Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Dk. Akwilina Kayumba, anahusishwa na matumizi mabaya ya madaraka na ya fedha za umma.

Wakizungumza na JAMHURI jijini Dar es Salaam, wafanyakazi wa OSHA, pamoja na madai hayo, wamesema Dk. Kayumba amekuwa akiwaongoza kimabavu.

 

Tuhuma nyingine ni kujilipa posho nyingi kinyume cha sheria na kanuni.

“Anajilipa posho nyingi, kwa mfano kwa siku anajilipa posho ya Sh 80,000 kwa kila kipindi anachofundisha, Sh 100,000 za ufunguzi na Sh 100,000 nyingine za ufungaji wa mafunzo, jambo ambalo si sahihi kwa mujibu wa sheria na taratibu.

 

“Jambo la kushangaza zaidi ni kuwa mtendaji mkuu amejigeuza na kuwa mhasibu, ofisa ununuzi na ofisa utumishi wa OSHA. Kwa mfano, yeye ndiye anayefanya kazi ya kulipa malipo yote ikiwa ni pamoja na posho kwenye mafunzo kama kwamba ofisi haina wahasibu,” wamedai wafanyakazi hao.


Dk. Kayumba anadaiwa pia kutumia wafanyakazi tofauti kuomba na kusaini uchukuaji fedha za mamlaka hiyo, na kukabidhiwa yeye kwa ajili ya kugharamia safari za mikoani anazojiandalia.


Shutuma nyingine zinazomzunguka Dk. Kayumba ni kufuta mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI), kuwabadilisha vitengo wafanyakazi na kutumia watu wasio wafanyakazi wa OSHA kufanya kazi zilizopaswa kufanywa na waajiriwa.

 

Kwa upande wake, Dk. Kayumba amezungumza na JAMHURI na kuyakana madai ya wafanyakazi hao.

 

“Hayo yote unayoyasema sijawahi, sichukui hata senti ya Serikali, najua hapa Tanzania kuna watu ambao wako corrupt (wala rushwa) mimi siko corrupt (si mla rushwa), lakini kuna mahali ninatakiwa nilipwe kama vile kuandaa hotuba. Mimi ni mtoto wa mkulima, nawapenda wafanyakazi wangu,” amesema Dk. Kayumba.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya OSHA, Gideon Nasari, amekiri kupokea malalamiko ya wafanyakazi na kwamba ameshaweka mpango wa kuyashughulikia.

 

“Nimeshazipata hizo habari na nimemwomba Katibu Mkuu wa Wizara ya Kazi na Ajira twende tukaangalie hayo mambo, tunataka tuongee na wafanyakazi na yeye (Dk. Kayumba) akiwapo, kwa sababu hata sisi hayo malalamiko hayajaturidhisha,” amesema Nasari.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Kazi na Ajira, Eric Shitindi, ameiambia JAMHURI kwamba hajapata malalamiko kutoka kwa wafanyakazi hao.


“Mimi sina taarifa yoyote, inabidi niyapate kutoka kwao, si kwako,” amesema.

1571 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!