



Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango leo tarehe 07 Septemba 2022 amekutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Bodi ya Jumuiya ya Mapinduzi ya Kijani Barani Afrika (AGRA) ambaye ni Waziri Mkuu Mstaafu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn, mazungumzo yaliofanyika kando ya Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Kigali nchini Rwanda.
Katika Mazungumzo hayo, Makamu wa Rais amemueleza Desalegn dhamira ya serikali ya awamu ya sita ya kuinua sekta ya kilimo hususani kuongeza uzalishaji pamoja kuwavutia zaidi vijana na wanawake ambao ni idadi kubwa iliopo kushiriki katika sekta hiyo. Amesema serikali imeongeza bajeti katika sekta ya kilimo kutoka bilioni 294 mwaka 2021/2022 hadi kufikia bilioni 751 mwaka 2022/2023 ambapo uzalishaji wa mbegu bora na uazishwaji wa skimu za umwagiliaji ukiendelea.
Aidha amesema serikali imeanzisha Program maalum iitwayo “Building Better Tomorrow” ambayo inawalenga wanawake na vijana kushiriki katika kilimo ambapo pamoja na mambo mengine imelenga kuanzisha miradi kilimo cha biashara kuanzia 12000 katika vijiji 12000 nchi nzima hivyo ni muhimu jumuiya na taasisi zinazoendeleza kilimo ikiwemo AGRA kuunga mkono ajenda hiyo.
Makamu wa Rais amesema Tanzania imebarikiwa kuwa na ardhi pamoja na eneo zuri la kijiografia ambalo linaweza kutumika katika kuchangia usalama wa chakula barani Afrika hivyo kuwakaribisha wawekezaji katika sekta ya kilimo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Jumuiya ya Mapinduzi ya Kijani Barani Afrika (AGRA) ambaye ni Waziri Mkuu Mstaafu wa Ethiopia Mheshimiwa Hailemariam Desalegn Amesema AGRA inaunga mkono jitihada za Tanzania katika kuinua sekta ya kilimo na ipo tayari kushirikiana na taasisi zingine katika ufadhili wa programu mbalimbali za miradi ya kilimo ikiwemo “Building Better Tomorrow”.
Aidha ameongeza kwamba sekta ya kilimo barani Afrika inapaswa kuendana na maendeleo ya teknolojia kwa kuwekeza katika teknolojia rafiki ili kuweza kufanya kilimo cha kisasa, kufanya uzalishaji bora na baadae kuweza kuvutia vijana zaidi.
Katika hatua nyingine Makamu wa Rais amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Rwanda Mheshimiwa Paul Kagame, mazungumzo yaliofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Kigali nchini Rwanda. Mazungumzo hayo yamefanyika kabla ya kuanza kwa mkutano wa wakuu wa nchi na serikali wanaoshiriki majadiliano katika mkutano wa Mapinduzi ya Kijani Barani Afrika leo tarehe 7 Septemba 2022.
Pia Makamu wa Rais amefanya mazungumzo na Rais mteule wa Mfuko wa Ufadhili wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) Alvaro Lario, Mazungumzo yaliofanyika kando ya Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Kigali nchini Rwanda.
Mazungumzo hayo yamelenga kuongeza ushirikiano baina ya Tanzania na Mfuko huo kwa lengo la kuendeleza miradi mbalimbali inayotekelezwa kwa lengo la kuendeleza sekta ya kilimo nchini Tanzania.
Kamishina Mkuu wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR), Bw. Filippo Grandi yupo nchini tokea tarehe 24 Agosti 2022 kwa ziara ya kikazi ambapo pamoja na mambo mengine, atafanya mazungumzo na viongozi wakuu wa Serikali na kutembelea Kambi za Wakimbizi mkoani Kigoma.
Bw. Grandi ambaye jana ametembelea Kambi ya Wakimbizi ya Nyarugusu ya mkoani Kigoma na baadaye kuwasili mkoani Dodoma na kupokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula ameelezea kuridhishwa kwake na huduma bora zinazotolewa kwa Wakimbizi ukilinganisha na miaka mitatu iliyopita alipofanya ziara kama hiyo mwaka 2019.
Kwenye Kambi ya Nyarugusu, ambayo inahifadhi Wakimbizi zaidi ya 130,000 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Burundi,Bw. Grandi alijionea hali halisi ya maisha ya wakimbizi hao na kusikiliza maelezo ya wawakilishi wao pamoja na taasisi mbalimbali zinazohudumia wakimbizi.
Baada ya kusikiliza maelezo, Bw Grandi aliahidi kuwa UNHCR itaendelea kushirikiana na wadau ikiwemo Serikali Ili kuboresha maisha ya wakimbizi pamoja na kukabiliana na athari zitokanazo na shughuli za wakimbizi kama vile uharibifu wa mazingira.
Ziara ya Bw. Grandi nchini imekuja kufuatia mazungumzo yake aliyofanya na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan jijini New York wakati wa Kikao cha 76 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2021.
Na Edward Kondela,JamhuriMedia,Morogoro
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki (Mb) amezitaka halmashauri na mamlaka za serikali za mikoa kuhakikisha zinatekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan la kutenga maeneo kwa ajili ya wafugaji ili kukuza sekta hiyo na kuepusha migogoro ya matumizi bora ya ardhi.
Waziri Ndaki amebainisha hayo Agosti 19, mwaka huu alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja katika Wilaya ya Malinyi Mkoani Morogoro na kuzungumza na wakulima na wafugaji katika vijiji vya Tanga na Njiwa, ambapo amesema serikali ina nia nzuri ya kuendeleza Sekta ya Mifugo na kuzitaka halmashauri hizo na mamlaka za serikali za mikoa kutekeleza agizo hilo huku akiwataka wafugaji kutolisha mifugo yao kwenye mashamba ya wakulima.
Ameongeza kuwa serikali pia imeelekeza maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya malisho kuanzia ngazi ya kijiji ambayo hayajasajiliwa, yanatakiwa kutambuliwa rasmi na kusajiliwa pamoja na kulindwa na kuhakikisha yanatumika kama ilivyopangwa kwa ajili ya kulishia mifugo pekee pamoja na kuwataka wafugaji kutoingiza mifugo yao kwenye maeneo ya hifadhi na mapori tengefu.
“Halmashauri na mamlaka za serikali za mikoa zinapaswa kuyalinda maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya wafugaji, kama yapo maeneo yaliyotengwa na kijiji au kata kwa ajili ya malisho hayo maeneo yasajiliwe rasmi kuzuia migogoro.” Amesema Mhe Ndaki.
Aidha amewaarifu wafugaji kuwa kufuatia taarifa zilizotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), wizara inatoa tahadhari kwa wafugaji za taarifa zinazoonesha kumekuwepo na vipindi virefu vya ukavu vilivyojitokeza katika kipindi cha Mwezi Machi na Aprili mwaka 2022 hali ambayo inatishia upungufu wa malisho ya mifugo pamoja na maji.
Amesema kufuatia hali hiyo wafugaji wategemee ukame hivyo wawe na tahadhari ya kuvuna mifugo na kubakiza ile inayoweza kutunzwa vizuri kutokana na kiasi cha malisho alichonacho mfugaji pamoja na maji.
“Tuchukue tahadhari ya kuvuna mifugo yetu tusije kukutana na ukame halafu tukaanza kulalamika mifugo imeanza kuwa dhaifu au kufa huku tulikuwa tukijua ni vizuri ukapunguza kwa kuvuna mifugo yako na kubaki na ile itakayotosheleza malisho uliyonayo pamoja na maji.” Amesema Mhe. Ndaki
Katika ziara hiyo ya kikazi ya siku moja ya Waziri Ndaki, Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Mathayo Maselle amezungumzia skimu ya umwagiliaji iliyopo Kijiji cha Njiwa na Itete ambayo imetengwa maalum kwa ajili ya kilimo imekuwa na changamoto ya wafugaji kuingiza mifugo yao katika eneo hilo jambo ambalo limekuwa likisababisha migogoro.
Hata hivyo kufuatia changamoto hiyo Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki ameutaka uongozi wa wilaya kwa kushirikiana na wakulima na wafugaji kutengeneza mfereji utakaosafirisha maji kutoka kwenye skimu hiyo hadi eneo lingine watakalolitenga kwa ajili ya kunyweshea mifugo maji badala ya mifugo hiyo kupita kwenye mashamba ya wakulima kwenda kunywa maji.
Nao baadhi ya wananchi waliohudhuria ziara ya Waziri Ndaki wametoa maoni kadhaa yakiwemo ya utatuzi wa migogoro ya wakulima na wafugaji kutokana na matumizi bora ya ardhi pamoja na kuomba uwepo wa mpaka maalum wa skimu ya umwagiliaji ya vijiji vya Itete na Njiwa ili wakulima waweze kufanya shughuli zao hali kadhalika wafugaji wapate huduma ya maji ya mifugo yao bila kuingiza mifugo kwenye mashamba ya wakulima.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki amefanya ziara ya kikazi ya siku moja katika Wilaya ya Malinyi Mkoani Morogoro na kuzungumza na wakulima na wafugaji ambapo amesema baadhi ya kero serikali inaendelea kuzifanyia kazi ili kuhakikisha inaondoa migogoro kati yao na kuwahamasisha wafugaji kujitokeza kwa wingi kuhesabiwa katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi litakalofanyika Jumanne ijayo Tarehe 23 Mwezi Agosti.
Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia
Wakala wa Nishati Vijijini (REA),hadi sasa umetumia takribani Shilingi trilioni 3 kwa ajili ya kazi ya kupeleka miradi ya umeme vijijini ili kuhakikisha nishati ya umeme inafika na kutumika kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwemo ya uzalishaji, kuboresha huduma na shughuli za kiuchumi.
Hayo yamesemwa jana na Mkurugenzi Mkuu wa REA Mhandisi Hassan Saidy wakati wa mkutano wa Wakala huo na wadau wake kuelezea masuala mbalimbali ya nishati vijijini uliorushwa mubashara na kituo cha televisheni cha Azam ambapo amesisitiza kuwa mradi unaoendelea hivi sasa (mradi wa usambazaji umeme vijijini awamu ya tatu mzunguko wa pili) pekee unagharimu kiasi cha shilingi trilioni 1.2.
Mhandisi Saidy ameongeza kuwa, kutokana na kazi zinazoendelea na mipango waliyoijiwekea, vijiji vyote nchini vitapata umeme kabla ya muda ulioelekezwa (mwaka 2025).
“Ilani ya Uchaguzi ya CCM imeahidi kufikisha umeme katika vijiji vyote ifikapo mwaka 2025, sisi kama REA hatutafika huko, tutakamilisha vijiji vyote kuvipatia umeme kabla ya mwaka huo” alisema Mhandisi Saidy na kuongeza kuwa
“Wananchi wakipata nishati ya umeme itasaidia sana katika uhifadhi wa mazingira, kwani hivi sasa zaidi ya asilimia 90 ya Watanzania wanatumia kuni na mkaa jambo ambalo linapelekea kuathiri mazingira kwa kuharibu misitu. Takwimu zinaeleza kuwa kwa mwaka mmoja, Tanzania inapoteza hekta 400 za misitu”
Ameendelea kwa kusema kuwa, REA inatumia gharama kubwa kupeleka miradi ya umeme vijijini hivyo amewataka wananchi wa vijijini kuchangamkia fursa hiyo kwa kuutumia kwa shughuli za kiuchumi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Sera, Mipango na Utafiti wa REA , Mhandisi Elineema Mkumbo, amesema hali ya upatikanaji wa umeme vijijini imepanda kutoka asilimia 2 mwaka 2007 hadi kufikia asilimia 69.6 kufikia mwaka 2020. “Lengo letu ni kuhakikisha vijiji na vitongoji vyote nchini vinapata umeme nyumba kwa nyumba.
Mhandisi Mkumbo ameeleza kuwa, kazi ya kupeleka umeme vijijini inaenda sambamba na kupeleka umeme katika vitongoji ambapo hadi sasa zaidi ya vitongoji 27,000 vimepatiwa umeme.
Naye Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi wa REA, Mhandisi Jones Olotu ameeleza kwamba, kufuatia kasi ya upelekaji miradi ya umeme vijijini na nishati hiyo kuwafikia wananchi wengi wa vijijini, Tanzania imeweka rekodi na kuongoza katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara ambao wananchi wake wamepunguza kuhama kutoka vijijini kwenda mijini na badala yake watu mijini kuhamia vijijini kwa ajili ya kufanya shughuli mbalimbali.
“Tanzania imekuwa nchi ya kwanza kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara kwa kubadilisha mtazamo wa watu kuhama kutoka vijijini kuja mjini, siku hizi ni kawaida kabisa watu wanahama kutoka mjini na kuhamia vijijini” alisema Mhandisi Olotu.
Mhandisi Olotu amebainisha kwamba, matokeo ya kasi ya upatikanaji umeme vijijini hivi sasa ni matokeo ya REA kuandaa mipango kabambe na mikubwa ukiwemo mpango mkubwa wa miaka mitano wa kupeleka umeme katika vijiji vyote nchini ambao REA inaendelea kuutekeleza huku vipaumbele vikiwa ni taasisi za umma ikiwemo zahanati, shule, vituo vya maji, polisi, nyumba za ibada kwa lengo la kuboresha huduma za jamii.
Akichangia katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Uendelezaji Masoko na Teknolojia wa REA, Mhandisi Advera Mwijage amesema, kazi ya REA syo tu kupeleka umeme vijijini bali ni kupeleka nishati mbalimbali vijijini ili ziweze kutumika na wananchi wa maeneo hayo katika shughuli mbalimbali ambapo katika kusambaza gesi asilia kwa ajili ya matumizi ya majumbani wanashirikiana na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na kazi hiyo wanaifanya katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Pwani.
Mhandisi Mwijage ameongeza kuwa, katika maeneo ya visiwa, REA imekuwa ikitumia nishati ya jua katika kupeleka miradi ya umeme ili kuhakikisha visiwa vyote nchini vinapata nishati hiyo ambapo kwa sasa mpango uliopo ni kuvipelekea umeme visiwa 36.
“Tanzania tuna visiwa 196, visiwa 53 havina makazi ya kudumu, vyenye makazi ya kudumu ni 143. Kati ya visiwa 143 vyenye makazi ya kudumu, visiwa 72 vina umeme na visiwa 71 havina umeme. Tulianza na visiwa 20 kuvipelekea umeme na sasa tuna mpango wa kupeleka umeme katika visiwa 36” alisisitiza Mhandisi Mwijage.
Akizungumzia suala la mawakala wa wauzaji mafuta vijijini ambao watakopeshwa ili kutoa huduma hiyo kwa wananchi wa vijijini, Mhandisi Mwijage amesema
“Kitu kikubwa kitakachozingatiwa kwa wauzaji na vituo vya mafuta vijijini ni usalama, mazingira ya kuuzia mafuta, eneo na kituo husika. Watakaokidhi vigezo watawezeshwa kupitia mikopo na lengo letu ni kuhakikisha kwamba katika utekelezaji wa zoezi hili walengwa na wanufaika wote watoke vijijini”
Nao wahariri wa vyombo vya habari Joyce Shebe, Salome Kitomali na Neville Meena wakizungumza katika mkutano huo wameishauri REA kuendelea kutilia mkazo suala la usawa wa kijinsia katika fursa na matumizi ya nishati, kuchangia na kukuza uchumi.
Wakala wa Nishati Vijijini (REA) tangu kuanzishwa kwake mwaka 2007 umekuwa na desturi endelevu ya kukutana na wadau mara kwa mara kueleza na kutoa mrejesho wa masuala mbalimbali ya nishati vijijini lengo likiwa ni kujenga uelewa wa pamoja kwa wadau na mwananchi mmoja juu kazi zinazoendelea kufanywa na Wakala huo.