Kila mtu anapaswa kufurahi na kujivunia mazingira anayoishi. Tunapaswa kukuza ndani yetu uwezo wa kushangaa, kufurahia na kumshukuru Mungu kwa kazi nzuri ya uumbaji. Tukazane kumwona Mungu kupitia viumbe vyake kwa kuviona kuwa vinawakilisha sura ya Mungu.
Tukiona kujifunua kwa Mungu katika kila kitu, tunaonja uwepo wa Mungu katika kila kitu na kila mahali. Papa Fransisko anasema: “Kwa kuutazama ukuu na uzuri wa vilivyoko duniani tunapata kumfahamu aliyeviumba.” Mazingira ni kama kitabu ambacho Mungu  anazungumza nasi kupitia kwacho, akidhihirisha urembo na uzuri wake kwetu sisi. 
Imani  inaturuhusu  kuona  kila mahali dalili za kazi ya Mungu na kuelewa kwamba  yupo  kati  yetu, katika maisha  yetu ya kiroho, kimwili na kihisia. Imani inaturuhusu kumwona Mungu katika  shani ya asili, ambapo tunaweza tukaendelea kugundua uwepo wake katika viumbe mbalimbali.
Binadamu anabakia kuwa kiumbe wa pekee katika uumbaji, lakini atathibitisha kuwa ni kiumbe wa pekee katika uumbaji kama anaishi kwa kuyatunza, kuyalinda na kuyapenda mazingira anayoishi na asiyoyaishi. Tuamshe tabia ya kuyapenda mazingira yetu. Binafsi naamini kwamba, kama unajipenda wewe mwenyewe ni lazima utakuwa unayapenda na mazingira yako unayoishi.
Unatakiwa kuyapenda mazingira yako. Wafundishe wanafamilia wako, marafiki zako, wafanyakazi wenzako, wanafunzi wako, waamini wako umhimu na faida za kutunza mazingira.
Fransisko wa Asizi, ni Mtakatifu anayeheshimika sana ndani ya Kanisa Katoliki. Enzi za uhai wake, mtawa huyu alikuwa rafiki wa mazingira. Fransisko wa Asizi alitunga utenzi wa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya mazingira. Utenzi huo aliupa jina la Kaka na dada mazingira.
Fransisko aliyatazama mazingira kama dada yake na kaka yake. Fransisko aliyatazama mazingira kama ndugu. Alitambua umhimu na  uwepo wa mazingira. Aliyapenda mazingira aliyoishi. Aliyatazama maajabu ya Mungu kupitia mazingira aliyoishi. Tunalo jukumu la kuyatazama mazingira kama ndugu yetu.
Rafiki mwingine wa mazingira alikuwa Mt. Martin de Porres. Huyu alikuwa ni mtawa wa Kanisa Katoliki.  Aliyapenda sana mazingira. Siku moja alikwenda ziwani akawaita samaki wote wa ziwani, wakaitikia wito wake, wakaja akawahubiria habari njema ya wokovu. Inasemekana kuwa samaki wale walimsikiliza mpaka alipomaliza mahuburi. 
Kwa hakika tunahitajika kumwomba Mwenyezi Mungu msamaha kwa kutoyatunza mazingira yake vizuri.  Vyanzo vingi vya maji vimekauka kwa sababu ya uharibifu wa mazingira. Wanyama wa mwituni wanateseka na wengine wanakufa kwa kukosa malisho kwa sababu ya uharibifu wa mazingira unaofanywa na shughuli za kibinadamu.  Inatosha kukanusha kwamba si kweli kwamba  mwanadamu kukabidhiwa mamlaka na dhamana  ya kuyatunza na kuyalinda  mazingira ni kigezo cha kutumia apendavyo kila kinachomzunguka. Inatosha kusema: “Mwanadamu ni mshika pembe tu na mchinjaji ni mwingine”.
Ninaamini kipimo cha kwanza cha jamii iliyostarabika ni matokeo ya kuishi tunu za  maadili bora na utunzaji bora wa mazingira.  Maadili ya mtu binafsi au ya taifa hayaoti yenyewe kama uyoga, lazima yajengwe, yaendelezwe na yalindwe  na  watu  waliodhamiria kufanya hivyo.
Kimsingi, ili jamii yoyote iweze  kuendelea  kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni  utunzaji bora wa mazingira ni chachu katika kufanikisha hatua ya namna hiyo. Jamii yoyote ile isiyoyapenda mazingira yake haiwezi kuzaa matunda chanya katika ulimwengu wowote ule. 
Tushirikiane kutunza mazingira yetu kuanzia kwenye ngazi ya familia, taasisi binafsi, sehemu za kazi na taifa. Ni rahisi  kulaumu, kushutumu na kutupia wengine  lawama.  Lakini kama kweli tunataka kuimarisha ubora wa mazingira yetu tunayoishi ni lazima tushirikiane kuyalinda na kuyatunza.  
Msingi  imara  hujengwa kuanzia chini. Dunia ya leo inaishi  katika  kipindi cha utumwa wa kimaadili. Jambo hili la mwanadamu  kuishi katika kipindi cha  utumwa wa kimaadili halijatokea kwa bahati mbaya. Limeruhusiwa liote  mizizi na kuchipuka kwa juhudi za binadamu  mwenyewe. Kwa bahati mbaya jambo hili limegeuka na kuwa mwiba kwa mwanadamu. Linamtesa usiku na mchana. Ni hakika kwamba, tukiruhusu dunia yetu ikageuka kuwa jangwa, tutateseka zaidi ya utumwa wa kimaadili.
 
Itaendelea… 

522 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!