasmi, JAMHURI limebaini.

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI na kuthibitishwa na baadhi ya watumishi wa Halmashauri ya Jiji umethibitisha kuwa kwa kiasi kikubwa hilo linatokana na uzembe wa halmashauri za manispaa kushindwa kuwa na mipango madhubuti ya kuhakikisha wafanyabiashara hao wanatengewa maeneo mahususi kwa ajili ya shughuli zao.

Hivi sasa watu wanaofanya kazi katikati ya Jiji la Dar es Salaam hawana haja ya kupanga muda wa kwenda sokoni, kwani karibu bidhaa zote zinazouzwa katika masoko zinapatikana kandokando ya barabara za katikati ya jiji.

Ukihitaji nyanya, mboga za majani, vitunguu, karoti, dagaa, viatu, vyombo vya nyumbani, nguo za mitumba, mabegi, mikanda, simu za mkononi, miwani, vifaa vya mazoezi, vitabu na mahitaji mengine mengi hakuna ambacho utakikosa.

Hata biashara ya vyakula inayofanywa na mama na baba lishe sasa imetekwa na wajasiriamali hao ambao hutumia mikokoteni kutengeneza vyakula mbalimbali kama vile ndizi za kuchoma, mishikaki, kuku wa kuchoma, chips, mayai, mihogo na viazi vya kichoma, sharubati ya miwa, soda na vyakula vingine.

Onyo lililotolewa na Rais Magufuli mwaka jana kuzitaka halmashauri kutowabughudhi wafanyabiashara hao limetumiwa na wajasiriamali hao kujipenyeza katika kila eneo lenye nafasi katikati ya jiji na kuanzisha biashara zao.

Jambo linaloleta wasiwasi ni kuwa, hakuna mpangilio maalumu wa wafanyabiashara hao wala udhibiti kiasi kwamba katika baadhi ya maeneo, wezi wa vifaa kwenye magari nao wanautumia mwanya huo kujichanganya kati ya wajasiriamali hao na kufanya uhalifu wao.

Kwa upande mwingine, imezuka hofu ya kuibuka kwa magonjwa ya mlipuko, kwani hakuna udhibiti wa kiafya kwa vyakula vinavyouzwa na wajasiriamali hao.

Wataalamu wa masuala ya afya na lishe wanasema vyakula vingi vinavyoandaliwa na vijana hao na baadhi ya mama na baba lishe havina sifa ya mlo kamili, jambo ambalo linaweza kusababisha matatizo makubwa ya afya ya jamii, ikizingatiwa kuwa watu wengi wanaofanya shughuli zao katikati ya jiji hutegemea vyakula hivyo.

Kwa mujibu wa wataalamu hao, kula vyakula visivyo na sifa ya mlo kamili kunaweza kusababisha watumiaji wake kuwa na upungufu wa virutubisho muhimu mwilini.

Akizungumzia hali hiyo, Ofisa Afya wa Manispaa ya Ilala, Reginald Mlay, anasema serikali inajitahidi kudhibiti hali ya mama lishe na baba lishe kuuza vyakula kiholela katika manispaa zote za Jiji la Dar es Salaam.

Anaeleza kuwa serikali ilitenga maeneo maalumu ya kuuzia vyakula hivyo, lakini kutokana na idadi ya watu kuongezeka kila siku utaratibu huo umevurugika.

Anasema maeneo mengi yaliyotengwa yalikuwa karibu na Buguruni, Kisutu, Mnazi Mmoja, Miti Mirefu pamoja na Karikoo karibu na Soko Kuu.

“Sasa hivi tunatekeleza agizo la Rais Magufuli kwamba wafanyabiashara wadogo waachwe wafanye biashara zao wasibughudhiwe. Katika Awamu ya Tano Rais Magufuli aliona watu  wengi wanapata shida, akaja na utaratibu wa kuwapatia vitambulisho wafanyabiashara wadogo ili wafanye biashara zao bila bughudha,” anasema Mlay.

Anasema wauza vyakula hao hawatatimuliwa katika maeneo wanayoyatumia hivi sasa, badala yake wao wamekuja na mkakati wa kutoa elimu ya afya na chakula kwao ili wauze  chakula hicho katika mazingira salama.

“Kuanzia ngazi ya mtaa hadi mkoa tuko kwenye mkakati wa kusimamia suala hili. Tunajipanga kufikisha elimu kwa mama lishe wote na tutahakikisha tunasimamia chakula kinakuwa kwenye hali njema,” anasema.

Aidha, anasema mpaka sasa hakuna sehemu ndani ya Jiji la Dar es Salaam kumeripotiwa mlipuko wa ugonjwa unaotokana na uuzwaji wa vyakula kiholela.

Anasema kwa sasa wameanzisha kipindi kwenye redio na Tv kuhusu afya na usalama wa chakula ndani ya jiji.

“Hawa watu si kwamba tumewaacha tu, kuna programu tumeanzisha City Radio na Channel Ten, kupitia vyombo hivyo tunawaelimisha waandaaji na watumiaji wote kuhusu usafi wa mikono kabla ya kushika chakula. Tunatoa elimu kuhusu mazingira ya kuandaa chakula, vyombo viwe safi, maji ya kuoshea vyombo na mikono yawe safi. Tunawashauri chakula kiliwe angalau kikiwa cha moto, tunawaelimisha kuhusu matumizi ya maji ya bomba na kisima yaliyo salama,” anaeleza Mlay.

Pamoja na hayo, Mlay anasema wana mpango wa kuwashirikisha mama na baba lishe 800 kwenye mafunzo maalumu ya kuzingatia usafi wa vyakula wanavyouza.

Anasema mpango huo ambao utazinduliwa hivi karibuni utawashirikisha zaidi ya mabwana afya wa serikali za mitaa takriban 50.

Aidha, anasema kwa sasa wako kwenye opresheni ya kuhakikisha matunda yote yanayouzwa katika Jiji la Dar es Salaam kuwa kwenye vifungashio.

Anawatoa hofu walaji wa mishikaki inayouzwa kwenye mikokoteni katika mitaa mbalimbali ya jiji kwani nyama yake inatoka katika machinjio ya serikali yanayotambulika kisheria.

Hata hivyo, amekemea tabia ya baadhi ya wapishi kutumia vitambaa na vipande vya magodoro kugeuzia chapati na kubainisha kuwa hilo linahatarisha afya za walaji, kwani usafi wa vifaa hivyo ni mdogo.

Naye, Enezael Emmanuel, Ofisa Afya wa Mkoa wa Dar es Salaam, anasema kwa sasa maofisa afya wa serikali za mitaa wanashughulikia suala hilo kwa kushirikiana na viongozi wa mitaa.

“Sisi huku juu tuna nafasi ndogo ya kutoa taarifa halisi ya hali halisi ilivyo huko mitaani, ila ukiongea na maofisa afya tuliowaweka huko watakueleza ukweli wote,” anasema Emmanuel.

Wakizungumza na JAMHURI, baadhi ya watu wanaofanya shughuli zao katikati ya jiji wameonyesha wasiwasi wao kuhusiana na ongezeko la wajasiriamali hao, hasa wauza vyakula.

Suzan Benedict, mkazi wa Ubungo, anasema japo naye anawategemea mama lishe kwa chakula cha mchana, anakerwa na hali iliyopo kwa sasa.

Kwa upande wake, Ajuaye Philipo, mkazi wa Kigogo, anayeuza mishikaki kwenye mkokoteni katika Mtaa wa Somali, Kariakoo, anasema anazingatia usafi wa mishikaki yake.

 “Hii ndiyo kazi inayonifanya nilipe kodi na kuendesha maisha yangu ya kila siku, naishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuja na wazo zuri la vitambulisho vya machinga,” anasema Philipo.

Nashon Lenard, anayefanya biashara ya kusafirisha mizigo kwenda mikoani anatahadharisha kuwa wauza vyakula hao wasipodhibitiwa wanaweza kusababisha kuibuka kwa magonjwa ya mlipuko.

“Mimi ningeshauri wanaouza vyakula katikati ya mji watengenezewe vitambulisho vyao maalumu na watengewe maeneo maalumu ya kuuzia vyakula ili kuongeza udhibiti… tunacheza na afya za watu,” anasema Lenard.

By Jamhuri