Muhongo, Maswi wanatisha

 

*Gharama za kuunganisha umeme zakuna wengi

*Migodi yote si hiari tena kulipa kodi ya mapato

*Afuta mashangingi ya bure, vigogo watakopeshwa

*Mnyika, Selasini wawanyoosha wabunge wala rushwa

 

Wananchi wengi wameeleza kufurahishwa na msimamo wa uongozi mpya wa Wizara ya Nishati na Madini wa kuwapunguzia wananchi ukali wa gharama za kuunganisha umeme, kufuta ununuzi wa mashangingi na kuwabana wenye migodi mikubwa kuanza kulipa kodi ya mapato.

 

 

Furaha ya wananchi pia imekolezwa na msimamo wa wabunge wengi kutoka vyama vyote, bila kujali itikadi zao, kusimama kidete kuwazima baadhi ya wenzao wanaotuhumiwa kuhongwa ili kuwang’oa viongozi wakuu wa Wizara ya Nishati na Madini.

 

Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema) alikuwa wa kwanza na akafuatiwa na wabunge kama Joseph Selasini (Rombo-Chadema), Anne Kilango-Malecela (Same Mashariki-CCM) na Ally Kessy (Nkasi Kaskazini-CCM).

 

Mikakati ya Kupunguza Gharama za Kuunganisha Umeme kwa Wateja

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, ikiwa ndiyo bajeti yake ya kwanza kusoma bungeni, aliwakuna wabunge na wananchi wengi pale alipotangaza kupunguza gharama za uunganishaji umeme kwa wateja.

 

Aliliambia Bunge; “Moja kati ya vikwazo vinavyokwamisha jitihada za Serikali za kuhakikisha kuwa huduma ya umeme inawafikia wananchi wengi zaidi na kwa kasi kubwa, ni gharama kubwa za kuunganisha umeme na kipato cha wananchi wengi wanaohitaji kupata huduma ya umeme. Gharama hizo zimekuwa kikwazo katika azma ya Serikali ya kutimiza lengo la asilimia 30 ya wananchi watakaounganishiwa umeme ifikapo mwaka 2015.”

 

Aliendelea kusema; “Kwa kuzingatia changamoto hizo, Serikali kupitia Tanesco imedhamiria kupunguza gharama za kuunganisha umeme wa njia moja (single phase) kwa wateja wadogo mijini na vijijini kwa wastani wa kati wa asilimia 30 na 77. Kwa kufanya hivyo, wateja wengi watamudu gharama na hatimaye kuongeza kasi ya kuunganisha umeme.

 

“Kutokana na uamuzi huo wa Serikali, gharama za uunganishaji umeme zitakuwa kama ifuatavyo: kwa wateja watakaojengewa njia moja (single phase) kwenye umbali usiozidi mita 30 bila kuhitaji nguzo, katika maeneo ya vijijini watalipa Sh 177,000 na wa mijini watalipa Sh 320,960 badala ya Sh 455,108 zinazolipwa na wateja hao  kwa sasa. Punguzo hili ni sawa na asilimia 61.11 kwa wateja waishio vijijini na asilimia 29.48 kwa wateja waishio  mijini.

 

“Kwa wateja watakaojengewa njia moja na kuwekewa nguzo moja, katika maeneo ya vijijini watalipa Sh 337,740 na wa mijini watalipa Sh 515,618 badala ya Sh 1,351,884 zinazolipwa na wateja hao kwa sasa. Punguzo hili ni sawa na asilimia 75.02 kwa wateja waishio vijijini na asilimia 61.86 kwa wateja waishio  mijini.

 

“Aidha, kwa wateja watakaojengewa njia moja na kuwekewa nguzo mbili katika maeneo ya vijijini watalipa Sh 454,654 na wa mijini watalipa Sh 696,670 badala ya Sh 2,001,422 zinazolipwa na wateja hao kwa sasa. Punguzo hili ni sawa na asilimia 77.28  kwa wateja waishio vijijini na asilimia 65.19 kwa wateja waishio  mijini. Viwango hivyo vya gharama vitaanza kutumika Januari, 2013.”

 

Alisema Serikali imeanzisha utaratibu wa kugharimia miundombinu ya kuwafikishia umeme wateja kwa miradi inayopata ruzuku kutoka Mfuko wa Nishati Vijijini (REF). Utaratibu huo utatumika kwa wateja watakaokuwa wamefunga nyaya za umeme kwenye nyumba katika maeneo ya miradi husika.

 

“Mpango huo utapunguza gharama za kuunganishiwa umeme kwa wastani wa asilimia 80 kulingana na idadi ya nguzo na mfumo utakaotumika (yaani single au three phase). Idadi ya wateja wa awali watakaounganishiwa umeme kupitia mpango huo ni 100,000,” alisema.

 

Migodi kulipa kodi ya mapato

Kwa miaka mingi kilio cha wabunge na wananchi kwa upande wa migodi, pamoja na mambo mengine, ni kuona kuwa migodi inalipa kodi ya mapato.

 

Kwa kulitambua hilo, Profesa Muhongo akasema; “Ili nchi yetu iweze kunufaika zaidi na shughuli za uchimbaji mkubwa wa madini, mikakati iliyopo ni pamoja na kuhakikisha kuwa migodi inaendelea na mingine inaanza kulipa kodi ya mapato na gawio kwa migodi ambayo Serikali ina hisa.

 

“Kabla mgodi haujaruhusiwa na Serikali kujengwa, wamiliki wake wanawajibika kuwasilisha taarifa za upembuzi yakinifu zinazoonyesha gharama za uwekezaji, muda wa mgodi kurudisha gharama na muda wa kuanza kulipa kodi ya mapato. Kimsingi, taarifa hizo ndizo zinazotumiwa na Serikali kufikia uamuzi wa kuingia mkataba wa uendelezaji mgodi na kampuni husika.”

 

Alisema bei ya dhahabu katika soko la dunia imeendelea kupanda kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na kiwango cha nyuma wakati migodi inaanzishwa. Hali hiyo inawezesha muda wa urejeshaji gharama za uwekezaji kupungua na hivyo kuanza kulipa kodi ya mapato mapema.

 

Hata hivyo, licha ya kupanda kwa bei ya dhahabu katika soko la dunia, baadhi ya migodi haijaanza kulipa kodi ya mapato kwa madai kwamba haijarudisha gharama za uwekezaji.

 

Akaagiza; “Hivyo, Serikali kupitia Wakala wa Ukaguzi wa Madini kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato (TRA) itaendelea kukagua na kuhakiki gharama za uwekezaji na uendeshaji kwenye migodi mikubwa na ya kati ili kuhakikisha kodi hizo zinalipwa mapema.

 

“Napenda kutoa rai kuwa migodi yote ianze kulipa kodi ya mapato bila kuleta visingizio kuwa hawajarudisha gharama au wanapata hasara pamoja na muda walioonyesha kwenye taarifa za upembuzi yakinifu kufika.

 

Bei zilizoainishwa kwenye taarifa za upembuzi yakinifu kwa wakati huo ni ndogo mara tano ya bei ya sasa, hali inayoashiria kuwa migodi imerudisha gharama za uwekezaji mapema kuliko inavyokadiriwa kwani gharama za uendeshaji haziwezi kupanda sawa na bei ya dhahabu inavyopanda.

 

“Ni matumaini yangu kuwa kama mwekezaji ameendelea kuchimba kwa muda wa miaka mitano hadi saba, ameshapata faida na kurejesha gharama zake. Kwa kuzingatia hali hiyo, kupitia Bunge Tukufu, naagiza kampuni zote zilizochimba madini kwa miaka mitano na kuendelea, zianze kulipa kodi ya mapato bila kuleta visingizio.

 

“Na kama kampuni bado inapata hasara na haiwezi kuchangia katika uchumi wa Taifa kwa kulipa kodi ya mapato, ifunge mgodi wake na kuondoka kwa kuwa madini hayaozi. Haiwezekani kukaa miaka saba unaendelea kupata hasara, lakini upo. Serikali itaendelea kushirikiana na kampuni zilizo tayari kuanza kulipa kodi ya mapato kwa wakati bila masharti.”

 

Magari ya umma kufutwa, sasa watakopeshwa

Katika hatua nyingine ya kutia matumaini, Profesa Muhongo akatangaza kuwa wizara yake imenuia kwa dhati kupunguza gharama za “mashangingi”, na kwamba kuanzia sasa watumishi wenye sifa watakopeshwa magari.

 

Akaliambia Bunge; “Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza mpango wa Serikali wa kupunguza matumizi ya fedha za umma, hasa katika ununuzi wa magari yenye gharama kubwa, napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kwamba Wizara yangu itatekeleza kwa dhati agizo la Mheshimiwa Waziri Mkuu la kudhibiti matumizi ya magari ya aina hiyo kuanzia mwaka 2012/13.

 

“Katika utekelezaji huo, viongozi waandamizi wa Wizara wakiwamo makamishna na wakurugenzi waliokuwa wanahudumiwa na magari ya gharama kubwa, wataanza kutumia magari ya kawaida ambayo ujazo wa injini hautazidi sentimita za ujazo (CC) 3,000 kwa utaratibu wa kukopeshwa.

 

“Mpango huo utawezesha Wizara kuokoa zaidi ya shilingi bilioni 1.4 kwa mwaka. Fedha hizo zitatumika katika shughuli nyingine za maendeleo. Aidha, mpango huo utapunguza matumizi ya magari ya Serikali baada ya saa za kazi na siku ambazo siyo za kazi”.

HOTUBA KAMILI YA WAZIRI WA NISHATI NA MADINI KWA MWAKA 2012/2013 soma UK. 7-15