Serikali imetakiwa kuangalia kwa mapana sekta ya kilimo pamoja na kukubali kufanyia kazi kwa vitendo ushauri unaotolewa na wataalamu wa kilimo na uchumi kwa ajili ya kufanya maboresho katika sekta hiyo.

Kutokana umuhimu wa kilimo katika kufanikisha Tanzania ya Viwanda. Mtaalamu wa Uchumi wa Kilimo, Profesa Anna Tibaijuka, amesema kuwa kinachokwamisha maendeleo katika sekta ya kilimo hapa nchini ni ukosefu wa mtaji, wataalamu pamoja teknolojia ambayo ni muhimu katika kilimo cha kisasa.

Amesema kuwa kitaalamu, ili sekta ya kilimo ifanyiwe kazi kikamilifu, utendaji wake unapaswa kuzingatia sayansi na teknologia pamoja na fedha kwa ajili kukamilisha miradi mbalimbali ya kilimo hapa nchini.

“Wataalamu wapo ila unaweza ukawa na utaalamu wa kilimo, lakini ukaishauri mamlaka husika unakuta ushauri wako hawaufanyii kazi,” amesema Prof. Tibaijuka.  

Mchumi huyo ameeleza kuwa nchi nyingi za Kiafrika ikiwamo Tanzania, kuna ardhi kubwa lakini ukosefu wa fedha na wataalamu ni kikwazo, hali inayosababisha utekelezaji wa shughuli za kilimo kutofikia malengo.

Amebainisha kuwa ili nchi ifanikiwe katika kilimo, lazima kutatua changamoto ya ukosefu wa fedha na wataalamu, jambo ambalo linaweza kufanikiwa kwa haraka.

“Nchi yoyote iliyoendelea duniani inatokana na shughuli za kilimo. Mfano Marekani imeendelea kutokana na kuipa kipaumbele sekta ya kilimo, huku wakitumia teknolojia bora,” amesema Prof. Tibaijuka.  

Prof. Tibaijuka ambaye aliwahi kufundisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Kitendo cha Utafiti wa Uchumi, amefafanua kuwa wapo wanafunzi wanaomaliza taaluma ya kilimo katika vyuo mbalimbali hapa nchini, lakini wameshindwa kuifanyia kazi taaluma yao kutokana na ukosefu wa mtaji.

Amesema kuwa sasa tunazalisha wasomi ambao ni vigumu kupata ajira, hata wale wanaobahatika kupata kazi ni wachache tofauti na idadi ya wanaohitimu masomo hayo.

“Ukisema vijana wajiajiri, jambo la msingi la kujiuliza wanajiari kupitia sekta gani? Kama ni kilimo wanapaswa kuwezeshwa ardhi, mikopo pamoja na elimu ya kilimo,” amesema Prof. Tibaijuka.

Prof. Tibaijuka ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo na Makazi katika Serikali ya Awamu ya Nne, amebainisha kuwa Serikali ya sasa ina mipango ya kufanikisha uchumi wa viwanda, ambapo bila kilimo cha kisasa ni vigumu kutekelezeka.

“Viwanda vinahitaji malighafi ya kutosha. Jambo hilo litasaidia katika kufanikisha utekelezaji wa viwanda hapa nchini na kupiga hatua kimaendeleo endapo kilimo kitapewa kipaumbele,” amesema Prof. Tibaijuka.

Ameeleza kuwa alipokuwa Waziri wa Ardhi alijitaidi kusema na kuishauri Serikali kuhusu mipango kadhaa katika sekta ya ardhi katika kuitumia vyema kwenye shughuli za kilimo.

Prof. Tibaijuka anafafanua kuwa Tanzania imebarikiwa kuwa na ardhi ya kutosha lakini tatizo ni upatikanaji wa fedha, jambo ambalo ni tofauti na nchi nyingine nyingi duniani.

“Ndiyo maana nilipokuwa waziri nilianzisha sera ya ubia katika mashamba makubwa (Land for Equity), lengo likiwa ni kupanua fursa ya uwekezaji pamoja na kuwabana wawekezaji,” amesema. 

Amesema kuwa sera hiyo ni rafiki kwa umma kwa sababu inaepusha migogoro ya ardhi inayoweza kujitokeza kipindi ambacho mwekezaji anaanza kuwekeza hasa katika sekta ya kilimo, jambo ambalo tunaweza kupiga hatua katika nyanja za kimaendeleo.

Hata hivyo, ametoa angalizo kwa Serikali kuwa makini wanapowakaribisha wataalamu na wawezekezaji kuwekeza katika sekta ya kilimo, hasa katika kuingia nao ubia kwenye mashamba makubwa.

“Tusipokuwa makini katika ardhi, siku za usoni unaweza ukakuta kuna migogoro ya ardhi baada ya watoto wetu kukosa ardhi kutokana na kutwaliwa na wageni,” amesema Prof. Tibaijuka.

Mhadhiri wa Uchumi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Humphrey Moshi, amesema kuwa kilimo kinachotakiwa kupewa kipaumbe kwa sasa ni kilimo cha umwagiliaji.

Amesema kuwa nchi inatakiwa kufanya maboresho makubwa katika sekta ya kilimo ikiwamo miundombinu ya umwagiliaji ili kuhakikisha inasaidia kukuza uchumi.

Profesa Moshi amesema kuwa kukiwa na maji ya kuaminika kutasaidia kuleta hamasa katika kilimo pamoja na kuchochea ukuaji wa uchumi hapa nchini.

Amesema kuwa viwanda ni biashara na ukizingatia biashara wakati mwingine inahitaji uamuzi wa haraka katika kufikia Tanzania ya viwanda.

Amefafanua kuwa tatizo lililopo ni wawekezaji kukosa ardhi kwa ajili ya kilimo wakati wanapohitaji kutokana na kuwa mikononi mwa watu.

“Asilimia kubwa ardhi hasa maeneo ya vijijini inamilikiwa na uongozi wa kijiji pamoja na watu binafsi, jambo ambalo wakati mwingine wawekezaji wanakuwa na wakati mgumu,” amesema Prof. Moshi.

Mbunge wa Kilwa Kusini, Suleimani Bungara, amesema kuwa jambo ambalo linatakiwa kufanyika kwa ufanisi mkubwa katika Serikali inayoongozwa na Rais John Magufuli ni kuongeza bajeti katika Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kama vile inavyofahamika isipungue asilimia 10.

Amesema kuwa ni vyema bajeti katika wizara hiyo ikaongezwa ili kuhakikisha changamoto zinatatuliwa na kupiga hatua katika sekta hiyo muhimu.

“Endapo bajeti ikiwa chini ya asilimia 10 ni tatizo katika utekelezaji wa masuala mbalimbali ya kiutendaji katika nyanja za kimaendeleo,” amesema Bungara.

Hata hivyo, amebainisha kuwa wakulima wanapaswa kuangaliwa kwa jicho la tatu kwa kupatiwa mikopo, ambayo itawasaidia kufanya kilimo cha kisasa na kuleta tija kwa Taifa.

“Sehemu nyingi hakuna wataalamu wa kilimo kwa ajili ya kutoa elimu ya kuhusu kilimo, kwani hata wale waliokuwapo wanafanya kazi chini ya kiwango kutokana na ukosefu wa fedha,” amesema Bungara.

Amefafanua kuwa baadhi ya wakulima wanalima kwa kubahatisha kutokana na ukosefu wa wataalamu, kwani wanatumia nguvu nyingi huku mavuno yakiwa madogo. Ushirikiano unaitajika katika sekta ya kilimo ili kuhakikisha wakulima katika maeneo mbalimbali wanapata mafanikio kupitia kazi wanayofanya.

Machi 1, mwaka huu, Shirika la ‘Twaweza’ walibainisha utafiti waliofanya kuhusu upungufu wa chakula, ambapo utafiti huo ulipewa jina la ‘Uchungu wa njaa’ huku takwimu zake zikikusanywa kwa awamu mbili na kubainisha kuna upungufu wa chakula.

Akifafanua kuhusu utafiti huo, Mkurugenzi wa Twaweza, Aidan Eyakuze, alisema kuwa ripoti hiyo imeonesha kuwa asilimia 51 ya kaya hazikuwa na chakula cha kutosha na unaonesha asilimia 69 ya kaya nchini zinahofia kuishiwa na chakula, huku asilimia 51 ikiripoti kutokuwa na chakula cha kutosheleza kaya nzima. 

Kutokana na hali hiyo ni kielelezo cha hali ya ugumu wa maisha iliyopo na umaskini wa kipato hapa nchini.

Inaelezwa kuwa wananchi wengi waliowahoji wamebainisha kuwa uhakika wa kupata chakula umepungua kati ya Septemba mwaka jana na Februari mwaka huu. 

Asilimia 65 ya watu waliohojiwa walikuwa na hofu ya kaya zao kukosa chakula ikilinganishwa na asilimia 45 waliosema hivyo Septemba mwaka jana.

Ripoti hiyo inaonesha kuwa asilimia 35 ya waliohojiwa waliripoti kuwa na mwanakaya angalau mmoja aliyeshinda na njaa siku nzima kwa sababu ya kukosa chakula katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita. 

Hata hivyo, hivi karibuni Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilitoa taarifa ya mwenendo wa uchumi wa nchi. Ripoti hiyo imebainisha kuwa katika kipindi cha robo tatu ya mwanzo wa mwaka 2016, uchumi ulikua kwa wastani wa asilimia 6.5 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 6.3 katika kipindi kama hicho mwaka 2015. 

Ripoti hiyo inaeleza kuwa nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2016/17, mapato yaliyokusanywa ni shilingi bilioni 8,065.2, ambazo ni sawa na asilimia 22.1 zaidi ya mapato yaliyokusanywa katika kipindi kama hicho cha mwaka wa fedha 2015/16. 

Hata hivyo, jumla ya matumizi ya Serikali yalifikia shilingi bilioni 8,535.4, yakiwa ni sawa na asilimia 1.3 zaidi ya matumizi katika kipindi kama hicho mwaka wa fedha 2015/16. 

Matumizi ya maendeleo katika nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2016/17 yalikuwa ni shilingi bilioni 2,083, ambayo ni sawa na asilimia 14.7 zaidi ya matumizi ya maendeleo katika kipindi kama hicho mwaka wa fedha 2015/16.

By Jamhuri