*Msekwa, Karume kutemwa rasmi, vigogo wengi kuangukia pua

*Wasira, Lukuvi, Membe, Makamba, Mukama wapambana

*Balozi Seif, Shamsi, Khatib, Mbarawa, Samia, Mwinyi vita kali

Wiki hii Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitakuwa katika hatua za mwisho za kukamilisha safu zake za uongozi, huku mtikisiko mkubwa ukitarajiwa kutokea kwa vigogo wengi kubwagwa kwenye nafasi ya ujumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) – viti 10 Bara na viti 10 Zanzibar.

Lakini kuna habari kwamba ili kulinda heshima ya vigogo wakongwe kuumbuliwa na wagombea vijana, kura za itifaki zinaweza kutumika. Shaka hiyo imeshawaingia wengi kutokana na kuwapo habari kwamba watakaohesabu kura wameshaandaliwa. Hatua hiyo inaelezwa kwamba itatoa mwanya kuandaa matokeo ya kiitifaki.

Mkutano Mkuu wa chama hicho utaanza Novemba 11 mjini   Dodoma, huku kukiwapo habari kwamba miongoni mwa mabadiliko makubwa yatakuwa kwenye nafasi za makamu wawili wa Mwenyekiti wa CCM Taifa kwa pande zote mbili – Bara na Zanzibar.

 

Makamu Mwenyekiti wa CCM (Tanzania Bara), Pius Msekwa, ana hatihati ya kurejeshwa kwenye wadhifa huo; huku kwa upande wa Zanzibar, Makamu Mwenyekiti, Amani Abeid Karume, naye akitarajiwa kurithiwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein.

 

Msekwa ambaye ni Spika mstaafu, anatarajiwa kupumzishwa ili nafasi yake ishikwe na kiongozi ambaye umri wake unaweza kumsaidia kukabiliana na mikikimikiki ya siasa za ushindani ndani ya CCM na nje ya chama hicho kikongwe.

 

Aidha, dhana ya kuwapa fursa vijana, kama ilivyodhihirishwa kwenye uchaguzi wa ndani ya chama hicho kuanzia ngazi ya Shina hadi Taifa, ni kigezo kingine cha kumpata mrithi wa Msekwa. Kwa upande wa Zanzibar, mabadiliko yako dhahiri kutokana na utamaduni wa chama hicho wa Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Mwenyekiti Taifa.

Mtifuano nafasi 10 NEC

Kinachosubiriwa na wana-CCM wengi ni mtifuano mkali wa kuwania nafasi 10 za wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC). Ugumu wa mchuano huo unatokana na ukweli kwamba miamba 31 kwa upande wa Tanzania Bara imejitokeza kuwania nafasi hizo; hii ikiwa na maana kwamba wanachama 21 watatupwa nje.

 

Kwa upande wa Bara, wagombea walioomba kuwania nafasi hizo 10 ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uratibu na Bunge, William Lukuvi (57); Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe (59); Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Dk. Fenela Mukangara (57).


Wamo pia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira (67); Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk. David Mathayo (43); Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama (63); Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba (38); na Katibu wa Fedha na Uchumi, Mwigulu Nchemba (34).


Wengine ni Otieno Baraka (34), Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki; Shy-Rose Bhanji (42); Twalhata Ally (31); Godwin Kunambi (27); William Malecela (51); Salehe Mhando (33); Innocent Nsena (38); Hiza Tambwe (53); Anna Magowa (54); Christopher Mullemwah (38); Mwanamanga Mwaduga (32) na Ruth Msafiri (50).

 

Katika orodha hiyo wamo pia Hadija Faraji (42); Dk. Hussain Hassan (64); Nicholaus Haule (34); Nussura Nzowa (30 ); Martin Shigela (37); Dk. Kesi Mtambo (76); Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Jackson Msome (53); Fadhili Nkurlu (44); Tumsifu Mwasamale (41); Assumpter Mshama (51) na Rashid Kakozi (33).

Kinachoweza kutokea

Hapana shaka kwamba safari hii, kama ilivyowahi kutokea huko nyuma, kura za itifaki zinaweza kuzingatiwa. Kwa maana hiyo, wajumbe wa Sekretarieti, wakiwamo kina Mukama na Makamba; na wengineo wanaweza kupita bila shaka kubwa. 

 

Wengine wanaoweza kuwika ni pamoja na Shigela pamoja na vijana wenzake hasa kutokana na ukweli kwamba kwa mara ya kwanza, Mkutano Mkuu wa Taifa wa mwaka huu unakuwa na wajumbe wengi vijana. Ni wazi kuwa vijana watabebana. Hata hivyo, haitashangaza kuona vijana kama kina Nchemba wakikwazwa.


Wasira anaweza kukwazwa na umri wake mkubwa, lakini pia anaweza kupita kutokana na umahiri wake wa kukitetea chama. Anatambulika kama mmoja wa watu wa karibu kabisa na Mwenyekiti Rais Kikwete; na kwamba hata kama ataangushwa, Mwenyekiti hatamwacha.

 

Membe anaweza kupita kutokana na ukweli kwamba amekuwa karibu na wana-CCM wengi, na pia kutokana na umahiri wake wa kujieleza na pia rekodi yake ya kusimamia masilahi mbalimbali ya nchi. Hata hivyo, mkubwa unaomkabili ni wa wafuasi wa makundi yanayotajwa kuwa ya maandalizi ya urais mwaka 2015.

 

Ingawa Membe anatajwa kuwa na kiu ya kuwania urais mwaka huo, bado kundi lake linaonekana kutokuwa na nguvu kama zile zinazotajwa kuwapo kwenye kundi la Edward Lowassa.

Zanzibar mtihani mzito

Kwa upande wa Zanzibar wagombea wako 28 wakiwania nafasi 10. Wagombea hao ni Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Iddi (70); Kidawa Hamid Salehe (52); Samia Suluhu Hassan (52); Abdisalami Issa Khatibu (72); Muhammed Seif Khatib (61); Khadija Hassan Aboud (48); Abdalla Ali Hassan (39) na Dk. Hussein Ali Mwinyi (46).

 

Wengine ni Dk. Abdalla Juma Sadalla (49); Mohamed Ahmada Salum (41); Abdulhakim Chasama (43); Ali Mohamed Ali (61); Haji Makame Ali (52); Ibrahim Khamis Fataki (40); Moza Jaku Hassan (32); Nassir Ali Juma (55); Jecha Thabit Komba (55); Khamis Mbeto Khamis (35) na Mohamed Hassan Moyo (42).

 

Orodha hiyo wapo pia Bhaguanji Mansuria (61); Moudline C. Castico (58); Omar Yussuf Mzee (53); Shamsi Vuai Nahodha (51); Yakoub Khalfan Shaha (52); Rose Joel Mihambo (34); Makame Mnyaa Mbarawa (51); Ali Omar Mrisho (60) na Mariam Omar Ali (38).

 

Vyovyote iwavyo, matokeo ya uchaguzi wa wajumbe wa NEC kwa Bara na Zanzibar mwaka huu yatakuwa ya kishindo kisichotarajiwa. Upepo wa mabadiliko unaovuma ndani ya CCM bila shaka hauwezi kuendelea kuwabeba wana-CCM wakongwe. Uchaguzi wa safari hii kwa kiasi kikubwa utakuwa ni mchuano kati ya wazee na vijana.


By Jamhuri