Ni kawaida kwa vijana kuomba kazi katika ofisi za mashirika na taasisi mbalimbali za serikali na zisizo za kiserikali zenye mazingira mazuri kiutendaji, lakini  imekuwa tofauti kwa vijana hao  kuomba kazi katika Chumba cha Kuhifadhia Maiti (mochari).

 

Hatua hiyo inanifanya niwe na shauku ya kutembelea katika Chumba cha Kuhifadhia Maiti cha Hospitali ya Taifa Muhimbili. Napiga moyo konde na kwenda katika hospitali hiyo, nakutana na Afisa Habari wa Hospitali hiyo, Aminiel Aligaesha, naye ananipeleka kwa Mkuu wa Idara, Dk. Emmael Moshi.

 

Dk. Moshi ananipokea na baada ya maongezi yetu ananipeleka katika Chumba cha Kuhifadhia Maiti cha Hospitali hiyo.  Katika chumba hicho nakutana na watu wanne wananipokea kwa uchangamfu mkubwa.

Baada ya salamu, Dk. Moshi anitambulisha kwa Mhudumu Mkuu wa chumba hicho, Gogo Mzome Abdadalah.

 

Mzome naye akiwa ameshika daftari lililoandikwa majina ya maiti zilizoletwa kwa ajili ya kuhifadhiwa ananikaribisha kwa uchangamfu  mkubwa “Karibu kaka mkubwa, jisikie nyumbani lakini kikazi sio katika huduma  yetu,” anasema huku akicheka kwa bashasha.

 

Mzome (56), mrefu, mnene wa wastani na mcheshi kwa kipindi chote baada ya maongezi ya saa moja ananyanyuka kitini na kunizungusha ndani ya chumba hicho, napatwa na woga lakini  napiga moyo konde naingia katika chumba hicho Tunaingia katika chumba hicho katika eneo la kwanza tunafika sehemu ya kuoshea maiti.

 

Tunangia ndani zaidi naona majokofu makubwa  ya kisasa yaliyohifadhi maiti, ananionesha vyumba mbalimbali kikwemo cha chakula mikutano na chumba cha katibu muhtasi wa chumba hicho.

 

Hapa niliwaona askari wa usalama barabarani wakitoa maelezo  kuhusu watu walifariki katika ajali. Gogo Mzome anaelezeka kazi hiyo kazi ya kutoa huduma mochari ni kazi kama kazi nyingine tofauti na watu wanavyofikiri huko mitaani.

 

Hiyo ni kauli ya Mhudumu wa Chumba cha Kuhifadhia Maiti katika Hospitali Taifa ya Muhimbili (MNH), Gogo Mzome, katika mahojiano na JAMHURI wiki iliyopita ofsini kwake.

 

Mzome ambaye ni Mkazi wa Wilaya ya Temeke  amesema anaipenda kazi hiyo na anaifanya kwa moyo, bila kushurutishwa na mtu au ugumu wa hali ya maisha.

 

“Kaka mkubwa, kifo cha baba yangu ndiyo kilichonifanya niipende kazi hii baba yangu Mzee Mohamed Mzome alifariki kwa shinikizo la damu mwaka 1980 nikiwa kijana wa miaka 25.

 

“Alifia katika mikono yangu, nikiwa nimemtoa nyumbani hadi Hospitali ya Wilaya ya Temeke nilikasirishwa na kitendo cha rafiki yake ambaye ni pia ni jirani yetu kwa kutotilia maanani kifo cha baba aliniambia nimuweka chini, yaani sakafuni nikaona hii si sahihi.

 

“Nilimbeba na kumuweka kitandani kisha kumtengeneza vizuri huku nikatoka kuwataarifu ndugu zangu na majirani wengine wakati nikitoka nje yule jirani yetu alitoa maneno ambayo sikuyaelewa nilikasirika sana ndugu zangu wakaja tukaendelea na msiba.

 

“Nikaona ni vizuri kuendelea kuwahudumia watu wanaopata matatizo kama haya, hili lilitokana na kupata uchungu baada ya kuona huduma niliyopata siku ya baba yangu alipofariki,” amesema.

 

Amesema aliendelea na tabia hiyo kwa  kuwa jirani zaidi na wafiwa kwa kushirikia kuosha maiti hadi ilipofika mwaka 1990.

 

Amesema aliandika barua ya kuomba kazi kama Mhudumu wa Chumba cha Kuhifadhia Maiti katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na kufanikiwa kupata kazi.

 

“Tuliomba kazi tulikuwa wengi lakini tuliopata tulikuwa watatu mimi na wenzangu wawili ambao ni Hamisi Kapongo na marehemu Sihaba Hussein Vumbi tukaungana na  watu wengine akiwemo Mkuu wa Kitengo cha Kuhudumia Maiti  marehemu Materu.

 

Amesema kuwa kazi hiyo ilikuwa siku ya kwanza baada ya Mkuu wa Kitengo Mteru aliwapeleka katika Chumba cha Kuhifadhia Maiti alifungua moja ya kabati lililokuwa na maiti.

 

Amesema kuwa baada ya kuona maiti nyingi alishindwa kujizuia aliogopa mno kwa kuwa hakuwahi kuona maiti nyingi wakati alizoea kuiona moja tu tena ya mtu aliyekuwa anamfahamu.

 

Amesema kuwa baada ya kuona maiti hizo miguu ilikufa ganzi, mkuu  huyo wa idara aligundua kuwa wanaogopa kuona maiti hivyo aliwatoa nje na kawapa kazi nyingine.

 

Amsema siku hiyo ilikuwa siku mbaya kwake alitamani kutorudi kazini siku ya pili lakini alipiga moyo konde na kurudi siku ya pili.

 

Mzome ambaye ni mjumbe wa siasa wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Kata ya 14 Temeke, amesema aliendelea na kazi hakuogopa.

 

Amesema kazi yake haitaji kunywa pombe au kuvuta bangi kwa ajili ya kuondoa woga kama ilivyoripotiwa kutoka mitaani.

 

“Watu wanasema kuwa ili kukaa katika chumba cha kuhifadhi maiti lazima uvute bangi huwezi mara utaambiwa kuwa maiti inanyanyuka, mtu kafa anawezaje kunyanyuka hayo ni maneno ya mitaani.

 

“Mimi kabla sijapanda cheo cha kuwa Mkuu wa Chumba cha Huduma ya Maiti nilikuwa nikilala usiku kucha na maiti zikiwemo tena kwa wakati huo hakukuwa na mazingira mazuri kama  ya sasa kuna majokovu  ya kuhifadhia maiti huzioni.

 

“Wakati huo maiti zilikuwa zinalala hovyo hovyo katika sakafu zikizidi unaziona maiti zimelala kila mahali ndani ya chumba lakini unalala nazo sijaona lolote kutokea.

 

“Kuna watu wengine wameendekeza ushirikina utakuta watu anakuja hapa kuchukua maiti yake mtu anaweka jiwe katikati ya jeneza hii ni imani tu  hakuna lolote,” amesema.

 

Amesema siku zote jamii imekuwa ikiwaona kuwa wao wamekuwa wakipata matatizo makubwa.

 

Mzome amesema  kila jambo zuri halikosi kasoro katika kazi katika kazi hiyo siku zote watu wamekuwa wakiamini kuwa watumishi wa kitengo hicho hujihusisha na uuzaji wa viungo vya binadamu.

 

Mtaalamu huyo anakanusha na kufafanua kuwa jambo hilo si kweli bali kinachofanyika ni kwamba wanapochoma sindano kwa ajili ya kuingiza dawa ya kuhifadhi maiti humpasua kwa sababu ya kutafuta mishipa.

 

“Kaka mkubwa maiti ni kitu kilichokufa hakina uhai damu haitembei hivyo sie humpasua ili kupata misuli itakayopitisha dawa sasa hapo hutegemea ni wapi umeipata lakini mtu anapokuja hapa na kukuta mwili umepasuliwa huanza maneno ya kuwa tumeiba viungo haya yote si sawa ni imani tu,” amesema Mzome.

 

Akizungumuzia mazingira ya kazi, Mzome amesema kuwa siku alipoona kazi hiyo ni ngumu ni pale ulipotokea mlipuko wa bomu katika Ubalozi wa Marekani.

 

Amesema ugumu wa kazi hiyo ulitokana na kuwa miili iliyofika katika ofisi yake ilikuwa imeharibika mno kiasi cha kushindwa kuhifadhiwa kwa kuwa ilikuwa vipande vipande.

 

“Siku ya Milipuko wa Ubalozi wa Marekani ilikuwa ngumu mno kwani miili ilikuja vipande vipande na hii ilitufanya kushindwa kuhifadhi vizuri miili na ugumu hasa ulikuja wakati wa utambuzi wa miili hiyo.

 

“Watu walishindwa kujua miili ya wapendwa wao anaweza kupata kichwa na sipate mwili mzima na mwingine anakuta anapata kiwiliwili  anatambua mwili wa mpendwa wake kutokana na nguo alizovaa lakini kichwa hakuna ilikuwa taabu sana,”  amesema.

Ubalozi wa Marekani ulilipuliwa Agosti 7, 1998 na watu 11 walikufa na 85 kujeruhiwa.

 

Mzome amesema tukio la pili ililompa taabu ni siku Ramadhan Seleman Mussa ‘Rama Mla Watu’ alipopatikana na kichwa cha mtu katika viwanja vya hospitali hiyo.

 

Hata hivyo, Rama pamoja na mama yake Khadija Ally Seleman waliachiwa huru na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam katika kesi iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Rose Temba.

 

Rama na mama yake walishtakiwa kwa kosa la mauaji ya mtoto Salome Yohana yaliyotokea mwaka 2008.

 

Kabla ya hukumu, Jaji Temba alipitia mwenendo mzima wa kesi hiyo na kubaini kwamba mshtakiwa namba moja (Rama) alionekana kuwa na hatia na kuzitaja sababu zilizomtia hatiani kuwa ni kukamatwa na kichwa cha mtoto huyo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na kiwiliwili chake kukutwa kwenye tundu la choo nyumbani kwa washtakiwa hao, Tabata jijini Dar es Salaam. Hali kadhalika, mwili huo wa Salome ulikuwa umeviringishwa na fulana ya Rama.

 

Jaji Temba alisema sababu nyingine iliyowatia hatiani Rama na mama yake ni maelezo ya Rama kuwa mama yake ndiye aliyemuua Salome kwa kumkata kichwa kwa kutumia shoka na kumpa kichwa hicho ili akipeleke kwa shangazi yake anayefanya kazi Hospitali ya Taifa Muhimbili.

 

Jaji Temba alisema licha ya ushahidi huo, alipitia maombi ya wakili wa washtakiwa hao, Yusuph Shekha aliyeomba mteja wake, Rama akapimwe akili.

 

Baada ya Rama kupelekwa katika Hospitali ya Mirembe mkoani Dodoma, jaji huyo alisema ripoti kutoka kwa Daktari Mndeme Erastus ilionesha kuwa wakati Rama akitenda kosa hilo alikuwa na matatizo ya akili.

 

Ripoti hiyo ilimfanya jaji huyo kuwafutia mashtaka washtakiwa hao kwa kuwa mshtakiwa wa pili aliingizwa hatiani kutokana na maelezo ya mshtakiwa wa kwanza.

 

Baada ya kutoa maelezo hayo, jaji huyo aliwaachia huru Rama na mama yake lakini aliamuru Rama awekwe chini ya uangalizi kwenye hospitali ya wahalifu ya Isanga mkoani Dodoma hadi akili yake itakapotengemaa.

 

Rushwa

Mzome amesema mazingira ya sasa hayaruhusu mtu kupokea rushwa kutokana na uongozi huo kuweka mambo kuwa ya uwazi zaidi.

 

“Mkurugenzi wa sasa ni makini lakini huduma imeboreshwa si kama zamani maiti inatafutwa katika faili, sasa mtu anakuja na kibali.

 

Tukiingia na kuangalia lebo tu unagundua kuwa kumbe  huyu ni John au Amani, unamtoa unampa mhusika aliyekuja na kibali si kama zamani utafute faili mara faili limehama sasa hakuna hiyo kaka mkubwa.

 

“Jambo lingine sie ni watu wa huruma hivi mtu nakuja hapa kafiwa utakuwa na hamu ya kudai rushwa huo utakuwa sio ubinadamu kabisa unatakiwa kufanya hivyo ukiwa na akili ya uwendawazimu,” amesema Mzome.

 

Alipoajriwa katika kitengo hiki cha kuhudumia maiti, hakutaka watu wafahamu wapi anapofanyia kazi. Awali, aliona ni kazi ya aibu. Hakuwaficha marafiki tu, bali  hata mkewe.

 

“Kila mara mke wangu aliponiuliza  nafanya kazi wapi nilimwambia kwa kifupi: Muhimbili. Lakini, baada ya kupita mwaka mmoja nikasema potelea mbali, na nikampasulia jipu,” amesema huku akiangua kicheko kikubwa.

 

Gogo Mzome  ni baba mtu mzima mwenye umri wa miaka 55 sasa, ana uzoefu wa hali ya juu katika kitengo cha kuhifadhi miili ya marehemu. Anatoa wito kwa Watanzania kuachana na dhana kuwa kazi hii ni ya fedheha.  Hii ni kazi kama kazi nyingine. Nisipofanya mimi atafanya nani?” anauliza Mzome.

 

Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Kitengo cha Kuhifadhia Maiti (Mochari), imekanusha habari zinazoenezwa mitaani kuwa kitengo hicho kinajihusisha na kuuza viungo vya binadamu.

 

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Huduma za Maabara, Dk. Emmaeli Moshi katika mahojiano na JAMHURI, wiki iliyopita.

 

Dk. Moshi amesema habari hizo ni uzushi na wala hazina ukweli wowote.

Katika mahojiano hayo, Dk. Moshi amesema kinachofanyika ni kuwa baada ya maiti kufikishwa mochari inafanyiwa uchunguzi na kuchomwa sindano kwa ajili ya kuihifadhi.

 

Amefafanua kuwa kwa kuwa maiti ni kitu kilichokufa damu yake haitembei mwilini hivyo hutafuta mishipa ambayo inaweza kupitisha dawa hata kama damu haitembei.

 

Amesema hutafuta sehemu mbalimbali  kitalamu kwa kupasua sehemu ambazo zinaweza kufanikisha zoezi hilo.

 

“Sasa  ndugu wa marehemu wanapofika kuchukuwa mwili wa mpendwa wao na kukuta mwili umepasuliwa hufikwa na wasiwasi na wengi hutoka hapo na kutangaza kuwa tunaiba viungo na kuviuza  jambo ambalo si sahihi,” amesema.

 

Amewataka ndugu wanaofika kuchukuwa miili ya  wapuuze habari hizo kwa kuwa ni za uzushi.

 

Mafaniko katika huduma ya kuhifadhi maiti

Dk.  Moshi ameliambia JAMHURI kuwa huduma katika chumba hicho zimeboreshwa.

 

“Kumekuwa na mafanikio makubwa katika utoaji wa huduma ya kuhifadhi maiti kutokana na ukubwa wa mji chumba hicho, kilizidiwa kutokana na kuwa na jokofu moja tu.

 

“Hii inatokana na kujengwa chumba chenye kufuata mfumo wa kisasa kwa kuongeza majokofu, chumba cha kwanza kilikuwa kidogo mno.

 

“Sisi kazi yetu kubwa ni kuhifadhi, kuandaa na kuchunguza, sasa kwa kuongeza vyumba vya kihifadhia maiti majokofu mengi ya kuweka miili, pia uwazi katika kutoa huduma umeongezeka,” amesema Dk. Moshi.

 

Amesema kutokana kuwa kuboresha huduma hizo sasa kitengo hicho kinafanya kazi kwa uwazi zaidi kwa kwa kuwa sasa wafiwa wanaruhusiwa  kuosha mwili wa marehemu na  kumpamba katika eneo hilo tofauti na zamani.

 

Amesema pia ndugu pia wanaruhusiwa kuona gharama kwa kuwa zimebandikwa katika kila kona za chumba hicho bila kificho

 

Matatizo

Dk. Moshi amesema pamoja na mafaniko hayo kuna matatizo ya uhaba wa wafanyakazi katika kitengo hicho kwa kuwa kazi hiyo ni ya wito na wenye wito ni wachache.

 

Amesema serikali sasa inatakiwa kuona kuwa kuna lazima ya kuandaa mitaala au kufungua chuo kitachokuwa kikifundisha watu watakaotoa huduma hiyo kwa kuwa sasa waliopo ni wakujitolea

 

“Serikali inatakiwa kutambua kuwa hii nayo ni taaluma kama ilivyo nyingine inatakiwa kuandaa mitaala au kufungua chuo kwa ajili ya  kufundisha wahudumu wa mochari kutokana na uhaba uliopo.

 

“Kwa sasa waliopo ni wa kujitolea na hapitia popote zaidi ya kuwapa mafunzo na kozi mbalimbali zinazotolewa hapa hospitali,” amesema Dk. Moshi.

 

Hata hivyo, Dk. Moshi anakerwa  na tabia ya watu kutojali wenzao wanaopotea na hawawatafuti pindi wanapoona hivyo.

 

Anashangaa kuona kuwa kuna maiti nyingi ambazo hazitambuliwi katika hospitali hiyo. Amesema hilo ni tatizo kubwa kutokana na maiti nyingi kutotambuliwa kwa muda mrefu.

 

“Nashindwa kuelewa hivi unaishi na ndugu yakoa au jamaa yako  anapotea lakini humtafuti hii ni hatari sana kuna maiti zinafikia hadi 30 kwa mwezi  zisizotambuliwa na ndugu zao hii ni tatizo kubwa kwetu.

 

“Maiti hizo zinatupa gharama kubwa kwa ajili ya kuzitunza na hata tunapowasiliana na Halmashauri ya Manispaa ya Jiji ambapo ndio mweye jukumu la kuwazika marehemu hao mara hutuambia kuwa hawana fedha, hivyo mtihani kuwa mgumu mno,” amesema.

 

Dk. Moshi ametahadharisha waendesha pikipiki kuwa makini katika uendeshaji wao kutokana na maiti nyingi kuhifadhia katika chumba hicho kuharibika katika maeneo ya vichwa hali inayowapa taabu wahifadhi.

 

Amewata waendesha bodaboda kuwapa wateja wao kofia ngumu wawapo safarini.

 

Naye Mkuu wa Kitengo cha Kuhifadhi Maiti katika MNH, Dk. Innocent Mosha anasema pamoja na  moyo wa ujasiri, kazi hiyo inahitaji uzoefu na umakini wa hali ya juu. Ukifanya uzembe kidogo tu unajitia matatani.

 

Kwa mfano, maiti za watoto wachanga mara nyingi huchanganya watu, utakuta wote wawili wana majina kwa mfano, Mwajuma Saleh, halafu wanafanana, basi hapo utata mzito hutokea.

 

Dk. Mosha anaongeza kuwa wahudumu wa chumba cha maiti hutumika pia kufanya uchunguzi katika miili ya marehemu wakishirikiana na madaktari.

 

Hali kadhalika anatoa wito kwa Watanzania kujenga tabia ya kuifanyia miili ya marehemu uchunguzi (postmortem) kabla ya kuzika.  Nia ni kujifunza na kupata ukweli wa chanzo cha kifo badala ya kuhisi.

 

1944 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!