Mtume Muhammad (S.A.W) ni mfano mwema wa kuigwa

Makala yetu leo inaangazia Sura ya 33 (Surat Al-Ahzaab), Aya ya 21 katika Quraan Tukufu ambapo Mwenyezi Mungu Mtukufu anatuambia kuwa: “Hakika nyinyi mnayo ruwaza njema (mfano mwema) kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa anayemtaraji Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, na akamkumbuka Mwenyezi Mungu sana.”
Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) ni mwanadamu aliyefaulu, kwa msaada wa Allaah, kuishi maisha anayoyataka na kuyaridhia Mola wake mtukufu kabla na baada ya kupewa Utume.
Kwa maneno mengine, Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) aliishi na alijipamba na tabia zinazoelekezwa na Quraan Tukufu, kitabu ambacho Mwenyezi Mungu Mtukufu amekisifu kuwa ni “Kitabu kisichokuwa na shaka ndani yake; ni uongofu kwa wacha Mungu.” (Quraan Tukufu, Sura ya 2 (Surat Al-Baqarah), Aya ya 2).
Ndiyo maana Bibi Aisha (Allaah Amridhie) alipoulizwa juu ya tabia (mwenendo) wa Mtume Muhammad alisema: “Tabia yake ni Quraan”; yaani, Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) amejipamba na vipengele vyote vya tabia njema vilivyobainishwa katika Quraan Tukufu.
Kwamba Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) alijipamba na vipengele vyote vya tabia njema vilivyobainishwa katika Quraan Tukufu, ni uthibitisho wa kuwa mwongozo wa Quraan Tukufu juu ya namna mwanadamu anavyotakiwa kuishi hapa ulimwenguni unatekelezeka. Yaani hakuna kikwazo cha kimaumbile kinachomzuia mwanadamu kuishi kwa mujibu wa mwongozo wa Quraan Tukufu.
Miongoni mwa tabia njema na mwenendo wa Mtume Muhammad ambazo tunatakiwa kuziiga na kujipamba nazo ni ukweli na uaminifu.
Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) jamii yake ilikubaliana kwa kauli moja kuwa alikuwa mkweli kwa kiwango cha kutopata kusema uongo hata kwa jambo la utani na muaminifu kiasi wanajamii, watoto kwa wakubwa, wenye mitazamo na hadhi tofauti tofauti katika jamii walimuamini na kuweka amana zao kwake.
Ukiangalia umuhimu wa sifa mbili hizi utaona matatizo mengi katika jamii zetu, ikiwemo jamii ya Kitanzania kwa ujumla wake, yanasababishwa na wanajamii kukosa sifa mbili hizi za ukweli na uaminifu.
Lau, ukweli na uaminifu vingetamalaki katika jamii basi tusingeshuhudia ufisadi, ubadhirifu wa mali za umma, wizi na dhuluma za aina mbalimbali katika jamii.
Sifa nyingine ni kutetea wanyonge. Historia ya mji wa Makkah inaonyesha kuwa baada ya babu yake Mtume Muhammad aitwaye Abdul-Mutwalib, aliyekuwa kiongozi aliyeheshimika na koo zote za kabila la Qurayshi, kufariki dunia na nafasi ya kuwaongoza Maqurayshi kuchukuliwa na mwanawe Abuu Talib, kiongozi huyu mpya hakuweza kupata nguvu na hadhi aliyokuwa nayo baba yake kutokana na umaskini aliokuwa nao na baadhi ya koo zilizokuwa na watu wengi matajiri na wenye nguvu kufanya jeuri kubwa na dhuluma isiyo na mfano kwa kuwaonea wanyonge na kupora walichonacho kiasi mwenye nguvu na uwezo wa kujitetea kwa silaha ndiye tu aliweza kuishi kwa amani na furaha.
Hali ya dhuluma na manyanyaso ilipozidi Ami yake Mtume aitwaye Zubeir bin Abdil Mutwalib aliwaita wakubwa wa koo za Kiqurayshi na kuwashauri kuanzisha chama cha kuwatetea na kuwalinda wanyonge na kila namna ya udhalimu waliokuwa wakifanyiwa na wale wenye nguvu.
Koo tano kati ya koo kumi na mbili za Kiqurayshi zilikubali suala hili la kuanzisha chama kitakachowasaidia wasiojiweza bila ya kujali ukoo wao au kabila lao na kumsaidia kila mwenye kudhulumiwa na kufanya kila linalowezekana kumrejeshea haki yake. Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) akiwa na umri wa miaka 20 (alipewa Utume akiwa na miaka 40) alionyesha utayari wake wa kupigania haki za wanyonge na kuchukia dhuluma dhidi ya utu na heshima ya mwanadamu kwa kushiriki kikamilifu na kutoa ushauri wake katika kuunda chama hiki.
Hata baada ya kupewa Utume, Mtume Muhammad alikuwa akifurahi sana kila alipokumbuka kuwa yeye alikuwa miongoni mwa wanachama wa Chama cha Kuwatetea Wanyonge na alikuwa akisema: “Niliyapenda makubaliano ya chama hicho kuliko ngamia mwekundu na mpaka sasa hivi nakubaliana na madhumuni hayo”.
Harakati za Mtume Muhammad katika kuasisi na kushiriki katika shughuli za chama hiki ni kielelezo cha tabia yake, tangu utotoni, ya kuwahurumia wanyonge na kusaidia utatuzi wa matatizo ya wanajamii.
Mtume Muhammad alifurahi sana kuwepo kwa chama hiki ambacho kilibeba matarajio ya kutatua tatizo sugu la dhuluma katika jamii.
Ni dhahiri kuwa tabia hii tukufu ya kuchukia dhuluma na ukatili dhidi ya wanyonge inapaswa kuigwa na kila mwanajamii na kurithishwa kizazi hadi kizazi kwani baadhi ya wanajamii wamekuwa na tabia ya kutotilia maanani dhuluma, uonevu na ukatili wanaofanyiwa watu wengine wakiamini hilo ni tatizo lao hao wanaodhulumiwa  na wao  haliwahusu.
Wakati mwingine kutoa msaada wa kufanikisha dhuluma dhidi ya anayedhulumiwa. Mwanajamii anapopuuza dhuluma inayofanywa kwa wengine kwa kudhani yeye yupo salama anakuwa hakukizingatia kisa cha ngombe watatu; mwekundu, mweupe na mweusi ambao simba aliona hawezi kuwashambulia wakiwa wamoja, hivyo kuwarubuni ngombe mwekundu na mweusi kwamba hana tatizo nao bali tatizo lake ni ngombe mweupe anayejidai nao wakadanganyika na ngombe mweupe akaliwa na simba huku akilia kwa mshangao wa kukosa msaada wa ndugu zake.
Lililofuata ni kurubuniwa ngombe mwekundu kuwa yeye rangi yake inafanana na simba hivyo hana tatizo isipokuwa yule ngombe mweusi, naye akadanganyika na hakutoa msaada kwa ngombe mweusi alipovamiwa na kuliwa.
Hatimaye, siku ya kuvamiwa na kuliwa ngombe mwekundu ndipo alipolia na kutamka maneno yenye hekima kubwa kuwa: “Mimi siliwi leo bali nililiwa siku ya kwanza tulipomsaliti ngombe mweupe na kuvunja kiapo cha ndugu kusaidiana.” Ukikizingatia kisa hiki cha ngombe utabaini falsafa ya mafundisho ya Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) aliposema: “Msaidie ndugu yako akiwa mwenye kudhulumu au mwenye kudhulumiwa”.
Mtu mmoja akauliza: “Ee Mtume wa Mwenyezi Mungu, ninaweza kumsaidia mtu aliyedhulumiwa, lakini nitawezaje kumsaidia dhalimu? Mtume akasema: “Mzuie asifanye vitendo vya dhuluma. Huo utakuwa ndio msaada wako kwake”.
Hivyo utaona kuwa tunapaswa kumuiga Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) kwa kupinga kila aina ya dhuluma na uonevu katika jamii na pia kuhakikisha tunashiriki katika harakati za kuwasaidia wanyonge na wenye kudhulumiwa kama Mtume Muhammad aliposhiriki katika Chama cha Kuwatetea Wanyonge katika mji wa Makkah.
Na unapozingatia kuwa haya aliyafanya akiwa kijana wa miaka 20 kabla ya hata kupewa Utume inadhihirika kule kuthamini kwake utu na kupinga tabia za kinyama katika jamii.
Tabia nyingine ni huruma hususan kwa watoto. Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) alikuwa mwenye kuwapenda na kuwahurumia watoto na akiwabusu (ada ya Waarabu kuonyesha heshima, upendo na huruma).
Siku moja akiwa na Al-Aqraa bin Haabis Al-Tamiimy Mtume alimbusu mjukuu wake Hassan bin Ali bin Abi Twalib. Al-Aqraa akistaajabu hilo alisema: “Hakika mimi nina watoto kumi na sijapata kumbusu yeyote miongoni mwao. Mtume Muhammad alimtazama na kumwambia: “Asiye na huruma hatahurumiwa”.
Kuwa na huruma na kuwahurumia viumbe wengine wakiwemo binadamu na hususan watoto ni tabia ya Mtume Muhammad inayopaswa kuigwa na jamii.
Ni dhahiri kuwa kuongezeka kwa vitendo vya ukatili dhidi ya watoto ikiwemo kutekwa (watoto kuibiwa), kubakwa, kuadhibiwa kiukatili na mengineyo ni ushahidi wa wazi kuwa jamii imepungukiwa huruma kwa kiasi kikubwa.
Kwamba mtu anafikia kumchoma mtoto eti ndiyo anamuadhibu kwa kosa la wizi au kupoteza pesa, anamuua mtoto kwa ugomvi usiomhusu baina ya muuaji na mwenza wake, ni mambo yanayoonesha si tu kukosekana huruma katika jamii bali pia kupungua utu wa mwanadamu.
Nimalizie makala hii kwa kuinasihi jamii kufuata tabia za utu alizojipamba nazo Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) ikiwemo tabia ya ukweli na uaminifu katika miamala yetu, iwe katika ngazi ya familia, majirani, sehemu za kazi na pia kwa yale yanayohusu masilahi ya taifa na usalama wake. 
Kadhalika tuongeze juhudi katika kuhakikisha jamii inachukia dhuluma na uonevu dhidi ya watu na masilahi yao.  Jamii itafakari athari ya kunyamazia dhuluma na uonevu katika jamii kwa dhana kuwa hayo ni mambo binafsi ya wanaodhulumu au kudhulumiwa.
Na kwa namna ya kipekee, jamii haina budi kuchukua hatua za kurejesha utu na huruma mahala pa unyama na ukatili.
Shime tuige tabia njema alizojipamba nazo Mtume Muhammad ambazo zinaendana na utu mwema wa mwanaadamu, kwani Mwenyezi Mungu ametuhakikishia kuwa yeye ni ruwaza njema (mfano mwema/kiigizo chema) kwetu.

Sheikh Khamis Mataka ni Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata). Simu: 0713603050/0754603050

Mwisho