Kwa muda wa mwezi mzima wananchi wa Mkoa wa Mtwara wapo kwenye maandamano. Maandamano haya yanaelekea kulifikisha taifa katika uvunjifu wa amani. Wananchi wanatumia nguvu, na kuna uwezekanao Serikali nayo itafika mahala itaishiwa uvumilivu itaanza kutumia nguvu. Mungu apishe mbali.

Sisi baada ya kupitia hoja za kila upande kwa kina, tunadhani tunao ufumbuzi wa tatizo hili. Ni kwa bahati mbaya kwamba maeneo mengi ya nchi hii madini yamekuwa yakigunduliwa, wawekezaji wanachimba na kuchukua kila kitu tunaachiwa mashimo. Hali kama hii imeshuhudiwa huko Tarime, Geita na Biharamulo.


Wananchi wamefika mahala sasa wanajiuliza kuna faida gani ya kumiliki ardhi, lakini yakipatikana madini katika eneo lako, iwe ni gesi kama ilivyotokea kwa Mtwara, dhahabu au madini mengine umaambulia kitu kinachoitwa fidia. Fidia yenyewe inayotolewa urefu wake ni sawa na mkia wa mbuzi.

Hii imewafanya Wanamtwara kuamua kuhoji. Tunapenda kuamini kuwa Mtwara wanahoji uhalali wa gesi kupelekwa Dar es Salaam si kwa shinikizo la kisiasa, mtu yeyote awaye au mashirika ya kimataifa yasiyopenda kuona gesi ikichimbwa, maana taarifa hizi zimeanza kutufikia pia. Inaelezwa yapo makundi yanapenyeza rupia kutengeneza vurugu.


Tumezisikia vurugu za mwishoni mwa wiki na mauaji yaliyoambatana nazo. Pamoja na kwamba tunatetea haki ya Wanamtwara kupata faida ya gesi, lakini tunasisitiza kuwa vurugu hazina tija. Utamaduni wa Watanzania kuwindana na polisi kama digidigi kuuana hautatufikisha popote. Tunajenga chuki zisizoweza kutusaidia lolote katika kufanikisha ajenda husika.


Sisi wa Jamhuri tunapendekeza kuwa kama sehemu ya kumaliza mgogoro huu, Sera ya Gesi itamke bayana kuwa mapato yote yanayotokana na gesi walau kiasi cha asilimia 2, itakizwa Mtwara. Kiundwe chombo ha kusimamia fedha hizi maana zitakuwa nyingi, na zitumike kutoa huduma za jamii kama maji, barabara, hospitali na shule. Sera hii ya asilimia 2 ipitishwe si kwa gesi tu, bali kwa madini yote nchini. Mungu ibariki Tanzania.

By Jamhuri