Mwanaanga maarufu kutoka Marekani Buzz Aldrin amewashtaki watoto wake wawili na meneja wa zamani wa biashara zake akidai kwamba waliiba pesa zake.

Aidha, anadai walimharibia sifa ambazo amejizolea katika maisha yake.

Kesi hiyo, ambayo ilifichuliwa Jumatatu, iliwasilishwa katika mahakama moja mjini Florida wiki moja baada ya watoto wake kuwasilisha ombi mahakamani wakitaka waruhusiwe kuchukua udhibiti wa fedha zake.

Jamaa zake walikuwa wamemwambia jaji kwamba anahitaji mlezi wa kumwakilisha kisheria kwa sababu uwezo wake wa “kufikiria umeshuka sana”.

Mzee huyo wa miaka 88 alikuwa mtu wa pili kuwahi kutembea kwenye Mwezi.

Katika mahojiano na gazeti la Wall Street Journal wiki iliyopita, Aldrin ambaye ni kanali mstaafu wa jeshi la wanahewa la Marekani alisema: “Hakuna mtu atakayekaribia kufikiria kwamba ninaweza kuwekwa chini ya mlezi.”

Kwenye kesi hiyo, anadai kwmaba mwanawe wa kiume, na binti yake pamoja na meneja wake wa zamani Christina Korp pia walivuruga uhusiano wake wa kimapenzi na watu wengine na kumzuia kuoa tena.

Mzozo unahusu zaidi usimamizi wa kampuni yake ya kibinafsi, Buzz Aldrin Enterprises, na shirika la hisani kwa jina ShareSpace Foundation.

Katika ombi waliloliwasilisha mahakamani, wanawe Andrew Aldrin, 60, na Janice Aldrin, 60, walisema baba yao hivi karibuni ameanza kujihusisha na marafiki wapya ambao wanajaribu kumpotosha na kumtenganisha na familia yake.

Walisema pia kwamba amekuwa akitumia pesa kwa “kasi ya kushangaza.”

Bw Aldrin kwenye kesi yake anadai kwamba mwanawe wa kiume na Bi Korp wamechukua udhibiti wa fedha zake bila idhini – ikiwa ni pamoja na turathi za kutoka anga za juu pamoja na vitu vingine vyake vya thamani kubwa kuhusiana na anga za juu, vyote vya mamilioni ya dola.

Ameongeza kwamba walifanya hivyo kwa lengo la “kujifaidi wenyewe.”

Kesi hiyo pia inadai wamekuwa wakimharibia jina kwa muda mrefu kwa kudai kwamba anakabiliwa na magonjwa magonjwa ya kiakili ya kupoteza kumbukumbu na kutojielewa, na pia anaugua ugonjwa wa Alzheimer.

Anamtuhumu mwanawe wa kiume kwa kumtumia vibaya mtu mzee kujifaidi kwa kumpokonya mali yake kwa kutumia njia za ulaghai.

Bintiye anamtuhumu kwa ulaghai na kwa kutotetea maslahi yake ya kifedha.

Mwanawe wa kiumbe wa kwanza hajahusishwa katika kesi hiyo.

Mtaalamu wa afya ya kiakili aliyeteuliwa na mahakama anatarajiwa kumpima Bw Aldrin baadaye wiki hii.

Kupitia taarifa, watoto wake wamesema wamesikitishwa sana na kesi hiyo isiyo ya haki.

“Familia yetu bado ina umoja na azma yetu ya kufanya kazi kwa pamoja na kutatua matatizo pamoja na kutimiza mambo makuu bado ni kuu,” watoto hao wa Aldrin wamesema.

By Jamhuri